Yah: Ninayo mengi ya kusimulia kwa nchi yangu ambayo naijua ndani nje, kinagaubaga

Nianze kwa kumshukuru tena Maulana jinsi ambavyo ananibariki kwa kuwa na maisha marefu na kuweza kuona maajabu mengi katika dunia hii, lakini kubwa zaidi ni dunia yangu ya Tanzania, hii ndiyo dunia ninayoijua mimi zaidi kwa kuwa katika maisha yangu ndiyo dunia ambayo nimeiishi na sijasimuliwa.

Naijua Tanzania kwa kadiri ya uelewa na uwezo wangu, naijua Tanzania kabla na baada ya kupata Uhuru, naijua Tanzania bila kusimuliwa, naijua kwa awamu zote na ninaijua kwa raha na taabu, naijua kwa shida na starehe, naijua kwa joto na baridi, naijua kwa njaa na shibe, naijua kwa uzalendo na ufisadi.

 Kama ingekuwa ni ndoa basi ningeweza kusema namjua mwenzangu vizuri kwa kipindi chote cha maisha yangu, kiufupi Tanzania ni nchi yangu naijua na sisimuliwi kuijua, ni nchi yangu ninayoweza kuisemea kifua mbele kuwa hii ndiyo Tanzania niijuayo mimi, sina mashaka yoyote na ukweli wa Tanzania yangu ninayoijua.

Nikitaka niwaandikie Tanzania yangu niijuayo hapa ninahitaji miaka kadhaa kuisemea nchi yangu, lakini itoshe tu kusema machache sana na madogo ambayo wengi hawaijui Tanzania kutokana na kuzijua nchi nyingine kwa kusimuliwa lakini Tanzania wanayoishi hawajui chochote.

Naijua Tanzania ya kabla ya uhuru, Tanzania ya watu milioni chache sana, Tanzania ya watu kudai uhuru kwa masikilizano, Tanzania ya kujitolea muda na kufanya siasa safi ya kudai uhuru. Tanzania ya kusikilizana baina ya raia wake, Tanzania ya umaskini na mali nyingi kushikwa na mkoloni, hiyo ndiyo ninayoijua kwa dhati ya moyo wangu.

Naijua Tanzania ya siku chache baada ya uhuru. Tanzania ya Watanganyika waliokuwa wengi hawajasoma sana, Tanganyika ya machifu na vinara wachache wa mali kutokana na umaskini wetu. Naijua Tanzania ya kuvumiliana na kutobaguana, Tanzania ya taifa na siyo rangi, Tanzania ya kwetu na siyo yao.

Naijua nchi yangu ya msimamo wa kisiasa barani Afrika na hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, naijua jinsi ilivyojitoa kuzikomboa nchi nyingine na hasa zilizotuzunguka, naujua mchango mkubwa tuliotoa ndani ya umaskini wetu mkubwa tuliokuwa nao, hatuna shule za kutosha, hospitali, barabara, viwanda na kadhalika.

Naijua nchi yangu baada ya maazimio mengi na utekelezaji wake, naijua Tanzania ya Azimio la Arusha na upokeaji mali kutoka kwa matajiri wachache na kuwa mali za Serikali, naijua nchi yangu kwa kuzingatia sheria ya utii katika zoezi hili, hivi siyo vitu vya kusimuliwa bali navijua kwa kuviona na kuvitekeleza.

Naijua Tanzania ya sogeza kwa nia ya kupata huduma muhimu kwa wananchi wake, naijua nchi yangu ya Muungano kwa kauli moja na utekelezaji wake, naijua nchi kwa ukarimu na unyenyekevu wa kweli kwa viongozi waliopewa dhamana, yapo mengi sana ya enzi hizo lakini yanahitaji miaka kuyasimulia.

Naijua nchi yangu kwa vijana wachache wachechefu wa tabia, viongozi vijana waliokuwa na tamaa ya mali na madaraka, nawajua waliokimbia kwa kuimbiwa nyimbo za kizalendo, nawajua wachache waliokuwa na tamaa na kutumika kutaka kuleta mapinduzi lakini kwa jinsi ninavyowajua Watanzania wa wakati ule walishindwa na kuishia kuwa watu wachache wasiolitakia mema Taifa hili.

Nawajua wananchi wa kweli wa Taifa hili lilipoingia katika vita nyingi ambazo wengi wetu siku hizi hawazijui, nalijua Taifa langu kwa vita ya ujinga, kutafuta silaha ya elimu kwa kujenga shule nyingi bila kutumia fedha bali nguvu zetu, naikumbuka vita hii kwa kujitolea mali na uwezo wa mtu bila kujali anatoka wapi na anakwenda wapi.

 

Naijua vita ya kilimo ilivyokuwa sanjari na uanzishaji viwanda ili tuzalishe mazao na kuyachakata hapa hapa nchini. Watu wengi tuliumia, viongozi wengi walijutia nafasi zao, wengi walifanya kazi kama mchwa na hiyo ndiyo iliyokuwa Tanzania ninayoijua mimi. Tanzania ya uzalendo, Tanzania ya kila mtu mchapakazi, Tanzania ya kutaka maendeleo bila siasa na Tanzania iliyojinasibisha na siasa ni kilimo cha kufa na kupona.

Ninayo mengi sana ya kusimulia kwa nchi yangu ambayo naijua ndani nje, Tanzania ambayo wengi wa kizazi hiki cha miaka 50 iliyopita hawaijui, naona ni busara nikaweka historia niijuayo kwa maana inawezekana ndiyo mipango ya Mwenyezi Mungu kuniweka hai ili niandike historia hii, sasa naanza.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.