Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ametoa wito kwa watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kampeni ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.

Zungu ameyasema hayo leo Oktoba 3, 2024 wakati akifungua semina kwa Shirika la Wanawake wenye ulemavu Tanzania (Vodiwota) ambayo imetolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Amesema kwamba takribani saizi ya viwanja vya Mpira milioni mbili vinapotea kwaajili miti kukatwa huku akifafanua kuwa matumizi ya kuni na mkaa kwenye kupikia ni sawa na kuvuta sigara 300 kwa siku.

“Kwa sababu hii Rais Dkt. Samia akaamua kusimamia zoezi la nishati safi ili kuepusha mambo haya…kwahiyo tumsikilize Rais wetu na tumuunge mkono katika zoezi hili kwa kumpamba, kumsemea, kumtetea pale anapokashifiwa na jamii, tuepuke na maneno mabaya ambayo yanasemwa kwa malengo ya kuchafua umoja wa taifa letu.

“Gunia zima la mkaa linauzwa Sh. 80,000 mpaka sh 90,000 sasa hivi kuna ukame mkaa umeshuka bei, mvua ikija mkaa unakwenda juu. Ukitumia mkaa unavuta sigara 300 kwa siku, kifua kinajaa na ukifika nyumbani huwezi kusoma magazeti na mzee,” amesema.

Aidha amewataka kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la kupigia kura ili kuweza kushiriki Uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Uchaguzi huu hautumii ile kadi ya Tume ya Taifa…bila ya kujiandikisha hupigi kura, sasa Mama Samia utampata vipi wakati hujamchagua Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa. Tumpambe Rais Samia kwa kuchagua wenyeviti wake wa serikali za mitaa,” amesema Zungu.

Meneja wa Ewura Kanda ya Mashariki, Nyirabu Musira amesema lengo la semina hiyo ni kuwapa mafunzo wanawake hao wenye ulemavu ili waweze kufahamu kuhusu matumizi ya nishati.

“Ewura tumealikwa na Vodiwota ambao wametaka kufahamu majukumu ya yetu na yana maslahi gani kwao. Kwahiyo tuko hapa kutoa elimu juu ya shughuli zetu, haki na wajibu wa mtumia huduma ambazo Ewura inasimamia, lakini vilevile masuala ya nishati safi ya kupikia.

“Tunafahamu ya kuwa serikali ina mkakati maalum wa kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo Ewura tuna wajibu kuhakikisha mkakati huu unatekelezeka,” amesema Musira.

Amefafanua kuwa, Ewura pia ina wajibu wa kuhakikisha walemavu wanapata huduma ambayo ni sawa na watu wengine bila kuwabagua au kuwatenganisha kutokana na hali yao.

“Kwa hiyo moja ya majukumu ambayo tunayo ni kuhakikisha mtoa huduma au yule ambaye tunamsimamia anaweka miundombinu ambayo itawasaidia hawa watu wenye ulemavu kuhakikisha wanapata huduma bora na kufikia mahitaji yao,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Vodiwota, Stella Jeirosi amesema lengo la kutaka kupata mafunzo hayo ya masuala ya nishati ni kumuunga mkono Rais Samia kwa kampeni anayoifanya ya kuhimiza jamii ya Watanzania kuachana na matumizi ya Nishati ambazo sio salama kwa Afya na ambazo zinaweza kuleta magonjwa mbalimbali.

“Kwahiyo kwa kuona hivyo na sisi kama Watanzania na ni sehemu ya jamii ambao tunatumia nishati tukaona ni vyema tumuunge mkono mama kwa kampeni hii ili watu wenye ulemavu waweze kutambua ubaya wa nishati ambazo sio salama kwaajili ya afya zao.

“Hivyo tukaamua tuwaombe Ewura watupatie mafunzo haya na tunawashukuru sana. Tunaamini matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu na endapo Watanzania tukizingatia tunakuwa na afya bora na kuokoa misitu ambayo inateketea kwaajili ya kukata miti ili watu watengeneze mkaa au kupikia Kuni,” amesema Stella.

Please follow and like us:
Pin Share