Alhamisi usiku Desemba 5 mwaka huu, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, alitangaza kifo cha Rais wa kwanza mweusi nchini humo, Nelson Mandela, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.
Akiutangazia ulimwengu na wananchi wa Afrika Kusini kuhusu kifo hicho, Rais Zuma amesikika akisema, “Mpendwa wetu Nelson Rolihlahla Mandela, mwasisi wa taifa letu la kidemokrasia, ameaga dunia. Ameondoka kwa amani akiwa na familia yake saa 2:50 usiku kwa saa za Afrika Kusini (kwa saa za Afrika Mashariki ni saa 3.50). Kwa sasa anapumzika. Kwa sasa ana amani.
“Taifa letu limempoteza mtoto wake mkuu wa kiume. Watu wetu wamempoteza baba. Licha ya kwamba tulifahamu kuwa siku kama hii ingemtokea, hakuna kinachopunguza upendo wetu kwake na hasara kubwa tuliyopata. Jitihada zake kutafuta uhuru zimemjengea heshima kubwa duniani.
“Unyenyekevu wake, upendo wake na utu wake, vimesababisha watu kumpenda. Mawazo yetu na sala zetu tunazielekeza kwa familia ya Mandela. Kwao tuna deni kubwa la kuwashukuru. Walijitolea kwa kiasi kikubwa na kuvumilia mengi ili watu wetu wawe huru. Amesema Zuma.
“Mawazo yetu yapo pamoja na mkewe, Graça Machel, mke wake wa zamani Winnie Madikizela-Mandela, pamoja na watoto wake, wajukuu wake na familia nzima. Mawazo yetu yapo pamoja na rafiki zake, marafiki katika mapambano na washirika wake walioshirikiana na Madiba katika mapambano ya ukombozi.
“Mawazo yetu yapo pamoja na wananchi wa Afrika Kusini ambao leo wanaomboleza kifo cha mtu, ambaye zaidi ya wengine amekuja kuleta hisia ya taifa moja. Mawazo yetu yapo pamoja na watu duniani kote ambao wamemkumbatia Madiba kama mtu wao, na ambaye aliona matatizo yao ni yake. Taifa letu limempoteza mtoto wao muhimu sana.
“Kile kilichomfanya Nelson Mandela kuwa kiongozi mkuu ni kile hakika kilichomfanya awe na utu. Tumeona ndani yake kile tunachokitafuta ndani mwetu. Na ndani yake tumeona mengi tunayohitaji.
“Ndugu zangu Afrika Kusini, Nelson Mandela alituleta pamoja na pamoja tunamuaga.
“Mpendwa wetu Madiba atapewa mazishi ya kitaifa. Nimeshaagiza kuwa bendera zote nchini Afrika Kusini zitapepea nusu mlingoti kuanzia tarehe 6 Desemba na kubakia hivyo hadi baada ya mazishi yake.
Wakati tukikusanyika kutoa heshima zetu za mwisho, hebu twende kwa utu na heshima ambayo Madiba alijijengea. Hebu tufikirie matarajio yake na matarajio ya familia yake.
“Tukiwa tumekusanyika, popote tulipo duniani, tukumbuke mambo ambayo Madiba alipigania. Hebu tuthibitishe dira ya jamii, ambayo ndani yake hakuna anayenyonywa, kukandamizwa au kunyanyaswa na mtu yeyote.
“Hebu tujibidiishe bila kupoteza nguvu kujenga Afrika Kusini yenye umoja, isiyo na ubaguzi wa rangi, isiyo na ubaguzi wa kijinsia, Afrika Kusini ya kidemokrasia na ustawi. Hebu tueleze kwa namna yetu wenyewe, shukrani kubwa tuliyonayo kwa mtu ambaye ametumia muda mwingi kuwatumikia watu wa nchi hii na kwa minajili ya utu. Huu kwa kweli ni wakati wa masikitiko makubwa. Lakini lazima pia uwe wakati wa maana kwa yale tuliyodhamiria.
“Dhamira ya kuishi kama alivyoishi Madiba, kupambana kama Madiba alivyopambana na bila kupumzika hadi tutakapofikia kile alicholenga katika kujenga Afrika Kusini yenye umoja, Afrika yenye amani na ustawi na dunia bora zaidi. Daima tutampenda Madiba! Roho yako ipumzike kwa amani. Mungu Ibariki Afrika.
Salama za rambirambi
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma kutokana na kifo cha Rais Mandela.
Katika salamu zake amesema: “Mwangaza mkuu umetoweka duniani. Nelson Mandela alikuwa shujaa wa wakati wetu.”
Bendera katika ofisi za waziri mkuu zinapeperushwa nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kumheshimu.
Cameron anasema, “Kukutana naye lilikuwa moja ya mambo ya heshima kubwa katika maisha yangu. Moyo wangu umeelekezwa kwa familia yake na kwa watu wote nchini Afrika Kusini na kwingineko duniani”.
Rais Barrack Obama
Rais Obama katika salamu zake za rambirambi amemtaja Nelson Mandela kuwa ni mmoja wa watu wenye ushawishi zaidi, jasiri na mtu mwema kuwahi kuishi.
“Amepata zaidi ya kile kilichotarajiwa kutoka kwa mtu yeyote. Leo amekwenda nyumbani,” Obama akiwa amegubikwa na majonzi amesema katika taarifa aliyoitoa Ikulu ya Marekani.
“Si wetu tena. Ni wa vizazi vyote,” amesema Obama.
Rais Obama alitaka bendera zote nchini humo kupeperushwa nusu mlingoti hadi jana jioni, ili kutoa heshima kwa kiongozi huyo mpinga siasa za ubaguzi wa rangi.
Rais wa zamani wa Marekani, George H. W. Bush, alielezea mshangao na kuona mtu wa aina yake Nelson Mandela kwa kuwa na uwezo wa kusamehe watu waliomfunga miaka 27 jela bila makosa, akitoa fundisho kwa sisi sote kuweza kusamehe hata maadui zetu.”
Rais mwingine wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, amesema marehemu Mandela atakumbukwa kama kinara wa utu wa binadamu na uhuru kwa amani na maridhiano.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemtaja Nelson Mandela kama mtu “mnyenyekevu na mfano wa kuigwa na binadamu.
Nelson Mandela alikuwa mtu wa aina yake duniani, mtu mwenye utu na aliyefikia mafanikio ya juu, mwamba wa haki na mnyenyekevu.
“Nimesikitishwa sana na taarifa za kifo chake. Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa ningependa kutuma rambirambi zangu kwa watu wa Afrika Kusini na hususan familia ya Nelson Mandela na wapendwa wake.
Rais Xi Jinping wa China
Katika salamu zake, Rais Xi Jinping wa China ameeleza kusikitishwa kwake na kifo cha Nelson Mandela, na kuitakia subira familia ya Nelson Mandela.
Xi amesema wananchi wa China daima watakumbuka mchango usio wa kawaida wa Mandela katika kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika Kusini kwa maendeleo ya watu wa nchi mbili hizo.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania
Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema; “Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21. Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwanamapinduzi, mvumilivu na mstahimilivu,” amesema Kikwete.
Rais Kikwete amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
“Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa. Ni wajibu wa wananchi wa Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake,” amesema.
Rais ameongeza kusema; “Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mandela Mahali Pema Peponi”.
Rais Kikwete ametangaza siku tatu za maombolezo na bendera zimepeperusha bendera nusu milingoti kwa siku tatu kati ya Desemba 6-8, 2013 kumuenzi Rais Mandela.
Rais Uhuru Kenyatta
Rais Kenyatta amesema kwamba amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ‘shujaa’ Nelson Rolihlahla Mandela.
Amesema kwa niaba ya serikali na watu wa Jamhuri ya Kenya, ameelezea masikitiko makubwa kwa familia na marafiki wa Nelson Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, huku akiwataka wananchi wa Afrika Kusini kuwa na moyo wa uvumilivu katika wakati huu mgumu.
Rais mstaafu Mwai Kibaki
Rais Kibaki amesema wakati dunia inapata habari za kusikitisha za kifo cha Nelson Mandela, Afrika itakuwa inasherehekea kuwa na kiongozi wake shupavu katika karne ya 20 na 21.
Amesema Mandela alishinda ubaguzi wa rangi na kufafanua maana halisi ya uhuru na kuchochea viwango vipya vya utu wa Kiafrika na undugu. Alikuwa mfano bora wa matumainiwa na dunia iliyo na usawa.
Raila Odinga
Odinga amesema Nelson Mandela anasema ni mmoja wa binadamu wachache ambao wanaangalia mbele, na unakutana nao mmoja katika karne moja au kizazi kimoja na pale tu tunapokuwa tumebahatika kuwapa watu wa aina hiyo.
Alikuwa mstahamilivu, shupavu, mnyenyekevu, mwenye kujaa matumaini na mvumilivu. Tuna bahati kwamba tumeishi na kumshuhudia akipata umaarufu na kuwa mfano angali hai.
Rais Yoweri Museveni
Rais Museveni amesema Mzee Mandela, Oliver Tambo, Govan Mbeki na wengine walijitolea maisha yao na ujana wao wote katika kupigania haki na kuikomboa Afrika Kusini. Walijivunia kweli walichoamini na wakatekeleza. “Sasa ni jukumu letu na wadogo wetu kuendeleza kazi ya Mandela,” alisema.
Rais Joyce Banda
Rais Banda wa Malawi amesema; “Wakati kama huu, sote tumepata mshtuko. Si kuwa hatukujua kitatokea, lakini ni huzuni kwa tulichopoteza. Ningependa kuelezea masikitiko yangu kwa kumpoteza kijana wa Afrika, Dk. Nelson Mandela, kwa sababu vita aliyopigana si tu dhidi ya ubaguzi wa rangi, bali ni vita dhidi ya unyanyasaji wa kila aina dhidi ya binadamu.
“Na ndiyo maana vijana, na wazee, wake kwa waume, weupe na weusi, tajiri na masikini wote wamejihusisha na yeye na vitu alivyopigania.”
Waziri Mkuu Manmohan Singh
Singh, Waziri Mkuu wa India, amesema; “Kifo cha Mandela. Huyu alikuwa mwakilishi wa utu duniani. Pia amekuwa chanzo cha matumaini kwa wengine wengi ambao wanakabiliana na unyanyasaji na kunyimwa haki, hata miaka yote hiyo baada ya kuwakomboa watu wake mwenyewe.
“Katika ulimwengu uliogubikwa na migawanyiko, amekuwa mfano mwema wa utangamano na sioni uwezekano wa kupatikana mwingine kama yeye katika miaka mingi ijayo.”
ICC yamlilia Mandela
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko The Hague, Uholanzi, imeungana na watu wa Afrika Kusini, Bara la Afrika na jumuiya ya kimataifa kuomboleza kifo cha jabali wa Afrika, Mzee Nelson Mandela, aliyekuwa sauti ya usawa na haki.
ICC imesema ni wakati utawala wa Mandela Julai 17, 1998 Afrika Kusini ilikuwa miongoni mwa mataifa 10 ya mwanzo kutia saini mkataba wa Roma kuhusu Mahakama hiyo.
Mandela alisema bara la Afrika limeteseka vya kutosha na ukiukwaji wa haki za binadamu na vyombo kama ICC vingekuwapo labda mateso hayo yasingekuwapo.
Mandela alifuata maadili
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema kwamba Mzee Madiba anatambulika kama kinara wa uhuru, usawa na haki za binadamu.
Ameongeza kuwa Mandela ndiye kiongozi anayefuata maadili kuliko mwingine yeyote katika kizazi hili.
“Aliamini katika haki za binadamu kwa wote, alichagiza haki za wanawake, usawa kati ya wanawake na wanaume na kuwawezesha wanawake kushika madaraka.