Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

HATUA zilizochukuliwa na serikali za kulinda soko na kudhibiti uingizai holela wa matunda nchini, umeongeza uzalishaji wake kutoka tani 6,530,302 mwaka 2022/2023 hadi tani 7,065,139 kwa mwaka 2024/2025.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde jana bungeni.

Alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Husna Sekiboko (CCM) aliyeuliza: “Je, serikali inachukua hatua gani kulinda kilimo cha matunda nchini ili kuokoa Soko la Matunda linalosuasua kutokana na uingizaji mkubwa wa matunda”.

Silinde alitaja hatua zilizochukuliwa na serikali katika kulinda soko na kudhibiti uingiaji holela wa matunda nchini ni kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ambayo inaweka utaratibu wa kuwezesha uingizaji na usafirishaji nje wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko, yakiwemo matunda.

Pia, kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kusindika matunda ili kuimarisha soko la ndani na kupunguza upotevu.

“Kutoa ruzuku ya pembejeo kwa mazao ya matunda ikiwemo maembe, machungwa na parachichi ili kuongeza tija,” alisema.

Pia, kuimarisha utafiti na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya matunda kulingana na mahitaji ya soko.

Katika swali la nyongeza, Sekiboko aliuliza, “Mkoa wa Tanga maarufu kwa kilimo cha matunda hasa machungwa lakini machungwa hayajapata soko viwandani, mkakati ni upi kurejesha kilimo cha matunda na kupata masoko viwandani?”.

Pia, aliuliza mkakati wa serikali ni upi kujenga vyumba baridi kuhifadhi matunda maana mengi hasa machungwa yanaoza.

Silinde alijibu serikali inahamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vidogo kuongeza thamani kama kutengeneza juisi na tayari wamepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kujenga vyumba baridi.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Anastazia Wambura (CCM) katika swali lake la nyongeza alitaka kujua mkakati wa kuzuia uletaji matunda yasiyokomaa sokoni.

Silinde alisema huwa wanachukua hatua kwa wanaobainika na imewahi kutokea mfanyabiashara aliyepeleka parachichi sokoni ambazo hazijakomaa, walimfutia leseni ya kutoshiriki biashara ya mazao.

“Tunaendelea kufuatilia wote wanaopeleka matunda sokoni yasiyokomaa ili hatua zichukuliwe,” alisema.