NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa Ziwa Tanganyika kuendelea kulinda ziwa hilo ili lisaidie katika shughuli za kijamii.

Amesema katika jitihada za kulinda ziwa hilo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kuhifadhi mazingira ya ziwa hilo kwa kushirikiana na nchi wanachama ili kuleta maendele endelevu

Khamis ameeleza hayo alipokuwa akizungumza wakati wa Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Usimamizi wa Ziwa Tanganyika (LTA) uliofanyika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Kinshasa.

Amesema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kwa wananchi kwani takriban wananchi milioni 13 wanalizunguka na kulitumia kufanya shughuli za kujipatia kipato kama vile uvuvi, kilimo, ufugaji na uchimbaji madini.

Naibu Waziri Khamis amefafanua kuwa licha ya manufaa hayo kwa binadamu, shughuli zisizo endelevu zimekuwa na athari mbaya katika ubora wa mazingira ya ziwa ikiwemo uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa ziwa kutokana na utupaji unaoendelea wa uchafu wa majumbani na viwandani ndani ya ziwa.

Ameongeza kuwa matumizi ya kupita kiasi ya kemikali za kilimo ndani ya bonde la ziwa yanatishia mazingira hivyo zinahitajika nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo

Naibu Waziri Khamis amesema ili kuboresha mazingira ya ziwa na maisha ya wananchi kwa ujumla kuna haja ya kutumia mikakati ya maendeleo endelevu kama ajenda muhimu ambayo Tanzania inatekeleza.

“Tunaamini kwamba, kupitia juhudi hizo za ushirikiano tunaweza kuimarisha lengo letu la pamoja la usimamizi shirikishi na endelevu wa maliasili pamoja na kuboresha hali ya maisha ya watu katika ziwa na bonde lake,” amesisitiza.

Pia, ameahidi kuwa Tanzania itashirikiana na nchi nyingine tatu zinazozunguka ziwa hilo katika utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za pamoja za ziwa na kuboresha maisha ya jamii katika bonde la ziwa.

Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo wa LTA umewakilishwa na Naibu Waziri Khamis aliyeambatana na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Viongozi wengine walioshiriki ni Waziri Mkuu wa DRC, Judith Suminwa Tuluka, Waziri wa Uchumi wa Kijani na Mazingira wa Zambia ambaye pia ni Mwenyekiti wa LTA, Mike Mposha, Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa DRC, Jean Pierre Tshimang, Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi,  Emmanuel Ndorimana na Katibu Mtendaji wa LTA, Tusanga Mukanga Sylvain.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Ziwa Tanganyika inaundwa na nchi nne zikiwemo Tanzania , Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zambia ambayo kwa sasa ndio inashikilia uenyekiti.