Na Albano Midelo,JamhuriMedia,Ruvuma
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA nchini Mhandisi Clement Kivegalo amesema yeye ndiye aliyesimamia mradi mkubwa wa maji kuyatoa ziwa Viktoria na kuyapeleka kwenye mikoa yenye uhaba wa maji
Amesema mradi kama huo unaweza kufanyika katika ziwa Nyasa na kupunguza uhaba wa maji nchini.
Mhandisi Kivegalo amesema hayo wakati anazungumza baada ya kukagua mradi mkubwa wa maji wa Mwerampya Kata ya Lituhi Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 6.4.
“Mimi ndiye nilisimamia mradi wa kuyatoa maji Ziwa Viktoria kuyapeleka Shinyanga,Kahama,na sasa yamefika Tabora,Igunga,Nzega na Sheluwi na yataenda Sikonge,Urambo na Kariua”,alisema.
Mhandisi Kivegalo amesema maji haya yametoka kwenye plant moja hivyo serikali inaweza kutekeleza mradi kama huu kwenye Ziwa Nyasa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ameipongeza RUWASA kwa kutekeleza miradi mikubwa miwili ya maji katika Kata za Lituhi na Liuli yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11 .
Amesema miradi hiyo ambayo inatarajia kukamilika Aprili 2023 inakwenda kumaliza changamoto ya maji katika vijiji 13 vilivyopo kwenye mradi.
Hata hivyo amesema Wilaya ya Nyasa ina vyanzo vingi vya maji likiwemo Ziwa Nyasa ambalo linaweza kumaliza changamoto ya maji katika Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani.
Mhandisi Manyanya anaunga mkono wazo la kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Nyasa na kuyapeleka maji hayo katika maeneo mengine yenye uhaba wa maji nchini.
Ziwa Nyasa ni miongoni mwa maziwa makubwa matatu nchini,Ziwa hili linatumiwa na nchi tatu za Tanzania,Malawi na Msumbiji.