KIONGOZI mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amehudhuria muendelezo wa kesi zinazopinga matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, zilizofunguliwa na chama hicho katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Mahakama ya Wilaya ya Hakimu Mkazi Kigoma, Zitto amelaani vitendo vya serikali vinavyokwamisha mwenendo wa kesi hizo kwa kuweka mapingamizi yasivyokuwa na msingi, ili kuchelewesha mchakato wa kusikiliza mashauri ya msingi.

Zitto amemtaka Jaji wa Mahakama Kuu kutoa wito kwa serikali kuacha kuingilia uhuru wa mahakama na kusababisha kucheleweshwa kwa haki.

“Kuna vipingamizi vya ajabu vinavyowekwa kwenye kesi hizi kwa makusudi, ili kuzuia haki ya wananchi kutendeka,” amesema Zitto.

Katika Mkoa wa Kigoma, ACT Wazalendo imefungua kesi 13 za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

Hadi sasa, kesi hizo zimekuwa na mapingamizi mengi, lakini chama hicho kimefanikiwa kushinda mapingamizi katika kesi moja kufikia leo huku mapingamizi mengine yakiendelea kusikilizwa.

Zitto aliongeza kuwa, ACT Wazalendo haitosita kufuata haki hadi ngazi za juu za mahakama, ikiwa haki haitapatikana katika ngazi za chini.

“Tutahakikisha tunasimamia haki za wananchi, kurudisha heshima kwa kura zao, na hatutakubali kuona haki inapotewa au kupuuzwa,” amesema Zitto.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa chama cha ACT Wazalendo kitasimamia haki za wananchi kwa nguvu zote na kwamba vita hii ya kutetea haki za wananchi na kulinda demokrasia itakwenda mbele bila kukata tamaa.