Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamisi wiki iliyopita yameibua hoja mbalimbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi; na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli waNishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndiyo chanzo cha maandamano haya. Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu, bali pia katika sekta nyingine ambako tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM.
Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha Taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngome ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala, basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona. Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa Jeshi la polisi, wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini? Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini.
Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya gesi yatumike Mtwara tu, la hasha. Si dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya.
Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao . Kwanini tuwasute na kuwasurubisha kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa Kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya fedha za kigeni?
Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe fedha za mkonge na kahawa. Mbona hataji fedha za korosho? Mwaka 2011 korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya tumbaku. Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za mkonge? Walifaidi fedha za kahawa? Wamefaidi fedha zao za korosho?
Tumesahau hata reli iliyoachwa na mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania ? Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuza dhahabu ya thamani ya dola bilioni 3.3 za Marekani bilioni.
Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye gesi asilia. Mtwara na Lindi wanakosea wapi? Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono.
Lakini kuna mahala lazima waelimishwe. Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana .
Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho.
Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na gesi yao . Nguvu ya mnyonge ni umoja. Serikali isiyosikia. Serikali ina hoja kuhusu kujenga bomba la gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania.
Kwa kuwa hii asilimia 14 ndiyo wenye sauti, basi watu wa Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa bomba? Tunaambiwa na wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7(block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke.
Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar es Salaam karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija? Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar es Salaam dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania ?
Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera? Leo bwawa laMtera lisipozalisha megawati moja hata Dar es Salaam izalishe megawati elfu kumi, umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara? Tuwasikilize watu wa Mtwara Watanzania siyo mabwege tena.
Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya gesi likiwamo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia.
Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa gesi bila kuathiri umoja wa Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia rasilimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima. Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu (Chadema) ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini.
Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera. Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea mwaka 2015 na tukishika dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo katika suala la gesi tu, bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi.
Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.