Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waajiri na waajiriwa wametakiwa kuzingatia kuwa mahali pa kazi panakuwa salama kwa afya ya macho wakati wote ili kuleta ufanisi mzuri katika kazi zao.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga na Muuguzi Mkuu wa Serikali Ziada Sellah katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani yanayofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Ziada amesema wito mkubwa katika maadhimisho haya ni kila waajiri na waajiriwa kuzingatia kuwa mahali pa kazi panakuwa salama kwa afya ya macho wakati wote.
“Hakikisheni kanuni ya 20/20/20 inatumika mahala pakazi yaani, kila baada ya kutazama skrini kwa dakika 20, mtu anapaswa kupumzika kwa sekunde 20 pia kuangalia kitu kilicho umbali wa futi 20. Hii ni pamoja na matumizi ya simu, kompyuta, vishikwambi na kwa wale wanaotazama runinga” amesema Ziada.
Amewataka wananchi kujikinga wasipate matatizo ya macho kwa kujiepusha na ajali sehemu za kazi yaani ofisini, shambani, barabarani, shuleni na sehemu zinginezo za kazi kwa kuvaa vitendea kazi sahihi.
Aidha, Ziada amewasihi wananchi kupima afya zao za macho mara kwa mara angalau mara moja kwa mwaka kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya ya macho.
“Tumesikia kuwa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za halmashauri vituo vya afya na zahanati zinatoa huduma za macho kwahyo ukiona umepita mwaka basi usisite kwenda kupima afya ya macho” amesisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Mwinyi Kondo amesema Serikali imejitahidi kuhakikisha upatikanaji wa huduma za macho zinapatikana kwani inaonekana kuna idadi kubwa ya wagonjwa nchini.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwa na ongezeko la asilimia 10 katika upatikanaji wa Huduma za Macho nchini kutoka asilimia 74 mwaka 2018 hadi asilimia 84.4 mwaka 2022, hii imesababishwa na wananchi wengi kuhitaji huduma hizo”. amesema Dkt. Kondo.
Nae Meneja Mpango wa Taifa wa huduma za Macho Dkt. Bernadetha Shilio amesema siku ya afya ya macho ni maalum kwa waajiri na waajiriwa, mpango wa Taifa wa Huduma za Macho ulikusudia kufikisha ujumbe muhimu wa kulinda afya ya macho mahala pa kazi.
“Kwa kufuata hili tumeweza kuendesha kampeni ya uelimishaji wa afya ya macho kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa sambamba na kuwachunguza wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi na vituo vya tiba”. amesema Dkt. Shilio.