Mkuu wa Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Volker Turk, amekaribisha uamuzi wa Zimbabwe wa kufuta hukumu ya kifo na kutoa wito kwa nchi nyingine kuchukua hatua kama hiyo.

Mapema wiki hii, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa alitia saini sheria ya kuondoa adhabu ya kifo, hatua itakayobatilisha adhabu za takriban wafungwa 60 ambao walikuwa wakikabiliwa na adhabu ya kunyongwa.

Kulingana na sheria hiyo ya kukomesha adhabu ya kifo, mahakama nchini Zimbambwe hazitoweza tena kutoa hukumu ya kifo na adhabu zozote za kifo zilizokwisha tolewa zitapaswa kubadilishwa kuwa kifungo jela.

Shirika la kutetea haki zabinaadamu la Amnesty International nalo limepongeza uamuzi huo likisema unatoa matumaini ya kuondoa kabisa hukumu hiyo katika kanda nzima.