Mpendwa msomaji, najua juma lililopita vyombo vya habari vilitawaliwa na mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi. Nawashukuru wanahabari kwa mshikamano waliouonesha nchi nzima kwa maandamano, wanahabari tuendelee hivi hivi bila kutetereka.
Narudia, tumezichoka kauli za kwamba baadhi ya watu wameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali au kitu kizito. Polisi sasa lazima wawe na adabu. Polisi lazima waheshimu uhai wa binadamu. Kumwaga damu kamwe haiwezi kuwa sifa.
Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 inazuia mauaji. Nadhani Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na wasaidizi wake wote waliokuwapo katika siku ya tukio inabidi wakamatwe mara moja. Polisi hawawezi kusema mara hii wamepata utaalamu wa ajabu na kubaini kwa uhakika kuwa Kamuhanda na wenzake hawakushirikiana na hicho “kiaskari” kinachodaiwa kumuua Mwangosi.
Kwa kipigo alichoshushiwa Mwangosi ni mahakama pekee ndiyo yenye uwezo na mamlaka ya kutafsiri iwapo mawazo ya askari hawa (mens rea) na matendo yao (actus reus), walioshiriki kumpiga Mwangosi inapaswa kuchunguzwa, na pia ni mahakama pekee yenye uwezo wa kutamka kuwa hawa wengine wasiofikishwa mahakamani hawakushiriki moja kwa moja (accessories to the crime) katika mauaji haya.
Sitanii, kwa sheria za Uingereza tunazozitumia hapa nchini, unapotokea uhalifu kama mauaji yaliyofanyika kwa Mwangosi, uchunguzi hauishii katika kutafuta nani aliyeua hasa, bali unahusisha pia wote walioshiriki uhalifu huu kabla ya tukio (accessory before the facts) na wale walioshiriki baada ya uhalifu kutendeka kama kumficha mhalifu au kuficha taarifa ambazo zingeweza kusaidia haki kutendeka (accessory after the facts).
Ni kwa mantiki hiyo, nasema Kamuhanda na wale askari tunaowaona kwenye picha wakimshushia kipigo Mwangosi, wanazo taarifa muhimu na wanawajibika katika kuhakikisha haki inatendeka. Inawezekana huyu askari aliyefikishwa mahakamani ndiye aliyekuwa ameshikilia mtutu uliofyatua bomu lililoua, lakini ukweli halisi unapaswa kupatikana kwa kuwakamua akina Kamuhanda waeleze iwapo hawakuwa na nia sawia na huyu askari anayeshitakiwa.
Kichwa cha makala haya kinasema Zijue amri 10 za kujihakikishia umasikini milele. Ni kutokana na uchungu wa kifo cha Mwangosi, nimejikuta nalazimika kuanza na mada hiyo, lakini kimsingi leo nilinuia kuwaasa ndugu zangu Watanzania kuchagua njia sahihi ya kuendesha maisha yao. Najua bado tunayo dozi kubwa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Sitanii, nafahamu kuwa Watanzania wengi tukipita mijini na kuona majengo ya National Housing Corporation (NHC) tunatembea kifua mbele tukijisifu na kuridhisha nafsi zetu kuwa hizo ni mali zetu. Ndiyo maana shirika kama la Umeme Tanzania (TANESCO) hatusiti kila kukicha kusema – tena kifua mbele – kuwa ni mali yetu sisi Watanzania. Hali ilikuwa hivyo hivyo enzi za TTCL au Posta na Simu na tulikuwa tukiyaona mashirika haya ya umma kuwa ni mali yetu.
Natumia neno ‘mali yetu’ kwa makusudi maana nashuhudia watu wengi wanavyohamasika pale shirika la umma linapotangaza kupata faida. Ndiyo maana leo tunajikuta Watanzania tunasononeka kupita kiasi pale Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inapopata hasara, kwa kauli moja tunasema shirika (kampuni) letu.
Ingekuwa ninaandika kwa kimombo makala haya ningesema hivi: Gone are those days (ya kale yamepita). Fungukeni Watanzania. Acheni kuwaza Kijamaa, wazeni Kujitegemea. Enzi za shirika letu, hospitali yetu, shule yetu, maji yetu, madini yetu, mafuta yetu na mengine yawayo zinapita kwa kasi. Mafuta yaliyopo chini ya ardhi yanahitaji mtaji wa kuyachimba.
Sitanii, tunachoweza kufanya kama taifa ni kuhakikisha tunayo Serikali makini na sikivu itakayoweka sera na kutunga sheria kali zinazodhibiti wasiolipa kodi. Serikali zote duniani hazifanyi biashara zaidi ya kukusanya kodi. Hata hizo nchi zinazochimba mafuta – wanaochimba ni watu binafsi kupitia kampuni walizozisajili isipokuwa Serikali zinapata kodi na gawio kulingana na hisa ilizonazo kwenye kampuni za uchimbani.
Katika somasoma yangu, nimekutana na maandiko haya yaliyopo katika lugha ya kimombo ila nayatafsiri (tafsiri hii ni yangu). Yanahusiana na amri 10 za kujihakikishia umasikini wa kudumu katika familia yako:-
1. Milele usiamke asubuhi na mapema: Kaa kitandani ukijinyoosha na kujigeuza hadi upate njaa na kuendelea kusinzia. Kama kitanda hakina kunguni haraka ya nini kuamka alfajiri?
2. Kamwe usiwe na mipango ya jinsi ya kutumia fedha zako: Unapopata fedha anza kuzitumia mara moja na zikiisha anza kuhesabu na kukumbuka ulivyozitumia. Usiwe na bajeti milele.
3. Kuwa mshindani: Hakikisha unavaa nguo za kisasa na kujipulizia pafyumu za bei ghali kuliko mfanyakazi yeyote ofisini kwako. Wasengenye majirani zako mara nyingi kadri inavyowezekana. Jirani au rafiki yako akinunua simu mpya, gari au nguo, wewe hakikisha unanunua ya bei kali zaidi kuliko yake.
4. Kamwe usifikirie kuweka akiba hadi utakapopata fedha za kutosha: Unawezaje kuweka akiba wakati unapata fedha kidogo kiasi hicho? Wanaokwambia uweke akiba hawakuhurumii au hawajui matumizi muhimu uliyonayo!
5. Usijihusishe katika masuala ya kijamii wanayofanya watu wasio wasomi: Iweje wewe mhitimu wa chuo kikuu ufanye biashara ndogo ndogo kama kuuza maandazi, sabuni au mafuta ya kupima kwa koroboi msomi wewe? Iweje wewe tajiri unayemiliki gari zuri likiharibika upande daladala. Kodi teksi daladala si saizi yako. Hayo waachie ambao hawajakwenda shule.
6.Usifikirie kuanzisha biashara hadi malaika kutoka mbinguni akuletee mtaji: Jamii inatarajia wewe uwekeze nini kabla hujapata mamilioni ya shilingi? Hata kama biashara nyingi mtaani kwako zimeanzishwa kwa mitaji midogo midogo, wewe msomi mwenye akili unaweza kuanzisha biashara pale tu unapokuwa na mamilioni. Usihangaike na vimikopo vidogo vidogo ni kujitia aibu.
7. Laumu kila kitu isipokuwa mtizamo wako: Ilaumu Serikali, laumu mfumo na zilaumu benki zinazokataa kukopesha fedha. Vyombo vyote hivi ni vibaya havitaki uwe tajiri. Yakiitishwa maandamano ya vyama vya siasa shiriki maandamano yote asubuhi mpaka jioni ukiimba nyimbo za ukombozi. Ikiwezekana usitenge muda wa kufanya kazi zako binafsi kujiletea pato, shiriki maandamano kuanzia Jumatatu hadi Jumapili na kwa miezi sita utakuwa umefanikiwa kujipatia umaskini wa kudumu.
8. Tumia zaidi ya kipato chako: Kufanikisha hili, nunua vyakula kwa mikopo. Usiweke akiba ya chakula ndani, kila asubuhi mwambie mkeo au mumeo na watoto wako kwenda kukopa robo kilo ya sukari/unga kibandani. Kuwa na wapenzi wa kutosha wanaodai matumizi kila sekunde na simu mpya kila mwezi. Kopa kutoka kwa marafiki zako na mwajiri fedha nyingi kadri inavyowezekana na wala usijali utazilipaje.
9. Nunua gari kuukuu kama shangingi linalokupa heshima mtaani lakini linalotumia mafuta yanayogharimu mara tatu ya pato lako kwa mwezi: Gari hili litakuhakikishia kuwa na madeni ya kutosha kwa mwaka kwani utaweza kwenda gereji na kituo cha kujazia mafuta mara nyingi kuliko inavyohitajika. Hapa hutapata muda wa kuweka akiba ndogo za kipuuzi na hatimaye kupata mtaji.
10. Wape watoto wako kila wanachotaka kwani wewe ni mzazi unayewapenda mno wanao: Hawapaswi kupata shida yoyote. Kwa njia hii utafanikiwa watoto wako kukua wakiwa wazembe, na hivyo nao watarithi umasikini wako wasiweze kukusaidia katika miaka ya uzee wako.
Sitanii, enzi za Ujamaa zimepita, sasa tunatekeleza Kujitegemea (Ubepari) ikiwa utatekeleza vyema hizo amri 10 za jinsi ya kuwa masikini utakuwa na uhakika wa familia yako kuwa masikini milele. Ukiamua kutekeleza kinyume cha amri hizi, utakuwa na uhaka wa kutajirika ndani ya mwaka mmoja. Tafakari, chukua hatua.