MOSCOW, URUSI
Michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kufanyika nchini Urusi kuanzia Juni hadi Julai
mwaka huu, ni tofauti na michuano mingine ya miaka iliyopita kwa sababu ya sheria za nchi hii
ambazo ni tofauti na nyingine.
Kanuni na sheria za nchi hii zina utofauti mkubwa ambao umesababisha mabadiliko kadhaa
katika masuala ya usafirishaji na usalama; ikiwa ni miongoni mwa mabadiliko katika michuano
hiyo. Tiketi pekee haiwezi kukupa fursa ya kuingia uwanjani.
Mojawapo ya vitu unavyotakiwa kuwa navyo tofauti na tiketi ni kitu kinachoitwa FAN ID –
Kitambulisho cha shabiki. Hii ni mojawapo ya masharti yaliyowekwa na mamlaka husika nchini
humo, lengo likiwa ni kuimarisha masuala ya usalama.
FAN ID ni kitu gani?
Hiki ni kitambulisho au nyaraka ambayo ni lazima uwe nayo ili kuweza kupata fursa ya
kuhudhuria mechi za Kombe la Dunia. Ili kuipata unahitaji kununua tiketi, baada ya hapo
unaingia kwenye mtandao wa FIFA (www.fifa.com/tickets) na kujaza fomu maalum ambayo
itakuwezesha kupata kitambulisho hicho maalum kwa ajili ya Kombe la Dunia (World Cup)
2018.
FAN ID ni muhimu na lazima kwa kila shabiki, wageni na raia wa Urusi kuwa nayo ili kuweza
kuingia viwanjani, hali ambayo imelalamikiwa na wengi kuwa inaweza kusababisha usumbufu
kwa wageni wanaoingia nchini humo.
Faida za FAN ID
Kwa kawaida, upatikanaji wa viza ya kuingia nchini Urusi ni mgumu sana kutokana na sheria za
nchi hiyo hasa katika masuala ya usalama, na ili kuondoa kasumba hii wakatengeneza mfumo
maalum ambao utaondoa bughudha kwa wageni zaidi ya millioni na nusu ambao
wanategemewa kusafiri kwenda Urusi wakati wa Kombe la Dunia.
Unapokuwa na FAN ID pekee utaweza kuingia katika mipaka ya nchi ya Urusi bila kuhangaika
kupata viza, hii ni moja ya faida kubwa za kitambulisho hiki, hivyo unahitaji pasi ya kusafiria,
tiketi yako na FAN ID ambayo mamlaka za Urusi wanazitumia kama kadi ya kutambua wageni.
Usafiri wa ndani bure
Unapokuwa na kadi ya shabiki itakuwezesha kupata fursa ya kutumia mabasi na treni maalum
kwa ajili ya World Cup bila malipo yoyote. Kadi hii pia itatosha kukupa fursa ya kutumia usafiri
huo bure.
Unachohitaji kufanya ili kupata fursa hii kujisajili kupitia mtandao wa tickets.transport2018.com.
Humu utahitajika kujaza fomu ambayo itahitaji kujua mji unaotaka kwenda, kuangalia mechi
gani, siku na muda, hivyo watahitaji uweke taarifa za tiketi za mchezo husika unaotaka kwenda
kuangalia.
Mhusika bila kuwa na FAN ID na tiketi inayoonesha unataka kwenda kuangalia mchezo gani,
utakosa nafasi ya kutumia treni maalum kwa ajili ya mashabiki. Usajili wa usafiri wa bure inabidi
uufanye ndani ya saa 24 kabla ya muda wa safari yako.
Urusi imeandaa treni maalum 500 zitakazokuwa zinasafirisha mashabiki katika miji 11 ambayo

itatumika kwa ajili ya mechi za Kombe la Dunia 2018.