Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kwanza akiwa Rais kwenye Jimbo la Iowa, nchini Marekani.Nimeiandika hii, si kwa jambo jingine, bali kutokana na umuhimu wa ziara hii. Najua Rais amepata kufanya ziara kadhaa nchini Marekani, ila hii ya Iowa nitaeleza kwa nini naipa msisitizo.

Sitanii, safari katika Jiji la Iowa, nasema Rais Samia amefanya ziara sahihi. Tanzania uchumi wetu umefungamanishwa na kilimo. Rais Samia amekwenda Iowa kushiriki Mjadala wa Norman E. Borlaug.

Mjadala huu unaojulikana kama ‘Mazungumzo ya Borlaug’ ulikuwa mkutano wa siku tatu, ukiwa umekusanya viongozi wa dunia na wataalamu katika maendeleo, kilimo, sera za kiuchumi, usimamizi wa rasilimali na lishe – wote wakiongozwa na urithi wa kihistoria wa Norman Borlaug na mafanikio ya washindi wa Tuzo ya Chakula Duniani katika kupambana na njaa ulimwenguni.

Washiriki wamejadili masuala na mienendo inayozingatiwa katika chakula na kilimo, yakiwamo mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa maji na rasilimali za asili; biashara, upatikanaji wa masoko na maendeleo ya vijijini; teknolojia na miundombinu; nafasi ya jinsia katika elimu na uongozi; kukuza afya ya binadamu na wanyama; pamoja na mada nyingine muhimu.

Mazungumzo ya Borlaug yanakamilishwa na matukio ya kando, muhtasari na semina zinazoandaliwa na NGOs, biashara za kilimo, vikundi vya utetezi, wadau wa umma na taasisi nyingine.

Kwa wiki nzima macho ya dunia kwa wafuatiliaji makini wa mwenendo wa uchumi na hali ya chakula duniani, macho yalikuwa jijini Iowa, Marekani. Mkutano huu ulikuwa na washiriki na wageni 1,200 kutoka nchi zaidi ya 65 – wakiwamo wataalamu na wabunifu katika jitihada za kimataifa za kukomesha njaa katika jamii ulimwenguni kote.

Sitanii, nimemsikiliza Rais Samia akichangia katika mjadala huu. Ameeleza Tanzania ardhi ilivyo na rutuba ya kutosha na jinsi nchi yetu ilivyojaliwa maji na ardhi nzuri ya kilimo. Amelinganisha nguvu ya kilimo ya lowa na nafasi iliyonayo Tanzania ya kuwalisha majirani zetu. Tanzania kwa sasa inajitosheleza kwa chakula.

“Kuwapo kwetu hapa [kwenye mkutano huu] lengo lake ni kuhamasisha nchi kuwa na utoshelevu wa chakula katika nchi zao, na baadaye kuchangia kuwa na usalama wa chakula ndani ya dunia hii.

“Kwa hiyo sisi Tanzania tumealikwa, na kutokana na yanayotokea nyumbani katika sekta ya kilimo, tumealikwa kuzungumza. Kuzungumza, ulimwengu utujue, wajue tunachokifaya na wajue tunawakaribisha vipi.

“Kama mnavyojua kwamba dunia ya leo hakuna kitakachofanyika kikatimia bila kushirikisha sekta binafasi. Kwa hiyo uwepo wetu hapa, ni kukutana na mashirika mbalimbali. Mashirika yenye teknolojia, mashirika yanayozalisha zana za kilimo, mashirika yanayofanya research, mashirika yanayonunua, lakini mashirika yanayohamasisha uzalishaji.

“Na unapoeleza kinachotokea nyumbani, tulivyofanikiwa, nini changamoto zenu, ni mashirika haya, mnakuwa na mikutano ya pembeni na unaweza ukavuna mashirika ambayo yanatamani kuja nyumbani, na kuwekeza katika maeneo kadhaa. Hiyo ndiyo kwa nini tuko hapa,” amesema Rais Samia.

Kuhusu Kilimo Biashara, amesema: “Ni lengo zuri ambalo tumejiwekea Tanzania, na tumejiwekea Kilimo Biashara kama lengo kwa sababu kama ukiangalia Tanzania tuna ardhi kubwa ambayo haijatumika kikamilifu kwenye uzalishaji wa mazao, haijatumika kitaalamu sana katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

“Lakini sasa Tanzania tumejaliwa maji, katika maziwa na maeneo mengine, ambayo pia, hatujayakusanya tukayatumia vizuri kwenye kilimo. Kwa muda mrefu kwa sababu ya maumbile tuliyojaliwa na Mungu, maeneo mengi ya Tanzania yanapata mvua kwa wakati, ukiacha mabadiliko ya tabianchi, ambayo yameleta changamoto, wakati mwingine misimu haitabiriki.

“Lakini kwa kiasi kikubwa, maeneo mengi ya Tanzania yanazalisha kwa kutegemea mvua, lakini na kwa kutegemea uzuri wa udongo wake. Dodoma kwa mfano, Dodoma hawajaanza kutumia mbolea… kama wameanza kutumia mbolea ni miaka ya hivi karibuni, labda miaka miwili, mitatu, lakini kwa muda mrefu Dodoma haitumii mbolea.

“Kwa hiyo kuna maeneo mengi ambayo walikuwa wanalima, hawatumii mbolea. Kwa maana hiyo, tulikuwa tunalima kilimo tulichokizoea. Hatukuwa tunalima Kilimo Biashara. Lakini changamoto iliyojitokeza duniani, changamoto ya chakula, kutokuwa na usalama wa chakula, imetufanya sasa Tanzania tuamke.

“Kwamba sisi tumejaliwa vya kutosha, na tunaweza kuzalisha vya kutosha, tukala wenyewe na tukawalisha majirani zetu au pengine tukalisha Afrika. Kwa hiyo sasa hii imetuamsha,” amesema Rais Samia.

Sitanii, mwaka jana nimepata fursa ya kutembelea Jimbo la Iowa, nchini Marekani. Nilijifunza mengi. Niliandika makala nikimtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, afanye ziara katika jimbo hili. Nafurahi nimemwona kwenye msafara.

Yapo niliyojifunza Iowa, ninayoamini yanaweza kutufaidisha tukiwaiga. Sekta ya kilimo ya Iowa inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa jimbo hilo, ikichangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa (GDP) la jimbo hilo na kutoa ajira kwa wakazi wengi wa Iowa. Idadi ya watu wa Iowa inakisiwa kuwa milioni 3.21 kwa mwaka 2024.

Kutokana na kilimo, Jimbo la Iowa mwaka 2022 lilipata takriban dola bilioni 46.6 (Sh trilioni 125.8) kutokana na mapato ya mauzo ya bidhaa za kilimo. Kiasi hiki ni asilimia 12.6 ya jumla ya Pato la Taifa la jimbo mwaka 2022.


Kilimo na viwanda vinavyohusiana na kilimo vinatoa zaidi ya ajira 385,000 huko Iowa, ambayo ni takriban mtu mmoja kati ya kila watano. Sisi hapa kwetu serikali yote imeajiri watu 515,000 ikilinganishwa na wenzetu ambao sekta ya kilimo imeajiri idadi hiyo.

Sitanii, zaidi ya asilimia 96 ya mashamba huko Iowa yanamilikiwa na kuendeshwa na familia. Hii inawahakikishia kipato cha uhakika. Sekta ya ufugaji kwa upande wake inachangia dola bilioni 20.4 (Sh trilioni 55) katika thamani ya ziada kwa jimbo hilo, ikiwa na karibu ajira 170,000. Kilimo na ufugaji vinaajiri zaidi ya wafanyakazi wa serikali yetu yote.

Mahindi, mifugo ya nyama na soya ndizo bidhaa zinazozalishwa kwa wingi na kuwa na thamani ya juu zaidi huko Iowa. Kilimo kimeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha huko Iowa.

Uzalishaji wa kilimo huko Iowa ulipiga hatua kubwa katika karne ya 20, kwa kuanzisha mitambo na kupanda aina za mazao ya mseto, pamoja na matumizi ya mbolea za kemikali na viuatilifu.

Mafanikio katika uzalishaji wa kilimo yalisababisha bei za bidhaa kuwa chini, hivyo mashamba kuwa machache, lakini makubwa zaidi. Ingawa mashamba bado yalikuwa sehemu kubwa ya ardhi ya Iowa mwanzoni mwa karne ya 21, chini ya moja ya kumi ya nguvu kazi ya Iowa ilikuwa inahusika moja kwa moja katika uzalishaji wa kilimo.

Uzalishaji wa zabibu pia unaongezeka kwa umuhimu katika jimbo hilo, ambalo lina mashamba ya mizabibu mengi ya kibiashara. Sehemu kubwa ya uzalishaji wa kilimo wa Iowa inauzwa nje ya nchi, hasa Canada, Mexico na Japan.

Zaidi ya hayo, asilimia kubwa ya mauzo hayo ya nje husafirishwa kwa reli na malori hadi Mto Mississippi, ambako huhamishiwa kwenye mabehewa ya majini kwa ajili ya kusafirishwa hadi Ghuba ya Mexico na kisha nje ya nchi.


Uvunaji miti ni mdogo na hupatikana hasa katika maeneo yenye milima zaidi ya jimbo, hasa katika milima ya Loess upande wa Magharibi na eneo la Driftless Kaskazini – Mashariki.

Kwa vyovyote iwavyo, Tanzania inayo mengi ya kujifunza kutoka Iowa, hasa kilimo cha mahindi ambacho kwa kutumia teknolojia na mbolea wanazalisha kwa wingi kutoka kwenye ekari moja na viwanda.

Sitanii, kwa kuwa wiki iliyopita ilikuwa na matukio mengi, sitatenda haki nikihitimisha makala hii bila kuyagusia japo kwa uchache. Hili la ziara ya Rais Iowa, limeungana na uamuzi thabiti wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuutangazia umma kuwa kodi zitakusanywa kistaarabu.

Sitanii, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, amewatangazia wawekezaji kuwa TRA haitafunga akaunti ya mfanyabiashara, bali yatafanyika mazungumzo ya kina. Mtazamo huu ni muhimu. Nampongeza Mwenda, japo hii haimaanishi kuwa wafanyabiashara sasa watatumia uchochoro huu kuacha kulipa kodi.

Suala jingine, ni mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenye vyama vya upinzani, wameshiriki mchakato ulioanzisha mwendo wa kuelekea Novemba 27, 2024 tutakapofaya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Sijasikia kelele kama za mwaka 2019. Naamini mwaka huu uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki.


Kama hiyo haitoshi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, ameeleza ufanisi uliopatikana katika miezi mitatu ya mwanzo ya Kampuni ya DP World inayoendesha kitengo cha makasha pale bandarini.

Sitanii, nilikuwa wa kwanza kuandika makala juu ya umuhimu wa DP World nilipopata safari ya kwenda Dubai na niliporejea nikaeleza umuhimu wa kuwa na wawekezaji kama hawa. Makala ile kwa muda iligeuka mateso kwangu. Nilitukanwa kila kona na wanaharakati hata watu niliowaheshimu. Kwa kupotosha wakasema bandari inauzwa.

Sitarejea mafanikio yote 10 iliyopata DP World, ila angalau basi niseme nimeguswa na tangazo la Prof. Kitila kuwa kwa mwezi sasa TRA inakusanya Sh trilioni 1 kutoka Bandari, kutokana na DP World kuboresha huduma. Hii ina maana kwa mwaka Bandari pekee inakwenda kuiingizia TRA Sh trilioni 12 na zaidi.

Hapo wamefanya uwekezaji kwa asilimia 30 tu kulingana na muda, itakuwaje ikifika asilimia 100? Kwa kweli katika hili la DP World, naomba Watanzania tujifunze jambo. Moja, tuepuke kumwagia wenzetu matusi linapotokea jambo, lakini pia, tujipe muda wa kufanya utafiti kabla hatujatoa maoni ya kitaalamu. Haya basi, DP World inafanikiwa, wako wapi manabii wa uongo waliosema haifai?

Sitanii, suala jingine, gazeti letu wiki iliyopita limechapisha habari ya TANROADS kuwa hoi kifedha. Mrejesho nilioupata kutoka kwa makandarasi sina sababu ya kuongeza neno. Itoshe tu kusema serikali iangalie kila namna makandarasi wanaouziwa nyumba na kufilisiwa walipwe japo kidogo.

Nafahamu El Nino, Kimbunga Hidaya, riba za mikopo ya nje zimepanda kwa wastani wa asilimia 30 hadi 40 kutokana na dola kucheza. Miradi mikubwa kama reli ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere yanaendelea kujengwa na mishahara ya watumishi wa umma inalipwa, ila hata makandarasi mjue wana familia. Walipwe japo kidogo hata kama kwa kusema haya, tunaambiwa tunatumika! Mungu ibariki Tanzania.

0784404827