Na Anthony Mayunga, JamhuriMedia, Mara
Baadhi ya wanawake na watoto wanaojihusisha na uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia zebaki hapa nchini ni waathirika wakubwa wa kemikali hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zebaki inapoingia mwilini inaharibu mfumo wa neva, moyo na kusababisha matatizo ya uzazi. Pia huharibu viungo vya ndani, huku wajawazito wakiwa na kiwango kikubwa cha kemikali hizo mwilini huwa na hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo ya akili.

Si hivyo tu, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha takriban asilimia 60 ya wanawake walioko katika maeneo ya uchimbaji wa dhahabu wana kiwango kikubwa cha zebaki mwilini na kitendo hicho kinatishia afya zao na maendeleo ya watoto.
Pia Sera ya Taifa ya Madini ya mwaka 2009 inasema matumizi ya zebaki katika uchimbaji madini yanatakiwa kukabiliana na viwango vya kimataifa katika utunzaji wa mazingira na afya ya watu, huku ikihimiza matumizi ya teknolojia mbadala ili wachimbaji waachane nayo.
Msimamizi wa Mradi wa Kudhibiti Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo, Dk. Befrina Igulu, amesema kutokana na serikali kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo, idadi ya wanawake imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika uchimbaji mdogo wa madini.

Huku karibu asilimia 20 hadi 30 ya watu milioni 7.2 wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani katika uchimbaji wa dhahabu ni wanawake.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu inakua kwa kasi na
kutoa ajira za moja kwa moja kwa takriban watu milioni 1.5 na ajira zisizo za moja kwa moja kwa watu milioni 7.
“Serikali kupitia NEMC imeanzisha mradi unaolenga kupunguza au ikiwezekana kuondosha kabisa matumizi ya zebaki kwenye uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu hapa nchini,” amesema Dk. Igulu.
Pia amesema wanawake wanaojihusisha na uchimbaji wa dhahabu wako katika umri mdogo wa kuzaa, matumizi ya njia zisizo salama katika uchenjuaji kama vile uchomaji holela wa zebaki unaohatarisha afya za akina mama, watoto na uchafuzi wa mazingira.

Kupitia mradi wa Kudhibiti Athari za Kiafya na Uchafuzi wa Mazingira (EHPMP), amesema wanaendelea kutoa mafunzo ya njia bora za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kwa njia mbadala.
Kutokana na tathmini zilizofanywa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeonyesha hali ilivyo kwa sasa wachimbaji wadogo wa dhahabu hutumia kiasi cha tani 13.2 hadi 24.4 ya zebaki kwa mwaka.
Hata hivyo, amesema matumizi yasiyo salama ya zebaki katika kuchenjua dhahabu husababisha athari kwa afya ya binadamu na mazingira, hasa katika mikoa 14 Tanzania Bara ikiwamo Geita, Mwanza, Mara, Morogoro, Singida, Mbeya, Shinyanga na Katavi.
Ameitaja changamoto kubwa kuwa ni uelewa mdogo kwa wanawake wa umri mdogo wa kubeba mimba kuhusu madhara ya zebaki kiafya na katika mfumo wa uzazi.

“Kwa watoto yanapotokea madhara katika umri mdogo husababisha uelewa hafifu, kinga dhaifu na kuhatarisha ustawi wa jamii nzima. Kwa akina mama pia husababisha kinga ya mwili kushuka kwa kiwango kikubwa na kuathiri mifumo ya neva na fahamu, uwezo wa mama kubeba mimba hupungua na kuwa na changamoto za mimba kutoka mara kwa mara,” amesema.
Ameyataja baadhi ya matatizo mengine ni watoto kuzaliwa mapema, kuzaa watoto wenye uzito mdogo, mabadiliko ya mhemko, ugumu wa kutembea na kushika mimba.
Kupitia Mkataba wa Minamata uliosainiwa Agosti 31, 2019 na nchi 113, kunatakiwa kuandaliwa mikakati ya afya inayolenga kupunguza athari za zebaki kwa wachimbaji.
“Mbali na utoaji elimu kwa wachimbaji na wadau wengine, mikakati inafanywa ya kutambulisha matumizi ya teknolojia zisizotumia zebaki katika kuchenjua dhahabu na mafunzo ya matumizi sahihi ya vifaa kinga na matumizi salama ya zebaki wakati wa kuchenjua dhahabu kwa wanawake,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA), Salma Ernest, amesema athari kwa makundi hayo kiafya ni kubwa na chanzo ni umaskini.
“Athari kwa kundi hili ni kubwa licha ya juhudi kubwa za serikali kupitia NEMC kutoa elimu, wapo wanaochimba lakini wengi wanapewa kazi ya kuchenjua kwa kutumia zebaki, baadhi utawakuta ni wajawazito na walio na watoto migongoni, wote wanaathirika kwa pamoja,” amesema.
Ameiomba serikali itambulishe njia mbadala itakayowanusuru wachimbaji wadogo, hasa wanawake wasipate madhara hayo.
“Mkataba wa Minamata unaelekeza kuanzishwa kwa njia mbadala lakini tunaomba iwe na vigezo na gharama nafuu wanayoimudu na uzalishaji wake uwe mzuri,” amesema.
Amekiri kupitia elimu kuna mabadiliko kwa baadhi ya wachimbaji, hasa wanawake, kwa kuwa wameanza kutumia vifaa na wengine wanawaweka watoto mbali, kwa sababu wanapochoma mvuke husababisha athari kiafya.
“Tunaomba Wizara ya Madini iendelee kujenga vituo vya mfano ambavyo vitawasaidia wachimbaji kuvitumia na kuepuka madhara kiafya,” amesema.
Septemba 10, 2019 Bunge la Tanzania liliridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki (Minamata Convention on Mercury) kwa kuwa takriban asilimia 25 hadi 30 ya wachimbaji wadogo wanaathiriwa na kemikali hiyo.
Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kulinda afya za binadamu na mazingira dhidi ya athari ya uchafuzi wa mazingira dhidi ya kemikali hiyo.

Pia usimamizi wake utahusisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali Viwandani na Majumbani ya Mwaka 2003, Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003 na Sheria ya Chakula na Dawa ya Mwaka 2003.
Tafiti zinaonyesha zebaki hudumu katika mazingira kwa kati ya miaka miwili au mitatu na inasafiri masafa marefu kwa njia ya hewa, maji, mito, maziwa, bahari na udongo kwa umbali wa kilomita 1,000 kutoka katika chanzo chake na huathiri binadamu, viumbe wengine na mazingira kwa ujumla.
