Mwenyekiti wa Taifa wa UDP, John Cheyo maarufu kama ‘Bwana Mapesa’, amesema suala la mwafaka wa urais Zanzibar ni gumu na halihitaji kuamuliwa kirahisi rahisi bila kutafakari.
Badala yake Cheyo amesema kuna haja kwa viongozi kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili wapate jawabu la jambo hilo ili liweze kumalizika salama.
“Suala la Zanzibar ni gumu na tusilichukulie kirahisi, kama kuna jambo gumu, basi usilifanye rahisi kwa kusema maneno mengi.
“Nasema ni gumu kwa sababu tangu awali matatizo tuliyokuwa nayo katika uchaguzi wa kuanzia mwaka 1995, 2000 ni tofauti, tulimaliza akapatikana Rais lakini bado watu walisema hawakushinda, hiyo ni kawaida.
“Lakini zamu hii hatukumaliza uchaguzi Zanzibar kwa hiyo matokeo hayakuwapo na Dk. Francis (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) hapa, amelisema hilo kwamba tumetunga Katiba ambayo haiko vizuri, yaani hata kama kuna kitu… kuna mvuke lazima kuwe na kitu kidogo cha kutokea,” amesema Cheyo wakati akizungumza Dar es Salaam katika kipindi cha Je, Tutafika? kinachorushwa hewani na kituo kimoja cha televisheni.
Ameongeza kwamba Watanzania wamefunga kabisa kwamba linalotamkwa na tume ndilo hilo iwe wanalipenda ama la “kwa sababu hakuna taasisi nyingine inayoweza kuiambia tume kwamba mlichosema si sahihi, hilo ndilo tatizo kubwa tulilonalo.
“Kwa hiyo, njia iko wapi mimi nasema njia iko kwenye meza. Hata kama ni siku ngapi wazungumze tu mpaka jawabu lipatikane,” amesema Cheyo na kuongeza:
“Na mimi na Francis hapa hebu tujishauri na mheshimiwa Rais ajue anachofanya tusitoe jibu la haraka haraka. Na hawa wanaotusaidia, wafadhili wetu na wenyewe wasitusukume tukatoa majibu ya haraka haraka.
“Tunawasihi sana watu wa Zanzibar kwamba pamoja na yote haya wamekaa kimya wametulia wanasubiri kinachotokea kwa viongozi wao, kwa hiyo tegemeo letu ni viongozi wetu wakae vizuri kwenye meza wapate jawabu la jambo hili ili tuweze kufika salama,” amesema.
Kwa mujibu wa Cheyo, Zanzibar kuwa tulivu ndiyo utulivu wa Muungano na ndiyo utulivu wa nchi nzima, hivyo anawatakia kila la heri Watanzania na anamwombea Rais Magufuli na kumtakia kila la heri katika kulitatua hilo.
“Namtakia kila la heri Rais Magufuli lakini ana kiporo kigumu na lazima kipate njia ngumu ya kuweza kutatua njia hii lakini naamini meza ndiyo pale kila kitu kitatokea na si vingine.
“Na hapa napenda kutoa rai kwa rafiki zangu wa upinzani tuweke Tanzania mbele siyo kila kitu kifanyike kama njia ya kupata mwafaka kisiasa,” amesema Cheyo.
Kwa mujibu wa Cheyo, yeye ni muumini wa siasa za ushindani kwani UDP iliingia kwenye uchaguzi wa ushindani mwaka 1994 “na niwaambie Watanzania wasisikilize kwamba tangu Uhuru hakuna kilichofanyika.”
Ameshauri pia Rais Dk. John Magufuli kuiwezesha nchi itafute njia mbadala za kutafuta pesa za maendeleo badala ya kutegemea misaada kutoka nje.
Akizungumzia kuhusu siasa za ushindani, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Biashara, Dk. Francis Michael, amesema Watanzania tumeanza kukomaa kisiasa; mfano uchaguzi umefanyika na umekwisha salama na tumempata Rais mpya kinyume na matarajio ya nchi nyingi za nje.
“Kwa sababu matarajio ya nchi nyingi za nje kwa sababu kimtazamo kwamba tufike mahali tuone lile ambalo si la kawaida linatokea katika Taifa la Tanzania lakini halikutokea kwa sababu ya ukomavu wa kisiasa ambao Watanzania wanalo.
“Kasoro ya baadhi ya sehemu chache ambazo vitu hivi haviwezi kukosekana, mfano bungeni tuliona kilichofanyika ambacho hakikuwa kizuri kimekwenda nje ya kanuni, mfano viongozi wanaingia bungeni huku wengine wakizomea si kitu kizuri ingawa nilisema kuna haki demokrasia ya kila mtu mwingine kutoa au kuweka mawazo yake.
“Lakini pia hii haki ya kidemokrasia ya haki za binadamu inasema usije ukaifanya haki yako ikapitiliza ikachafua haki ya mwingine,” amesema Dk. Michael.
Pamoja na mambo mengine ameshauri Rais Magufuli kuangalia namna ya kubadili sheria za uwekezaji kwa sababu kuna wawekezaji wanaokuja kuwekeza pasipo kuwa na nia nzuri, mfano huko nyuma tuliona kuna watu wanawekeza kwenye mashirika hewa na kadhalika.
Pamoja na mambo mengine, anasema anakumbuka enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ilikuwa tofauti na sasa ambapo watu wengi wamekuwa wakikimbilia huko kwa kutaka kutawala.
“Kuna kipindi nilikuwa naongea na waziri mmoja wa Serikali ya Awamu ya Kwanza hivi sasa ni mzee, siku ukiambiwa uende Ikulu hulali unawaza, lakini leo hii Ikulu pamekuwa sehemu ya kukimbiliwa,”amesema mhadhiri huyo.
“Wawekezaji wa nje siyo wabaya lakini tujiulize hizo sheria tulizoziandaa zikoje? Siyo tunaona tu kwamba watu wa nje wanatunyonya, ndiyo maana nasema sheria zetu mbalimbali zirekebishwe,” amesema.