Miongoni mwa habari zilizochapishwa kwenye gazeti hili zinazungumzia Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika habari hiyo, Maalim Seif ametajwa sehemu mbili. Kwanza ni namna ambavyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kinavyohaha kuweka mambo sawa ili aridhie uchaguzi mkuu urudiwe tena Januari, mwakani.
Hatua hiyo inatokana na uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu kukumbwa na dosari ambazo zilimsukuma Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kufuta matokeo yote kama alivyodai.
CUF imeishauri ZEC kutengua uamuzi wa mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, kwa vile hana mamlaka ya kikatiba na sheria ya uchaguzi kuweza kufuta uchaguzi huo.
Pili, Seif ametajwa kwa namna anavyojipambanua kuwa ni mshindi na anasubiri kuitwa na kutangazwa na ZEC.
Seif ambaye juzi alizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu ngazi za Wilaya na Majimbo katika ukumbi wa Majid, Kiembesamaki Zanzibar kabla ya kuzungumza na JAMHURI, anasema: “Leo nilikuwa nazungumza na wajumbe wa CUF, nimewaambia kabisa kwamba hawana sababu ya kukimbia.”
Badala yake, kiongozi huyo wa muda mrefu CUF, anawataka wafuasi na wapenzi wa chama hicho kutembea kifua mbele kutokana na ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.
Anasisitiza hakuna sababu za kurejewa kwa uchaguzi huo kwa sababu ulifanyika kwa amani na hakukuwa na dosari ya kuusitisha kwani washindi wa uwakilishi na udiwani walikwisha kutangazwa.
Katika hali ya kawaida tu, sisi wa JAMHURI hatuwezi kuacha kuizungumzia Zanzibar. Hii ni kwa sababu ni sehemu ya muungano inayotambuliwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya kwanza (1) na ya pili (2).
Wakati nchi yetu ikiwa kama darasa kwa nchi nyingine hasa za Kiafrika zinazoshindwa kuachiana madaraka, leo hatuwezi kuacha kuizungumzia Zanzibar ambako kumeibuka mzozo wa kimamlaka ambapo sasa pande mbili za siasa zinavutana. Kwetu sisi wote ni washindi kwa sababu ni Wazanzibar kadhalika ni Watanzania.
Tunachokiona sisi ni kwamba Rais mpya wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli atakuwa na kibarua kigumu kuanza kutekeleza ahadi zake kama itatokea Zanzibar kutoelewana.
Wito wetu sisi ni kwamba Wanzibar waketi chini, wafuate taratibu za kumaliza mzozo wao ili kumpa nafasi au nafasi viongozi wapya ambao wengi wameingia kwenye vyombo vya uamuzi kama watu wapya.
Ama kwa hakika, leo hii Dk. Magufuli akienda Zanzibar kutafuta mwafaka kwa mambo wanayoweza kuyaweka sawa atakuwa ameacha kuanza kutimiza ndoto mpya za Watanzania ambao kwa sehemu kubwa wanahubiri mabadiliko.
Mabadiliko ya kuwaletea maisha nafuu Watanzania, katu hayawezi kwenda sambamba na kuanza kutatua migogoro ambayo usuluhishi wake uko kwenye sanduku la kura kuamua kiongozi wa nchi.