Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb.) ameiagiza Bodi ya Stakabadhi za Ghala kuhakikisha zao la Mwani, linakuwa zao la kwanza kuingizwa kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika Mkoa wa Tanga likifuatiwa na Katani, Korosho kilimo cha mbogambaoga na matunda .
Vilevile amewashauri Vongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Madiwani na Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Vyama vya Ushirika kutoa elimu na kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mfumo huo wenye manufaa makubwa kwa Wakulina na Taifa kwa ujumla.

Aidha, ametoa rai kwa Taasisi za umma na binafsi kuchangamkia fursa kwa kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa maghala, usafirishaji wa mazao, na uongezaji thamani kwa bidhaa zinazohifadhiwa na kuuzwa kupitia Mfumo huo ili kuhakikisha miundombinu ya hifadhi ya mazao inapatikana mara mfumo huo utakapoanza kutekelezwa rasmi.
Waziri Jafo ameyasema hayo Aprili 11, 2025 wakati akiongoza Kikao cha wadau wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Kidigitali kilichofanyika mkoani Tanga kikilenga kujadili namna bora ya kutumia Mfumo huo katika kunufaisha wazalishaji wa bidhaa hususan za kilimo kwa kuwapatia bei shindani iliyopo sokoni.

Vilevile Wadau hao walipata fursa ya kutoa changamoto zao, maoni na mapendekezo yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa mfumo huo ambao umekuwa mkombozi kwa wakulima
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amebainisha kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utawasaidia wakulima kupata thamani halisi ya mazao yao, kuongeza tija, kipato huku ukileta mageuzi katika sekta ya kilimo na biashara kwa mkoa wake huku akiahidi kuchagua mazao kumi yatakayochukuliwa katika mfumo huo.





