Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ZFDA umekabidhiwa rasmi Cheti cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015.
Cheti hicho cha ubora ni kielelezo cha taasisi ya ZFDA juu ya kusimamia misingi imara ya kuhakiki ubora wa huduma katika kiwango cha kimataifa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Cheti hicho Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa vitendo wa azma ya serikali inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya hususan upatikanaji chakula, dawa na Vifaa tiba.
Amesema kunahitajika ubunifu na jitihada za makusudi za kila mfanyakazi wa ZFDA kuhakikisha Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba ni bora na salama kwa afya za wananchi.Amefahamisha kuwa mafanikio hayo yaliyopatikana yawe chachu ya kuongeza ufanisi kiutendaji ili kufikia dira iliyowekwa.
“Mkifikia dira dira hiyo itakuwa mmetekeleza kikamilifu jukumu mllopewa na Serikali la kulinda afya ya jamii.Serikali inaaamini mnao uwezo wa kuwa taasisi bora ya udhibiti Afrika na Duniani kwani hakuna kizuizi cha kufikia dira hiyo” Alisema Waziri Kombo.Aliitaka menejimenti ya ZFDA kuimarisha udhibiti wa uingizaji wa Chakula, Dawa na Vipodozi nchini kiholela ili kulinda afya za Wazanzibari.
“Ndugu wafanyakazi mna jukumu kubwa sana kwa Wananchi wetu na mbele ya Mungu maana mtakaporuhusu uingizwaji wa bidhaa duni zenye madhara mtahatarisha afya za Wananchi na kesho mbele ya haki Mungu mutaulizwa” aliwanasihi Waziri Kombo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya ACM Ltd iliyokabidhi cheti hicho Nyasha Mupukuta alisema haikuwa kazi rahisi kwa Taasisi hiyo kupatiwa Cheti hicho cha ubora.Alisema kulipita ukaguzi wa kutosha na wa muda mrefu kabla ya Cheti hicho kutolewa na hivyo kuendelea kuipongeza ZFDA kwa kazi kubwa waliyoionesha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Burhani Othman Simai wakati akielezea sababu zilizopeleka kupatiwa ZFDA kupatiwa Cheti hicho ni pamoja na kuwepo kwa sera na miongozo ya ubora, mkataba huduma kwa wateja, kanuni za maadili za wafanyakazi (code of Conduct), wafanyakazi kusaini fomu za conflict of interest or competing interest na taratibu sanifu za utendaji kazi (SOP).
Sababu nyingine ni ufanyaji wa tathmini ya mteja kuridhika huduma zinazotolewa (customer satisfication survey) na kuainisha majukumu ya kazi kwa kila mfanyakazi (Job Description).
Hafla ya kupokea cheti hicho cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 zilifanyika katika Ofisi ya ZFDA Mombasa mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na Wakurugenzi mbalimbali na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Zanzibar Andy Michel.