Na Dk. Juma Mohammed

Utafiti wa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia unaweza kuzidisha umaarufa wa Visiwa vya Zanzibar ambavyo vimetajwa na waandishi wengi wa vitabu na hata watu wengine mashuhuri waliopata kuvitembelea visiwa hivi kwa miaka mingi iliyopita.

Ugunduzi wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia unaweza kuigeuza historia nzima ya Zanzibar. Kitabu maarufu cha kale kilichoandikwa na Wilfred Schoff cha “Periplus of the Erythrean Sea” kinaitaja Miji ya Zanzibar na umaarufu wake kwa wasafiri na wafanyabiashara kwa zama hizo.

Katika kitabu  hicho, kilichoandikwa mwaka 100 A.D. (kabla ya Nabii Issa), Zanzibar imetajwa kwa jina la ‘Menouthias’ ikiwa tayari ni nchi yenye watu mchanganyiko tena walio na ustaarabu wakiwa wanavaa nguo za hariri.

Naam! Baada  ya karne nyingi kupita, Zanzibar inaweza kurejea katika zama ambapo watu wake watavaa nguo za hariri zitakazopambwa na kila aina ya mapambo.  Inaeleweka na kila mtu kwamba hadi sasa moja kati ya rasilimali yenye kuleta mapato mengi duniani ni rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Uchumi wa mafuta na gesi asilia umewakomboa wananchi wengi katika nchi zenye kuzalisha nishati hiyo. Tunaona namna watu katika mataifa yenye kuzalisha mafuta na gesi asilia walivyokuwa na jeuri ya pesa, sisemi hapa Zanzibar watu watakuwa na jeuri ya pesa la hasha.

Umuhimu wa mafuta na gesi asilia unafahamika na kila mmoja. Ninachokusudia kueleza hapa leo ni kuwa hali za maisha ya wanyonge visiwani Zanzibar itabadilika kwa haraka na kufikia katika maisha mazuri, ingawaje safari hiyo ni ndefu na yenye misukosuko njiani, lakini tutafika katika uchumi endelevu na imara.

Kwa miaka kadhaa sasa kilio cha wanasiasa na hata baadhi ya wananchi visiwani Zanzibar ni kuona suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia linaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano ili kila upande usimamie wenyewe rasilimali hiyo.

Jambo hili lilizua mjadala mrefu na hatimaye baada ya mazungumzo ya Serikali mbili katika usimamizi wa rasilmali za mafuta na gesi asilia, iliamuliwa kuwa kila upande katika Jamhuri ya Muungano upewe uwezo wa kusimamia rasilmali hizo na kuanza kwa kufutwa kwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano Sheria ya Mafuta ya mwaka 1980.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria mpya ya Mafuta ya mwaka 2015 ambayo ilijengeka katika misingi ya usimamizi wa rasilmali za mafuta na gesi asilia  kwa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha sheria yake yenyewe ambayo itasimamia shughuli kama hizo kwa Zanzibar.

 Kwa msingi huo basi ndio wiki iliyopita shughuli rasmi za utafiti wa utafutaji na uhimbaji wa mafuta na gesi asilia zilianza baada ya kampuni ya RAK Gas ya Ras Khaimah inayomilikiwa na Falme za Kiarabu (UAE) wakishirikiana na SMZ wameanza kufanya utafiti huo chini ya Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza.

Eneo ambalo litahusika na utafiti huo ni kitalu cha Pemba- Zanzibar kinajumuisha maeneo yote ya nchi kavu ya Visiwa Zanzibar vikubwa na vidogo pamoja na maeneo ya bahari iliyozunguka Visiwa hivyo.

Kiongozi wa timu ya Watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna akitoa maelezo kuhusu kazi ya utafiti huo, amesema watatumia muda wa miezi mitatu kufanya utafiti huo Unguja na Pemba.

Ni vyema ieleweke kuwa, ingawa uwekezaji katika mafuta na gesi asilia unahitaji fedha nyingi, faida ya moja kwa moja katika uwekezaji huo inapatikana kwa muda usiopunguwa miaka minane na kuendela.

Hivyo, ni vizuri wananchi wakaelewa kuwa uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi asila ni kazi inayochukua muda mrefu na inahitaji uvumilivu na ndio maana zipo kampunchache zinazowekeza katika sekta hiyo.

Uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mafuta na gesi asilia ni katika bahari, hivyo maeneo yanayotegemewa kwa upande wa Zanzibar ni  maeneo ya pwani ya Wesha katika Kijiji cha Tundaua, Mkoa Kusini Pemba na maeneo ya pwani ya Unguja.

Iwapo Zanzibar itagundulika kuwa na rasilimali ya kutosha ya mafuta, ugunduzi huo utabadili mwelekeo mzima wa kiuchumi wa Zanzibar. Kwa mujibu wa wataalamu wa fani ya mafuta, kuna kila dalili kwa eneo la Bahari ya Zanzibar na  visiwa vyake vidogo vidogo kuwa na mafuta.

Mwaka juzi nilibahatika kuhudhuria mafunzo ya menejimenti ya mafuta na gesi asilia nchini China, moja kati ya wataalamu wa fani hiyo alitueleza kwamba kwamba Zanzibar ni eneo lenye uwezekano mkubwa wa mafuta na gesi asilia ambapo Serikali imeshauriwa  kuharakisha utafutaji na uchumbaji wa  rasilimali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za kitaalam kuhusu rasilimali ya mafuta na gesi asilia ilidhihirika kuwa Zanzibar ni moja kati ya eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi asilia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Zanzibar ni katika nchi yenye akiba kubwa ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa nchi za mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki. Bila shaka kuanza kwa utafiti kumepokelewa kwa furaha na wananchi wa Zanzibar ambao walikuwa na shauku ya kuona kazi hiyo inaanza kwa haraka zaidi.

Nazipongeza Serikali zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.

Pia naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha ombi la nyongeza  kutaka kuongeza mipaka yake ya bahari. Katika Andiko hilo kwa Umoja wa Mataifa, Tanzania ilidai nyongeza ya eneo lenye ukubwa wa maili za majini 150 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari.

 Ni muhimu kutambua kuwa Tanzania Bara ina Ukanda wa Pwani wenye urefu wa kilometa 1,424 na upana wa maili za majini (nautical miles) 200.

 Eneo hilo la Bahari limegawanyika katika Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) yenye upana wa maili za majini 12 sawa na kilometa za mraba zipatazo 64,000 na eneo la Bahari Kuu (Deep Sea) lenye upana wa maili za majini 188 sawa na kilometa za mraba zipatazo 223,000.

Andiko hilo kwa mujibu wa Sheria ya kimataifa ya masuala ya bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4 ambayo inatoa ruksa kwa nchi ambayo iko kando kando ya bahari kudai nyongeza ya eneo la bahari.

Kama inavyofahamika kuwa sheria ya Kimataifa ya bahari inatoa haki kwa kila nchi kupewa maili za kwanza 12 ambazo ni exclusive kwa ajili ya usalama wake. Azimio la UN la Desemba 10 mwaka 1982 limetoa haki hiyo katika mkutano wake uliofanyika kule Montego Bay, Jamaica.