Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafungulia kesi za uhujukumu uchumi wafanyabiashara watakaobainika kwa makusudi wanaficha vyakula na bidhaa kwa lengo la kuwapandishia bei wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo, kwenye mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na wahariri na waandishi wa habari, Ikulu Zanzibar.
Amesema kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo,Serikali imejihakikishia kuwepo kwa bidhaa nyingi ikiwemo vyakula kama unga wa ngano,mafuta ya kupikia, sukari na mchele kukidhi mahitaji ya mfungo wa Ramadhani.
Dkt.Mwinyi ameeleza, Serikali haitarajii kuibuka kwa mfumuko wa bei ama bidhaa kuadimika hali itakayosababisha taharuki kwa wananchi na waumini wa dini ya Kiisaam ambao watakua wakitekeleza ibada ya Swaumu.
Rais Dkt.Mwinyi amesema kipindi kifupi kilichopita baada ya mkutano wake na wafanyabisahara mbalimbali wa vyakula kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula, ghafla vyakula vilienea nchi nzima nakuonya kwa mfanyabiasa atakayebainika anaficha vyakula kwa nia ya kujinufaisha, Serikali haitosita kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi.
“Kuhodhi vyakula ili vipande bei ni uhujumu wa uchumi, atakaeficha vyakula kutamshitaki kwa kosa la uhujumu uchumi, tumetaarifiwa, mchele upo,sukari ipo, ngano ipo na mafuta ya kupikia yapo kwa ajili ya Ramadhani, tukikubaini umehodhi kwa lengo binafsi tutakushitaki kwa kosa la uhujumu uchumi” ametahadharisha Dkt. Mwinyi.
Kuhusu mfumuko wa bei, Dkt.Mwinyi amesema sio tatizo la Serikali bali linachangiwa na sababu mbalimbali za kidunia, amesema Zanzibar inaingiza mchele kutoka Pakistani ambako kumekumbwa na mafuriko aidha, ngano kutoka Ukraine ambako nako kumbekumbwa na vita baina yao na Urusi hali iliyosababisha bei za vyakula kupanda nakuongeza kuwa kwa asilimia kubwa Zanzibar pia inategemea vyakula kutoka Tanzania Bara ambako kwa baadhi ya mikoa inayozalisha vyakula ilikumbwa na janga la ukame.
Kuhusu bandari Malindi Rais Dkt.Mwinyi, ameeleza Serikali inatambua ufinyu wa bandari hiyo unaosababishwa kuwa na gati moja hali inayosababisha usumbufu kwa kukawia kushushwa mizigo mingi kwa wakati, nakueleza mpango wa serikali kuondosha changamoto hizo kwa kukamilisha ujenzi wa bandari ya Mangapwani inatarajiwa kutoa huduma zote muhimu zikiwemo bandari za kushushia, vyakula, nafaka, mafuata na bandari nyengine lengo ni kuongeza kasi ya uendeshaji bandarini.
Aidha, Dkt.Mwinyi ameeleza Serikali imechukua jitihada za dharura kwa kuagiza mashine za kisasa zenye wepesi wa kushushia makontena, kuendelea kulitumia eneo la Bwawani kuhifadhia makontena na kutumia bandari ya Mpigaduri kushushia mizigo ili kupunguza msongamano kwa bandari ya Malindi.
Ameeleza kukamilika bandari ya Mangapwani kutatoa fursa kwa bandari ya Malindi kutumika kuwa bandari ya utalii kwa kupakia na kushushia masuala yanayohusu utalii pekee.
Kuhusu masuala ya udhalilishaji, Rais Dk. Mwinyi amevitaka vyombo vya Sheria kuangalia kesi za watoto kati ya miaka 18 na 17, alieleza kumekua na malalamiko mengi kuhusiana na kesi hizo zinazodaiwa wasichana kuwatengenezea kesi za makusudi wavulana ambao wengi sheria huwatia hatiani, kwa kesi za udhalilishaji wa kinyama kwa watu wazima wanaume kuwadhalilisha watoto wachanga wa miaka 2 hadi 5 na zaidi, Rais Dk. Mwinyi alivitaka vyombo hivyo kutofumbia macho kesi za aina hiyo wala kuzipa dhamana.
Akitoa ufafanuzi kwa watoa huduma wa kimataifa wa Uwanja wandege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, kampuni ya kimataifa ya DNATA,kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kwenye mkutano wao wa hadhara uliofanyika Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kipindi kifupi cha huduma zinazotolewa na kampuni ya DNATA.
Serikali imengiza zaidi ya bilioni nane kwa robo mwaka ya kwanza ambapo inatarajiwa kuchangia zaidi ya bilioni 32 sawa na asilimia 12 kwa mwaka ikilinganishwa na kampuni wazawa walioongoza viwanja hivyo kwa zaidi ya miaka 25 ambao walikusanya milioni mbili tu,sawa na asilimia 5 kwa mwaka.
“Serikali ya Awamu ya Nane, imewapa kazi kampuni ya DNATA kuendesha Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Terminal 3, hoja ya ACT kwanini imepewa DNATA badala ya kampuni wazawa haina mantiki, kampuni za ndani zilitoa huduma kwa zaidi ya miaka 25 na Serikali ilikuwa haipati kitu hata mishahara ya wafanyakazi Serikali ilitoa hazina, Serikali ilipata hasara tupu” alifafanua Dk. Mwinyi.
Amesema kwa kipindi chote hicho hata mapato ya maegesho ya ndege ilichukua kampuni binafsi za ndani na hali ya uwanja wandege haikua kama sasa ilivyo ambapo Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ni wa kwanza kwa ubora Tanzania nzima ikilinganishwa na viwanja vya ndege vya Dar-es salam na Kilimanjaro.
Ameeleza wanachokisema ACT Wazalendo hakina uhalisia na wala hawatetei kwaajili ya maslahi mapana ya nchi wala kuitetea Serikali bali ni kupotosha umma kwa maslahi yao binafsi hata hivyo, aliwafahamisha wananchi Serikali inafanya yale ambayo nchi inataka kwa maslahi ya umma.
Kuhusu Serikali kuwaachia sekta binafsi kutoa huduma kwa wananchi, Dk.Mwinyi alieleza ni mfumo mzuri wakuendesha sekta za umma ili wananchi wanufaike na huduma za jamii, alieleza kwasasa Serikali imeanza mfumo huo kwa sekta ya Afya ambapo hospitali za serikali zitatoa huduma za vipimo na maabara kwa kusimamiwa na taasisi binafsi kisha Serikali itagharamia ili kuwaondoshea wananchi usumbufu wa kukosa huduma hizo. Aidha alieza huduma hizo zitakua endelevu kwa tasisi nyengine za umma zinazotoa huduma za kijamii.
Katika hatua nyengine Rais Dk.Mwinyi amevipongeza vyama vya siasa kwa kuanza mikutano ya adhara pia alivitaka vyama hiyo kuhubiri amani yanchi badala ya kupotosha umma kwa mambo wanayofanyiwa na serikali yao na kuongeza kwamba hachukii kukosolewa, lakini watu wakosee kwa kutengeneza sio kuupotosha umma.
Amesema demokrasia sio kuchochea,kueneza chuki kwa watu na kueleza masuala ya uvunjivu wa amani bali inataka kushirikiana, kueleza mambo yenye kutengeneza kwa mustakbali wa taifa na sio kupotosha umma.
Amewatanabahisha wanasiasa wanaotumia majukwaa ya siasa kuwaaminisha umma masuala yasiyo na uhakika na kuwashauri kufanya uchunguzi wa kina ili kuwaelewesha wananchi mambo yenye ukweli na sio kuwapotosha.