Mishahara ya wafanyakazi
Shirika linajiendesha kwa kuchechemea. Machi 29 mwaka huu ndipo lilipoweza kulipa mshahara wa Februari. Mshahara wa Machi hadi sasa haujulikani wafanyakazi watapata lini.
Machi 4 mwaka huu, Naibu Mkurugenzi wa Tazara, Damas Ndumbalo, aliliambia gazeti la JAMHURI kuwa mshahara wa Februari ungelipwa Machi 15, lakini badala yake uchunguzi wa Jamhuri umebaini kuwa ilipofika Machi 15 uongozi wa Tazara ulitoa waraka kuwasihi wafanyakazi kuwa wavumilivu, kuwa mshahara ungelipwa Machi 23. Hata hivyo, tarehe hiyo ilipita kimya kimya hadi juzi.
Awali, Ndumbalo aliiambia JAMHURI kuwa Tazara ina wafanyakazi wengi kuliko mahitaji. Alisema ina wafanyakazi zaidi ya 3,000 na wanalipwa mshahara wastani wa dola milioni moja karibu Sh bilioni 1.6, lakini Mleke amesema mshahara wa wafanyakazi wote wa Tazara ni Sh bilioni 1.2 kwa mwezi.
Ingawa mzigo upo pale Tazara na wasafiri wa kawaida wanaendelea kufanya safari zao, bado haionyeshi kama uongozi una mpango mkakati wa kuhakikisha sasa Mamlaka inaanza kutengeneza fedha.
Ndumbalo anasema ingewezekana wafanyakazi wakapunguzwa hadi 1700, shirika lingekuwa na ahueni, lakini Serikali iliyowaajiri ndiyo yenye jukumu la kuwaondoa.
Kwa sasa Tazara ina injini 14 za treni na mabehewa 1,780, hivyo kwa wastani kila injini moja ya treni inahudumiwa na wafanyakazi 200, idadi ambayo ni kubwa kuliko sehemu yoyote duniani. Kwa wastani behewa linapaswa kuhudumiwa na wafanyakazi 50 kutoka hapa hadi Zambia, hivyo 150 hawana kazi ya kufanya.
Umuhimu wa treni
Kwa maelezo ya kitaalamu, treni moja ya Tazara inasafirisha wastani wa behewa 27 zenye uwezo wa kubeba mzigo tani 1,860 kwa wakati mmoja. Mzigo huu ukiingizwa kwenye malori unabebwa na wastani wa malori 50.
Hii maana yake ni kwamba barabara zinaharibika zaidi, muda wa kupakia na kupakua unaongezeka, na gharama za kusarisha mzigo zinakwenda juu.
Zipo taarifa kuwa wakubwa wengi wanamiliki malori, hivyo wanafanya mbinu hadi kutoa hongo kwa watu wenye uwezo wa kuamua treni isifanye kazi ili malori yao yaendelee kuwaneemesha.
Lori moja likisafirisha mzigo kutoka Dar es Salaam hadi Lubumbashi, DRC linatoza hadi dola 7,000 za Kimarekani, karibu Sh milioni 12 kwa safari moja, wakati gharama ya kusarisha mzigo kama huo kwa kutumia reli ni nusu ya gharama hiyo.
Kinachotakiwa hapa ni Serikali kusimama kidete ikasema imetosha, kwa makusudi iamue kufufua reli zote mbili – Reli ya Kati na Reli ya Tazara. Reli hizo kwa pamoja zinaweza kusafirisha mizigo na abiria kwa kasi na ufanisi wa hali ya juu, na nchi ikapata mapato makubwa na uchumi ukakua.
Wateja walalamika
Mmoja wa wateja ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia JAMHURI kuwa Tazara iliishakufa siku nyingi.
“Unapakia mzigo, unalipia kisha unapigiwa simu kuwa treni imeishiwa na mafuta eneo kama Mlimba, inabidi mchangishane wafanyabiashara kwenda kununua mafuta ya kujaza kwenye treni
“…Sielewi aina ya biashara wanayofanya Tazara. Hata kama ni shirika la umma wamevuka mipaka. Serikali inapaswa iingilie kati au wabinfasishwe,” anasema.
Zipo taarifa kuwa baadhi ya watendaji ndani ya Tazara wanashindana kuiba mafuta. Ndumbalo alisema: “Niliagiza wafanyakazi wachukuliwe hatua za kisheria. Uchunguzi umeonyesha kuwa kati ya mafuta yote tunayotumia, asilimia 30 ya mafuta huibwa.
“Sisi tunatumia mafuta ya dola milioni moja kwa mwezi, hivyo kwa kiwango hicho tunaibiwa wastani wa dola 300,000 kila mwezi. Wanaoiba mafuta si wakurugenzi, wanaiba madereva, mafundi na hadi tarehe 19 Februari tuna taarifa kuwa lori mbili za mafuta ziliibwa.”
Ndumbalo anajitetea kuwa Mamlaka inahitaji kuwa na wastani wa dola milioni 3.5 kila mwezi ili liweze kujiendesha kwa ufanisi. Hivyo akasema wakati mwingine hali ya ukosefu wa mafuta inatokana na upungufu wa fedha baada ya mzigo unaosafirishwa na Tazara kuwa umeshuka hadi chini ya tani 500,000 kwa mwaka.
Uwezo wa Tazara kusafirisha mzigo ni tani 5,000,000 kwa mwaka.