Wafanyakazi wataka utangazwe mgogoro

Kwa nyakati tofauti, wafanyakazi waliozungumza na JAMHURI, walisema kuwa Sheria ya Tazara ya Mwaka 1975 imepitwa na wakati kwa kiwango kikubwa.

Sheria hiyo inatamka wazi kuwa milele Mkurugenzi Mkuu lazima atoke Zambia, na kwamba Mkuu wa Chuo cha Mpika, Zambia kinachomilikiwa na Tazara naye kisheria anapaswa kuwa Mtanzania.

Wafanyakazi wanasema mbia anayepata hasara zaidi kutokana na sheria hii ya Tazara ni Tanzania, ambayo hapa ni makao makuu na kuna wafanyakazi wengi Watanzania wanaoishi kwa tabu pasipo ulazima.

Wanasema wakati umefika wa kutangaza mgogoro, kwa ajili ya kupitia Sheria ya Tazara na kutoa fursa kwa wadau kutoa mawazo yatakayoiwezesha reli hiyo kujiendesha kibiashara zaidi.

Kwa sasa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kutumia reli hii ya kisasa inayounganika na mfumo wa reli wa nchi za Zambia, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hii ingekuwa fursa ya Tanzania kuweka kampuni binafsi au Tazara yenyewe kusarisha mzigo kwa wingi, kuiwezesha kupata faida kubwa na ya uhakika kama ilivyokuwa zamani.

Sasa maisha si kama zamani. Nia njema na usimamizi waliokuwa nao waasisi wa reli hii – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Kenneth Kaunda wa Zambia – ni tofauti na sasa. Kwa sasa ama viongozi wachache wanalenga kujineemesha au wapo wasiojua wanachostahili kufanya, hivyo wanaona heri Mamlaka ife maisha yao yaendelee.

Ukiacha hilo, sehemu ya kushushia abiria na mizigo ya Tazara imetengenezwa kisasa kuliko vituo vya nchi nyingi za Ulaya. Reli hii bado ni fursa ya pekee, ingawa jengo la kusubiria abiria linavuja kama mwembe ikinyesha mvua. Fedha zinazohitajika kukarabati jengo hili si nyingi, ila ni ukosefu wa vipaumbele.