Mizigo yarundikana

Gazeti la JAMHURI lilijipenyeza na kutembelea maeneo yote reli ya Tazara Makao Makuu Dar es Salaam na kushuhuhudia maajabu. Kuna mzigo wenye uzito wa karibu tani 22,000 ukisubiri kusafirishwa kwa mwaka mzima sasa.

“Mzigo huu ni wa kampuni ya Miombo. Kampuni hiyo imetuvumilia kuliko maelezo,” anasema Mleke.

Mzigo huo wa mbolea ya kupandia na kukuzia mahindi, unaelezwa kuwa ulitolewa bandarini Julai, mwaka jana, na hadi sasa umefunikwa maturubai baada ya kushindikana kusafirishwa. Mzigo huo ni wazi hauwezi kusafirishwa kwa malori ukaisha, kwani kuna milima ya mbolea.

Inaelezwa kuwa mbolea ingekuwa inasafirishwa nyingi zaidi kuliko hiyo inayopitia Tazara kwa sasa, lakini kinachotokea ni kwamba mzigo unazidi kurundikana bila kusafirishwa.

Hivyo, wamiliki wa mbolea hiyo wameamua kuanza kuusafirisha kidogo kidogo kwa kutumia malori. Wanapobahatisha hutumia usafiri wa Tazara unaosafirisha walau tani 4000 kwa mwezi.

Mleke ameiambia JAMHURI kuwa wafanyakazi wana nia na uwezo wa kufanya kazi, lakini kinachotokea ni kwamba uongozi hautekelezi wajibu wake.

Suala la kutonunua mafuta na vifaa vya kufanyia matengenezo ya mabehewa na injini za treni, linarejesha nyuma juhudi za shirika kujikwamua kiuchumi.

“Hivi kama hujui kusoma, hata picha huioni? Jamani sisi Tazara tunapata mzigo bila kujitangaza. Wateja wanakuja wenyewe tu, lakini tunashindwa kuwaheshimu na kuwasafirishia mizigo yao. Eti useme leo una meneja wa procurement (manunuzi)… mafuta yanaisha ndipo anaanza kuagiza mafuta? Hili haliingii akilini,” anasisitiza Mleke.