Tanzania ilitumia zaidi ya Sh trilioni 4 kununua bidhaa mbalimbali za mafuta kati ya Januari na Novemba mwaka jana kiasi ambacho ni zaidi ya gharama iliyotumika kwa mwaka mzima wa 2018, takwimu rasmi za biashara ya nje zinaonyesha.

Fedha hizo ambazo jumla ni dola milioni 1,941.9 za Marekani (takriban Sh trilioni 4.47) pia ni zaidi ya kiasi kilichotumika kununua mafuta kwa miezi 12 mwaka 2017.

Gharama za kuagiza mafuta mwaka 2018 zilikuwa dola milioni 1,871.5 na kiasi cha dola milioni 1,850.6 zilitumika mwaka 2017. Hii ni sawa na Sh trilioni 4.3 na Sh trilioni 4.25 mtawalia kwa bei ya dola sokoni kwa hivi sasa.

Tanzania huagiza zaidi ya lita milioni tatu za mafuta kwa mwaka ambazo ni pamoja na dizeli, petroli, mafuta ya taa na mafuta mazito ya kuendeshea mitambo.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema gharama za kuagiza mafuta zimekuwa zinapanda miaka ya karibuni kwa sababu ya kuongezeka matumizi yake kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Nyerere na reli ya kisasa (SGR). Miradi hii pia imesababisha kuagizwa kwa wingi bidhaa za kukuza mitaji kama vile vifaa vya usafiri na ujenzi pamoja na mitambo.

Kwa mujibu wa Tathmini ya Hali ya Uchumi kwa Mwezi (MER) ya hivi karibuni, thamani ya mafuta yaliyoagizwa kipindi cha mwaka unaoishia Novemba 2019 iliongezeka kwa asilimia 30.2 hadi dola milioni 2,078.6. Kiasi hiki kilikuwa ni sawa na asilimia 23.1 ya fedha zote zilizotumika kuagiza bidhaa nje ya nchi kwa kipindi hicho ambazo zilikuwa ni dola milioni

8,997.7.

Jumla ya dola milioni 11,004.5 (karibu Sh trilioni 25.3) zilitumika kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya nchi wakati wa mwaka unaoishia Novemba 2019. Kwa mwaka mzima wa 2018, biashara hii ilikuwa na thamani ya dola milioni 10,338.2 (Sh trilioni 23.8) ukilinganisha na dola milioni 9,591.6 (Sh trilioni 22.1) mwaka uliotangulia.

Wiki iliyopita, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema kwa hivi sasa nchi ina akiba ya mafuta ya kutosha yanayoweza kudumu kati ya siku 28 hadi 56. Kiongozi huyo alitoa ufafanuzi huo alipokuwa akikabidhi tuzo zilizoandaliwa na Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa watoa huduma wake mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kuna ziada ya mafuta ya dizeli ya siku 28 lita milioni 197, petroli ziada ya lita milioni 97.04 kwa siku 38 na mafuta ya ndege ziada ya lita milioni 30.9 kwa siku 56.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, aliliambia JAMHURI kuwa kwenye mwaka wa fedha wa 2018/19 taifa lilinunua bidhaa za mafuta zenye ujazo wa lita bilioni 3.28.

Mafuta hayo ni pamoja na dizeli lita karibu bilioni 1.9, petroli lita bilioni 1.13, mafuta ya taa lita milioni 41.8, mafuta ya ndege lita milioni 201.8 na mafuta ya mitambo lita takriban milioni 16.2.

“Matumizi yetu ya bidhaa za mafuta kwa siku ni kama ifutavyo: petroli lita milioni 3.6, dizeli lita milioni 5.7, mafuta ya taa lita 130,000, mafuta ya ndege lita 610,000 na mafuta mazito ya kuendeshea mitambo lita 210,000,” Kaguo anasema.