- Maeneo bado ni mengi watanzania waitwa
- Fursa ujenzi wa mitambo, ununuzi wa dhahabu
- Nyang’wale kinara ukusanyaji maduhuli
ZAIDI ya leseni 4,000 zipo katika utaratibu wa kutolewa katika maeneo manne ya Mkoa wa Kimadini Mbogwe mkoani Geita, huku wazawa na wawekezaji kutoka nje wakitakiwa kuchangamkia fursa zilizopo mkoani humo.
Akizungumza katika mahojiano, Afisa Madini Mkazi wa Mbogwe, Mhandisi Jeremiah Hango amesema maeneo yaliyotengwa ni Nyamikonze ambapo leseni 81 ziliweza kugawiwa kwa wachimbaji wadogo, kuna eneo la Mwamakiliga leseni 27 zilitengwa.

“Maeneo mengine ni Bukombe kijijini leseni 140 na sasa hivi mchakato wa Kigosi ambapo takribani leseni 4,000 zimeweza kutengwa,”amesema Mhandisi Hango
Amesema, zoezi la ugawaji bado linaendelea na kwamba fursa zilizopo zikitumiwa vizuri serikali itaweza kukusanya kiasi kikubwa cha maduhuli.
“Nawakumbusha wamiliki wa leseni ambao wameshikilia leseni katika mkoa wetu wa kimadini Mbogwe wazifanyie kazi leseni hizo, nyingi hawazifanyii kazi, kuna leseni za utafiti ambapo ukienda saiti watu wanaofanya utafiti ni wachache sana, amesema Mhandisi Hango na kuongeza.

“Vile vile niwakumbushe kama leseni hizo hawatazifanyia kazi tutazifuta na kuwapa watu wengine wenye nia ya kufanyia kazi leseni na sio kuzishikilia,”
Aidha amesema, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya madini katika Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali yamekuwa yakiongezeka kila mwaka tangu mkoa huo wa kimadini ulipoanzishwa mwaka 2021.
“Mwaka 2021/2022 tuliweza kukusanya Shilingi Bilioni 21, mwaka 2022/2023 tulikusanya Shilingi Bilioni 22, mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 tumekusanya Shilingi Bilioni 27 mwaka huu wa fedha mpaka sasa hivi tumeweza kukusanya Shilingi Bilioni 22,”amesema Mhandisi Hango na kuongeza,
“Tunaamini kwa mwelekeo huu tunaoenda nao mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka tutaweza kuzidi lengo tulilokusanya katika mwaka wa fedha uliopita.” amesema.

Ameendelea kusema kuwa asilimia 90 ya madini yanayochimbwa Mbogwe ni dhahabu, yapo pia madini ujenzi.
“Mapato ya Mbogwe asilimia 60 tunayapata katika wilaya ya Nyang’wale ndiko uchimbaji wa madini kwa kiasi kikubwa unafanyika, lakini kuna juhudi ambazo zinafanyika kwa upande wa Serikali kuhakikisha uwezeshwaji wa wachimbaji kuzitumia fursa zilizopo.
“Tuna fursa nyingi katika mkoa wetu wa kimadini Mbogwe, kuna fursa ya biashara ya madini, tuna masoko mawili ya Nyang’wale na Masumbwe, wafanyabiashara wakubwa wa madini ‘dealers’ wenye uwezo wa kununua hii dhahabu waje waombe leseni.
Pia amesema kuna fursa ya ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ambapo kwa sasa ni michache kwa maana wachimbaji wamehamasika kuachana na matumizi ya zebaki kwenda kwenye matumizi ya mitambo ya kuchenjulia ya CIP.


