· Wachimbaji wahamasika kuachana na Zebaki

· Waita wawekezaji kujenga mitambo ya kuchenjulia

JUMLA ya leseni 1356 zimetolewa katika halmashauri tatu za Mkoa wa Kimadini Kahama ambazo ni Ushetu, Msalala na Kahama huku wazawa na wawekezaji kutoka nje wakitakiwa kuchangamkia fursa zilizopo mkoani humo.

Akizungumza Afisa Madini Mkazi wa Kahama Leons Welengeile amesema, leseni za utafutaji madini zipo jumla 77 ambazo zinahusisha utafutaji wa dhahabu kwa asilimia kubwa, leseni kubwa za uchimbaji zipo katika maeneo mawili ambayo ni migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi.

“Kwa sasa shughuli zinafanyika katika mgodi wa Bulyanhulu na mgodi wa Buzwagi upo katika hatua za ufungaji mgodi,”amesema Leons

Amesema, mbali na hatua za ufungaji mgodi pia katika eneo la mgodi wa Buzwagi yapo maeneo yaliyotengwa maalum (Special Economic Zone) kwa ajili ya shughuli za uwekezaji wa viwanda na yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya taasisi za elimu.

“Katika eneo hilo kwa sasa takribani kilomita za mraba 13 zimetengwa na kuwa eneo maalum la uwekezaji ambapo kuna shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo uwekezaji katika utengenezaji wa vifaa na vipuri mbalimbali vinavyotumika migodini, viwanda vya utengenezaji baruti na viwanda vya uongezaji thamani madini,”amesema Leons na kuongeza,

“Pia kuna maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa taasisi za elimu hususan elimu ya ufundi ambazo zimelenga kukuza uelewa na utaalam kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya Wilaya ya Kahama wa shughuli mbalimbali za migodini.

“Mbali na hivyo, tunasimamia leseni saba za uchimbaji wa kati na mbili zipo katika hatua ya ufungaji mgodi, lakini pia kuna leseni nne zipo kwenye hatua ya uendelezaji na moja ipo kwenye hatua ya uchimbaji.”amesema.

Leons amesema pia, hadi mwezi Februari 2025 wametoa jumla ya leseni 1270 za uchimbaji mdogo na asilimia 40 ya leseni hizo ndio zimeendelezwa na asilimia 60 zipo kwenye hatua mbalimbali za utafiti.

Aidha, amesema kuna fursa nyingi katika Mkoa wa Kimadini Kahama ambazo ni fursa za biashara ya madini ambapo lipo soko moja na vituo vitano vya ununuzi wa madini.

Pia amesema kuna fursa ya ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ambayo kwa sasa ni michache kwa maana wachimbaji wamehamasika kuachana na matumizi ya zebaki kwenda kwenye matumizi ya kuchenjua kupitia mitambo ya CIP.

Amesema, katika Mkoa wa Kimadini Kahama, wana miradi mitatu ya uendelezaji wachimbaji wadogo kwa njia ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi ‘technical support agreement’, ambayo ni Shangaza, LHT na Super Mabomu.

“Awali shughuli za uzalishaji katika maeneo hayo zilikuwa ni chache ambapo wastani ilikuwa kilo moja au mbili za madini ya dhahabu ndio zilikuwa zikizalishwa, lakini kutokana na uwekezaji uliofanywa kwa njia ya Mkataba wa Msaada wa Kiufundi, tumeshuhudia maeneo hayo kwa sasa uzalishaji umeongezeka hadi kufikia wastani wa kilo tano za madini ya dhahabu kwa mwenzi,” amesema.