Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

ZAIDI ya kampuni 50 zimeweza kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane).

Hayo yamebainishwa na Afisa Kumbukumbu kutoka Brela Faridi Hoza wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema Brela katika maonesho hayo wanatoa Huduma mbalimbali ikiwemo Usajili wa majina ya biashara, usajili wa makampuni, usajili wa alama za biashara, usajili wa Ataza, leseni.

“Tuko hapa katika maonesho ya Nanenane kutoa huduma mbalimbali na rai yetu kwa Wafanyabiashara na Wakulima waweze kutembelea banda letu la Brela kwasababu kuna mengi mazuri ambayo tumewaandalia.

“Kwamfano ukija hapa kama una changamoto yoyote tunakuhudumia papo kwa papo na kama unakwama sehemu yoyote tunakusaidia. Lakini pia tunahudumia Wakulima, Wafanyabiashara kuweza kufanya maombi ya usajili,” amesema kuongeza kuwa:

“Tunafanya Usajili wa papo kwa papo kitu ambacho si rahisi. Kwahiyo kama wewe ulikuwa una changamoto kuna sehemu ulikwama ukija hapa tunakusaidia. Lakini pia tunatoa Elimu na mpaka sasa zaidi ya kampuni 50 tumeweza kuzisajili katika maonesho ya Nanenane,” amesema.

Mmoja wa wananchi waliotembela banda la Brela, Yahaya Hassan ameshukuru kwa huduma alizopatiwa na kutoa wito kwa wananchi wengine waweze kutembelea.

“Huduma niliyokuja kuipata ni kufatilia taarifa za Kampuni kitu ambacho nimeweza kikifanya kwa haraka kwani nisingekuja kwenye maonesho ingenilazimu kusubiri siku tatu na zaidi.

“Lakini kwa kuwa timu ya Brela iko hapa hapa kila kitu unahudumiwa hapa hapa, kwahiyo nawashauri na wengine ambao wana changamoto ambazo zinahusu kampuni au majina ya kibiashara waweze kusogea Brela ili wapate Huduma kwa haraka,” amesema Hassan.