Na Mary Margwe, JamhuriMedia, Simanjiro
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga amesema zaidi ya sh.bil.19 zimetengwa kwaajili ya ujenzi wa kujenga barabara na madaraja katika Halmashauri zote za Mkoa huo.
Hayo alizungumza jana wakati akikagua zahanati mpya ya kitongoji cha Oltotoi Kijiji Cha Kimotorock, Kata ya Loiborsiret, wilayani Simanjiro Mkoani humo, mbele ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo Kiria Laizer, Mkuu wa Wilaya hiyo Fakii Raphael, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Baraka Kanunga Laizer, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Gracian Max Makota, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Tumaini Sebastian Lukumay.

Sendiga amesema hayo kufuatia changamoto za ubovu wa barabara za Simanjiro iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kimotorock Elia Parnelo, ambapo Mkuu huyo amesema wamepewa zaidi ya sh.bil. 19 kwaajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na madaraja ambazo zimeidhinishwa Kwa ajili ya kukamilisha hilo, kinachosubiriwa ni mvua tu ikatike ili wakandarasi waingie barabarani.
” Tunafahamu Mkoa wetu, tangu Mwaka Jana mwezi wa 9-10 mvua zilianza kuonyesha hadi hivi Sasa bado haijaisha, tumepewa fedha nyingi sana Kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara pamoja na madaraja, ambapo zaidi ya sh. bil.19 tumepatiwa” amesema Sendiga.
” Lakini sisi kama Mkoa tuliona ni busara na hekina tusiitupe hii fedha kwasababu tukianza ujenzi wa barabara Leo, mnajenga asubuhi greda inapita asubuhi na kesho kabla barabara haijaisha mvua imenyesha barabara inabomoka tena, fedha inakua inapotea bure” amesema Mkuu huyo.
Aidha Sendiga amefafanua kuwa barabara mbaya zaidi ni za wilaya ya Mbulu, Hanang’ na Kiteto, huku akisema kuwa barabara za Simanjiro zina nafuu ukilinganisha na hizo , hivyo waendelee kuwa na subra na uvumilivu ili mvua zikate , kipindi cha jua kikianza tu wakandarasi wanaingia barabarani, kwani fedha zipo barabara zitachongwa.

” Barabara za Simanjiro zina nafuu kidogo, ulienda Mbulu, Hanang’ na Kiteto hali ya barabara ni mbaya kweli kweli, kwahiyo tunaendeelea kuwaomba kuwa na subra kidogo ya uvumilivu mvua zikate, tunajua kile kipindi cha jua kikianza tu wakandarasi wanaingia barabarani kwa sababu fedha zipo ” amesema Mkuu huyo.
” Kwahiyo tutachonga barabara hizo na sio tu kwa Simanjiro bali za Mkoa mzima huku kwenu Simanjiro kidogo kuna nafuu, lakini hata tukichonga barabara Sasa hivi mvua ukija tunarudi pale pale pa mwanzo , kwahiyo tubumiliane kidogo mvua zikate Sasa tuanze matengenezo ya barabara zetu” ameongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga.
Hata hivyo Mkuu huyo aliwapongeza wananchi hao kwa kujitokeza kwa wingi, Kwa kwenda kwenye ziara hiyo na kumsikiliza na kuweza kutoa maelekezo ya Serikali.
