– Awaasa vijana kutunza afya, kuwa waaminifu

– Awataka kujiepusha na migogoro isiyo na tija

Azindua mkutano wa umoja wa vijana migodini

Mwandishi Wetu

Zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinazotolewa kwenye migodi ya madini nchini zinatolewa na watanzania huku vijana wakiaswa kutunza afya zao na kuepuka makundi hatarishi ili kuzifikia fursa zilizopo kwenye migodi.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 7, 2024 na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akimwakilisha Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde kwenye ufunguzi wa kongamano la mafunzo ya fursa katika Sekta ya Madini kwa vijana sambamba na umoja wa vijana wa migodini (Tanzania Youth in Mining), kwenye ukumbi wa EPZA uliopo viwanja vya Bombambili ambako Maonesho ya Saba ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Geita yanayoendelea.

Mhandisi Lwamo amesema, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imekuwa kinara kuhakikisha makundi yote yanashiriki ipasavyo katika Sekta ya Madini ambapo imekua ikitoa leseni za uchimbaji wa madini, vibali vya huduma kwenye migodi ‘local content’ na kuongeza kuwa mpaka sasa hivi zaidi ya asilimia 90 ya watoa huduma ni watanzania.

Amesema, Taifa lolote ili liendelee linapaswa kuwa na vijana wenye malengo na tija na kuwataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo fursa katika uchimbaji, fursa za biashara na watoa huduma migodini ‘Local Content’.

“Fursa kama hizi ili muweze kuzifikia ni lazima muwe kwenye vikundi na Serikali kupitia vikundi vyenu itaweza kuwafikia na kutimiza lengo la vijana na kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla,”amesema na kuongeza.

“Vijana, jambo kubwa na la msingi niwaase ili kufikia ndoto zenu ni lazima mtunze afya zenu, mnaweza kuwa na ndoto kubwa za mafanikio lakini kama afya zenu mnachukulia mzaha mzaha hamtazitimiza tunzeni afya,”amesisitiza Mhandisi Lwamo.

Pia, amewaasa kuwa waaminifu kwa kuwa vikundi vingi vya vijana vinakufa kutokana na kukosa uaminiufu.

“Tumeona vikundi vingi vinavurugika wakati mwanga umeanza kuchomoza, mmetoka kwenye shida, imefikia wakati wa kupata faida mnaanza kuleta vurugu kwenye vikundi, hatutaki vijana ambao mna ndoto kubwa ya kutufikisha kwenye ‘Vision ya 2030’ ya Madini ni Maisha na Utajiri mkaishia njiani, kwa kuingiza tamaa, kutokuaminiana ambako huzaa vurugu zisizo na faida,”amesema Mhandisi Lwamo.

Aidha, amesema Serikali siku zote imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kuhakikisha inaendelea kutoa leseni kwa wachimbaji vijana ili wanufaike na rasilimali madini na kwamba ili kuendelea kama taifa, kuna vitu vya msingi ambavyo vitapaswa kuzingatiwa ikiwemo kutunza na kuendeleza maliasili ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia.

“Tutaziendeleza kwa kuwa na elimu ya kutosha ya kuendesha rasilimali hizi kibiashara, hivyo tumieni fursa za elimu ya ujasiriamali ili muweze kufikia ndoto zenu kwa kunufaika na maliasili zilizopo.

“Sio wote mtachimba, naamini wapo wenye vipaji vya uchimbaji, wengine biashara, kusambaza baruti, wengine uchenjuaji wa dhahabu au madini yatakayopatikana, kila mtu ajiangalie kipaji alichonacho akifanyie kazi kwa kuchangamkia fursa, Tume tupo kuwapa mwongozo ili mfikie ndoto zenu, hivyo zingatieni mafunzo mtakayopewa hapa hakikisheni hamtoki bure,”amesema Lwamo.

Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Madini Taifa, Hamis Mohamed amesema umoja huo uliundwa kwa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rais Samia aliagiza tuunde umoja ili changamoto zetu ziweze kutatuliwa kwa urahisi pia tupate sehemu ya kusemea vitu vinavyotuhusu kama vijana katika Sekta ya Madini ikiwemo kusaidiwa kuzifikia fursa mbali mbali zilizopo,”amesema Hamis na kuongeza

“Wachimbaji vijana tuna changamoto nyingi, Serikali haiwezi kututatulia changamoto zetu zote, zipo kupitia umoja wetu tunakabiliana nazo na kuzitatua sisi wenyewe,”amesisitiza.

Uzinduzi wa umoja huo wa vijana umekwenda sambamba na mafunzo ambayo yametolewa na Mtaalam kutoka Tume ya Madini, Mjiolojia John Maganga ambaye alimwakilisha Afisa Madini Mkazi wa Geita, Samwel Shoo, ambapo amezungumzia fursa za kiuchumi, maadili kwa vijana na kwamba dhamira ya Serikali ni kuboresha maisha katika Sekta ya Madini.

Please follow and like us:
Pin Share