Kampuni ya kutengeneza mabasi aina ya Yutong kwa kushirikiana na Benbros Motors Ltd, imezindua basi la kisasa lenye uwezo mkubwa ili kupunguza ajali za mara kwa mara.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Masoko, Albert Currussa, wa Benbros Motors Ltd anasema kwamba kampuni hiyo imeingiza sokoni gari hilo F12Plus lenye uwezo wa kuhimili barabara za aina zote.
Albert anasema kwamba basi hilo lina uwezo mkubwa wa kuzuia ajali kutokana na ubora wake, kutokana na utatifi uliofanywa na wataalamu kabla ya kuundwa kwake.
“Kutokana na kujali maisha ya abiria, kampuni yetu ililazimika kutumia muda wa miaka miwili kuunda mfumo wa mabasi haya mapya ya F12Plus, basi hili limeanza kuundwa mwaka 2014 na lilitakiwa kuzinduliwa Mei 2015 lakini kutokana na kuendelea kuliboresha tumezidisha miezi sita,” anasema Albert.
Pia anaeleza kuwa kutokana na ubora wa mabasi ya kampuni hiyo, katika kipindi cha miaka mitano, imefanikiwa kuuza mabasi 500 katika nchi za Afrika, na kwa mwaka 2015 pekee imeuza mabasi 67,000 duniani yenye thamani ya dola ya Marekani bilioni 4.
Anaeleza kuwa pamoja na kuingiza kiasi hicho cha fedha, Yutong hutenga asilimia 10 ya mauzo yake kwa mwaka na kuyatumia katika tafiti mbalimbali ili kuboresha bidhaa zao ziweze kuendana na mahitaji ya wateja husika.
Katika uzinduzi huo, Benbros motors imetoa ofa kwa wateja wa kwanza wa F12Plus watakaonunua mabasi hayo katika kipindi cha kufunga mwaka kwa kuwapatia garatii ya miaka miwili, pamoja na kuyapatia huduma zote mpaka yatakapotembe na kufikisha kilometa 200,000.
Katika uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, amewataka Yutong kujenga kiwanda cha kuunganisha magari hapa nchini.
Nape amesema kwamba Serikali imefurahishwa na ujio wa basi hilo la kisasa lenye uwezo wa kupunguza ajali ambazo zinagharimu maisha ya Watanzania.
“Nayapongeza makampuni haya mawili yaliyoweza kuungana kufanya kazi pamoja, ni vyema kufuatilia na kutathmini sifa za gari hilo na kufanya uamuzi. Ajali zimeua Watanzania wengi sana, ninyi ni mashahidi, imefika mahali watu wanataka kuzoea hali hii,” anasema Nape.
Pia amewahimiza Benbros Motors na wabia wao kujenga kiwanda cha kuunganisha magari yao nchini na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kuweza kufanikisha hilo ili kuendana na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
“Tunawaomba muhamishie kiwanda cha kuunganisha magari yenu nchini, msiyalete yakiwa yameungwa. Mkiungia hapa nchini mtasaidia kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira,” alisema na kuongeza:
“Serikali inawahakikishia kuwa itatoa ushirikiano wa kutosha kuweza kuwekeza kwa kuleta viwanda vyenu nchini, msiogope maana hii ni Serikali ya kazi,” anasema Nape.
Kufuatia ombo hilo la Serikali, Albert ameiambia JAMHURI kwamba kampuni yao inalichukua na kulifanyia kazi ili kuangalia uwezekano wake ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na viongozi husika.
Pia amesema kwamba mabasi hayo yanauzwa kwa gharama ndogo tofauti na mabasi mengine ambapo basi moja jipya linauzwa kwa dola za kimarekani 138 na kuendelea kutokana na mahitaji ya mteja.
Pamoja na unafuu huo alioutaja, pia amebainisha kuwa gharama za uendeshaji ni ndogo ikiwa ni pamoja na usalama wa hali ya juu kwa watumiaji wake.
“Hatuwezi kulipuuza, ninachoweza kukwambia sasa ni kwamba kwa vile na viongozi wangu wapo hapa, tutakaa na kulijadili kwa kina ili kuona jinsi ya kufanya, lakini nakuhakikishia ya kwamba inawezekana na pia itakuwa imetusaidia kibiashara na nchi kwa ujumla ukizingatia Serikali inahamasisha wawekezaji katika viwanda,” anasema Albert.
Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency The Kilimanjaro iliyopo Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na wafanyabiashara wa mabasi ya abiria kutoka Tanzania na Zambia.