Yoweri-Museveni.president-of-UgandaKatika Uchaguzi Mkuu wa Uganda uliofanyika Februari 18, mwaka huu, waangalizi 50 waliwasili kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakiongozwa na Rais (mstaafu) wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Yeye na timu yake waliwasili Uganda Februari 9 na wakaondoka mara baada ya uchaguzi.

Kikosi cha Mzee Mwinyi kilikuwa na watu kutoka nchi za EAC, isipokuwa Uganda yenyewe kwa vile nchi ya uchaguzi hairuhusiwi kujitathmini yenyewe. Kwa hivyo walitoka Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi pamoja na wajumbe kutoka Bunge la EAC (EALA), Makao Makuu ya EAC na asasi za kiraia.

Dhima yao imekuwa ni kushuhudia mtiririko mzima wa uchaguzi, kuanzia maandalizi yalivyofanywa kabla ya upigaji kura hadi kuhesabiwa na kutangazwa matokeo. Walitakiwa washuhudie ngazi zote hizi kisha watoe maoni yao iwapo mambo yaliendeshwa kwa mujibu wa utaratibu na sheria au la.

Waganda walipiga kura ili kumchagua rais wa nchi hiyo na wabunge. Huu ulikuwa ni uchaguzi wa sita tangu Rais Yoweri Museveni ashike madaraka miaka 30 iliyopita, chini ya chama chake cha National Resistance Movement (NRM).

Museveni na chama hicho walishika madaraka Januari 29, 1986 baada ya kuendesha vita vya msituni. Mwaka 1995 iliundwa katiba ambayo iliweka kikomo cha mihula miwili kwa rais. Lakini mwaka 2005 Bunge la Uganda lilibadili katiba hiyo na kuondoa kikomo ili Museveni aendelee kukalia kiti cha urais bila kikomo.

Wabunge wengi walipinga kuondolewa kwa kikomo hicho, lakini tunaambiwa utawala wa NRM ulitumia mamilioni ya dola ili ‘kuwashawishi’ wabunge wakubali.

Katika uchaguzi huu wa majuzi kulikuwako wagombea tisa wa urais, lakini watatu ndio maarufu zaidi. Nao ni Rais Museveni (NRM), Dk. Kizza Besigye (Forum for Democratic Change – FDC) na Amama Mbabazi (Go Forward – GF) ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Museveni.

Wakati kikomo cha urais kinaondolewa katika katiba, Mbabazi alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ndiye aliyetetea kuondolewa kwa kikomo. Amekuwa kada mkuu wa NRM kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka jana.

Ili kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa usalama na utulivu, polisi iliongeza nguvu zake kwa kuomba msaada kutoka majeshi ya ulinzi, magereza na usalama wa taifa. Wanajeshi 70,000 wametumika kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), yaani majeshi ya kulinda mipaka ya nchi sasa yanatumika kuwadhibiti raia siku ya kupiga kura.

Pia walichukuliwa askari magereza na wanamgambo. Hata askari wa kuwalinda wanyamapori dhidi ya majangili nao walichukuliwa kwenda kulinda vituo vya upigaji kura. Kwa ujumla idadi ya mapolisi, wanajeshi na askari wa kila aina waliotumika kwa kazi hiyo ni 150,000.

Ukiachia hao, kulikuwako pia maelfu ya vijana waliojiunga na kikosi kisicho rasmi kilichoitwa crime preventer (wazuiaji uhalifu). Kazi yao eti ni kutunza usalama wa raia wakati wa uchaguzi.

Hawa ni vijana “waliojitolea” kulinda usalama wa jamii. Wengi wao ni kutoka NRM. Wamefunzwa na polisi ingawa hakuna sheria inayowatambua kama kikosi cha usalama. Mkuu wa Polisi, Jenerali Kale Kayihura aliwaambia vijana hao kuwa badala ya kutumia marungu watapewa bunduki  ili “kuilinda nchi isivamiwe”.  

Kayihura pia aliwahi kutamka kuwa “hatutatoa nchi kwa wapinzani ili wachafue amani tuliyoijenga.” Hii ina maana gani? Je, ripoti ya Mzee Mwinyi ilizungumzia hayo?

Kama hiyo haitoshi, siku chache baadaye, Justine Kasule Lumumba, Katibu Mkuu wa NRM, aliuambia mkutano wa kampeni katika Wilaya ya Wakiso kuwa vyombo vya dola viko tayari kutumia risasi na kumuua mtu yeyote ambaye anaonekana akivuruga amani na utulivu. Yaani polisi inajifanya mahakama na hukumu ni kifo. Je, waangalizi watasema nini?

Wiki chache kabla ya uchaguzi polisi iliteremsha shehena ya silaha, zikiwamo gari za polisi, maji ya kuwasha na gesi ya machozi. Hivi ndivyo polisi ilivyojitayarisha kulinda usalama. Na kazi hiyo waliifanya kama walivyokusudia.

Siku tatu kabla ya uchaguzi, kulitokea mvutano kati ya polisi na wafuasi wa Besigye katika Jiji la Kampala. Watu kadhaa walijeruhiwa, wakati polisi iliporusha gesi ya machozi. Wapinzani wakazuia barabara na kurusha mawe.

Hii ni baada ya polisi kumkamata Besigye kwa saa kadhaa. Gari lake lilikuwa likipitia mjini Kampala, katika msafara wake uliosindikizwa na mamia ya wafuasi. Ndipo polisi walipotumia gesi ya machozi kuwatawanya wafuasi hao na wakamkamata Besigye.

Baada ya muda walimwachia bila kumfungulia mashtaka na wakampeleka hadi nyumbani kwake. Walipoulizwa, polisi walisema walimzuia kwa “usalama wake”. Hata hivyo, Besigye mara moja alitoka nyumbani na kuingia mitaani. Tena mara hii alikusanya watu wengi zaidi barabarani. Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kukamatwa na mara hii walikamatwa pia wafuasi wake 20.

Hii si mara ya kwanza kwa polisi kutumia nguvu za silaha dhidi ya waandamanaji, pamoja na gesi ya machozi na hata risasi za moto. Katika uchaguzi wa mwaka 2011, watu tisa walipoteza maisha mjini Kampala, wakati polisi walipowadhibiti waandamanaji wasiokuwa na silaha. Mamia wengine walikamatwa.

Besigye tayari ameshagombea urais mara tatu dhidi ya Museveni na kila mara hutangazwa kuwa ameshindwa. Jenerali David Sejusa, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa chini ya NRM, ametamka kuwa Besigye alishinda uchaguzi wa 2006, lakini NRM iliiba na kuchakachua kura na Museveni akatangazwa mshindi. Sejusa alisema haya baada ya kukimbilia Uingereza mwaka 2013. Huyu ni jenerali aliyewahi kushirikiana na Museveni katika vita ya misituni.

Besigye aliwahi kuwa daktari wa Museveni tangu wakiwa msituni hadi alipoamua kuwa Museveni amekuwa dikteta na akaachana naye. Katika kampeni yake amekuwa akihutubia mikutano mikubwa kote nchini.  Wananchi wengi wakihudhuria na kutoa michango ya kila aina – mafenesi , kuku, mbuzi, chakula na kadhalika –  ikiashiria jinsi alivyokuwa akiungwa mkono na wakulima masikini. Wengine walidiriki hata kumzawadia punda ili aweze kusafiri hadi vijijini.

Ama kwa upande wa Museveni, yeye amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 30 sasa. Hivyo kama atashinda mara hii, basi atakuwa amekaa madarakani kwa miaka 35 na hapo atakuwa amevunja rekodi ya marais wa Kiafrika waliotawala kwa muda mrefu.

Inasemekana Museveni anamtayarisha mtoto wake, Brigedia Muhoozi Keinerugaba ili kushika madaraka ya urais. Hii ilipingwa na wenzake katika jeshi. Mmojawao ni Jenerali Sejusa, Mkuu wa Upelelezi, ambaye alipinga hadharani na akakamatwa na kuwekwa gerezani. Ndipo alipoachiwa akakimbilia Uingereza.

Wapinzani wengine ni makamanda waandamizi kama Jenerali Aronda Nyakairima, Meja Jenerali James Kazini, Kanali Jet Mwebaze na Kanali Noble Mayombo ambao wote wamefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Rais Museveni mwenyewe amewahi kusema kuwa hatakubali hata kidogo kuachia madaraka kwa wapinzani wake. Amesema yuko tayari kurudi msituni. Haya aliyasema Desemba 2015 wakati akihutubia Wilaya ya Namutumba.

Alisema: “Eti kuna watu wanasema Museveni ang’atuke. Wanataka niachilie utajiri wa mafuta ili waje wafaidi wao? Wanaosema hayo watanifanya nirudi msituni.”

La kustaajabisha ni kuwa ni Museveni huyu huyu ambaye aliwahi kusema kuwa viongozi wa Kiafrika wanaokaa madarakani kwa muda mrefu ndiyo wanaosababisha vurugu katika bara hili. Sasa baada ya kukaa miaka 30, na kufikia umri wa miaka 71, analenga kuweka rekodi ya muhula wa tano.

Amekuwa moja kati ya watawala wa Afrika waliokalia urais kwa muda mrefu. Wengine ni marais wa Rwanda, Burundi na DR Congo.

Si hayo tu, bali sasa anataka kushindana na marais wenzake kama Jose Eduardo dos Santos wa Angola na Teodoro Obiang wa Equatorial Guinea (wote wawili wametawala tangu mwaka 1979), Robert Mugabe wa Zimbabwe (tangu mwaka 1980) na Paul Biya wa Cameroon (tangu mwaka 1982).

Wengi wameingiwa hofu kuwa majeshi yanaweza kuingilia kati iwapo Museveni atashindwa. Ni vizuri ikumbukwe kuwa Museveni mwenyewe ni Jenerali wa jeshi tangu wakati wa vita ya misituni.

Mara nyingi tunasikia nchi za magharibi zikiwalaumu watawala wa aina hii. Lakini huo ni unafiki. Ukweli ni kuwa Marekani na mataifa ya magharibi yamekuwa yakimuunga mkono Museveni, hasa kutokana na majeshi yake yalivyo msitari wa mbele kupigana na al-Shabab nchini Somalia.

Ndiyo maana mataifa hayo si tu yamekuwa yakimpa “misaada” ya kijeshi, bali pia hufumbia macho na masikio kuhusu matendo na maneno yake yanayokinzana na demokrasia na utawala bora.

Badala yake majeshi ya Marekani yamekuwa yakiwafunza wanajeshi wa Uganda wakati raia wa Uganda wanaajiriwa kama mamluki kwenda kusaidia uvamizi wa Marekani huko Iraki. Huu ndiyo ‘urafiki’ wa Museveni na Marekani.

Wakati wa uchaguzi kulikuwa na kasoro kadha ambazo ziligundulika. Moja ni hesabu ya wapigakura walioandikishwa ambao ni 15,297,197. Tume ya uchaguzi (UEC) ilisema 8,027,803 ni wanawake na 7,249,394 ni wanaume. Sasa tukijumlisha idadi hizi tunapata 15,277,197 wakati kwa mujibu wa UEC jumla ya raia waliojiandikisha ni 15,297,197.

Ndipo swali linaulizwa, hii ziada ya 20,000 imetoka wapi?  Wengine walisema hawa ni wapigakura hewa ambao walitumiwa ili kuzidisha kura za Museveni.

Mkuu wa chama cha Democratic Party (DP), Norbert Mao tayari amewasilisha kesi katika Mahakama ya Katiba akiituhumu UEC kuwa imeboronga daftari la wapiga kura. Yeye Mao mwenyewe alikataliwa kugombea ubunge kwa madai kuwa jina lake halikuwamo katika daftari.

Hata mwenyekiti wa UEC, Badru Kiggundu aliwaonesha waandishi wa habari kura bandia zilizochapishwa na wagombea ambao walipanga kuzitumia ili kuongeza idadi ya kura zao. Wanaweza pia kuzitumia ili kuchafua jina la UEC na hivyo kubatilisha uchaguzi, amedai Kiggundu. Hata hivyo, alipoulizwa ni nani watu hao alishindwa kuwataja, ila alisema ameripoti jambo hilo kwa polisi.

Hii ndiyo baadhi ya mikanganyiko iliyojitokeza wakati wa uchaguzi. Wenyewe kule wanaita ‘manyanga manyanga”.

Uchaguzi huu wa Uganda haukuendeshwa kwa misingi ya itikadi wala dira. Hakuna mgombea aliyeahidi kubadili mfumo. Kila mmoja aliahidi atakuwa meneja bora zaidi ya mwenziwe. Suala zima ni utawla bora. Si Besigye wala Mbabazi aliyehoji mfumo uliowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), mfumo wa soko huria/holela ambao umezaa ufisadi.

Ni mfumo huu uliowekwa tangu mwaka 1987 ndiyo uliosababisha jamii kugawanyika katika tabaka la matajiri wa kupindukia na masikini wa kutupwa. Haya yanaonekana wazi nchini Uganda. Ni nchi tajiri ambayo ina mafuta ardhini yanayokisiwa kuwa mapipa bilioni 6.5. 

Kwa hiyo suala zima ni ulaji.  Kila mmoja amekaa mkao wa kula. Kila mmoja anasema sasa ni zamu yake.