Mweusi aliyetwaa taji la Miss Israeli 2013
*Atimiza ndoto ya kukutana na Rais Obama
Ilikuwa Februari, mwaka huu wakati mrembo Yityish Aynaw (21), mzaliwa wa Ethiopia alipotwaa taji la ulimbwende la Miss Israel katika mashindano ya kitaifa yaliyofanyika nchini humo.
Ushindi huo ni wa kihistoria, kwani ni mara ya kwanza katika nchi ya Israel mtu mweusi kutwaa taji la urembo kitaifa.
Yityish alizaliwa Ethiopia katika Kijiji cha Chahawahit, kaskazini mwa nchi hiyo, karibu na mji wa Gondar. Baba yake alifariki akamwacha akiwa bado mdogo.
Mama yake pia alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu na kumwacha Yityish akiwa na umri wa miaka 12. Maisha yalibadilika, Yityish akawa kama amechanganyikiwa. Yeye na kaka yake aitwaye Yellek waliamua kuondoka Ethiopia kwenda Israeli na kuishi huko pamoja na babu na bibi yao, ambao pia ni Waethiopia lakini wanaishi nchini humo.
“Niliamua kuondoka Ethiopia kwa sababu nilipata uchungu sana wa roho, lengo langu lilikuwa kuondoka eneo lile na kuelekea sehemu nyingine ili nisahau yote yaliyopita na kuanza maisha mapya,” alisema mrembo huyo katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Marekani (CNN).
Akiwa na umri mdogo, Yityish alikumbana na changamoto za kujifunza lugha mpya, utamaduni na changamoto nyingine zilizotokana na hali ya kuanza maisha mapya katika nchi ya Israel. Kwa kipindi kirefu kumekuwa na wimbi la raia wa Ethiopia kukimbilia Israel. Yityish alikutana na hali kama hiyo, hivyo ikamfanya aishi maisha kama ya wenyeji wa nchini humo.
Bila kuonesha hali yoyote ya aibu, aliweza kumudu mila zote zikiwamo zile za Kihebrania na hatimaye baada ya kumaliza shule alijiunga na Jeshi la Israeli.
“Ni kweli ilikuwa ni miaka mitatu ya kihistoria, nilitumikia jeshi, nilijifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na lile la kujitambua mwenyewe, ilikuwa ni hatua ya maendeleo kwangu. Nilikuwa binti wa miaka 19, lakini jeshi lilininyoosha na pia nilijifunza ukakamavu katika maisha,” alisema.
Baada ya kumaliza mafunzo ya jeshi, alipata ajira katika duka la kuuza nguo. Yityish alikuwa mrefu, mwenye sura ya mvuto lakini hakutarajia katika maisha yake kama angejiunga katika tasnia ya urembo au kushiriki katika mashindano ya aina hiyo. Ni rafiki yake aliyemshawishi, tena kwa kupeleka jina lake katika orodha ya washiriki wa mashindano ya urembo.
“Mimi na rafiki zangu tulicheka sana juu ya hatua hiyo. Kusema ukweli sikuwa na muda, jeshi ni jeshi halitaki mzaha, kwa hiyo nilipomaliza jeshi rafiki yangu alinisisitiza na kuniambia kuwa sasa sina la kujitetea,” alisema mrembo huyo.
Yityish anatamani siku moja apate watoto halafu awahadithie historia hii ambayo kwake ni kitu ambacho kimempatia mwanga katika maisha yake.
Tangu apate ushindi huo Februari, mwaka huu, maisha yake yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Kwanza jina lake limekuwa maarufu kila kona ndani na nje ya Israel na katika mitandao yote ya mawasiliano duniani. Yityish alikaribishwa katika dhifa maalum wakati Rais Barak Obama wa Marekani alipofanya ziara nchini humo.
“Hii ni hatua ambayo sikuitarajia, Rais Obama ni kiongozi ambaye nilikuwa natamani kufuata mfano wake. Wakati nikiwa shuleni niliwahi kufanya mradi uliohusisha kazi zake, kwa hiyo ni mtu ambaye historia yake ninaifahamu vizuri.
“Najua ni mambo gani ambayo amefanya na amekuwa akifanya. Kwangu ni kama mwalimu au mtu ambaye natamani kuiga mfano wake. Kusalimiana naye kwangu ni kama nimekamilisha kitu fulani katika mzunguko wa maisha yangu,” alisema.
Yityish anaona kuna kila hali ya mabadiliko juu ya suala la ubaguzi wa rangi. Lakini pia anasema kuna baadhi ya rafiki zake ambao wamekuwa wakitendewa vitendo vya kibaguzi kutokana na rangi zao.
“Sula hili lilinigusa na hata kama halijatokea kwangu najua ubaguzi wa rangi upo katika nchi hii na sehemu nyingine duniani, ni kitu ambacho kinatakiwa kukomeshwa,” alisema Yityish.
Mrembo huyo ambaye awali maisha yake yalikumbana na mitihani ya hapa na pale, sasa anajiona kuwa binti ambaye anatarajia kuwa mfano bora katika jamii. Kwa sasa anataka kuwa mtaalamu wa mavazi na kusaidia jamii katika masuala mbalimbali kama mfano wa kuigwa.
“Natamani kuwa na familia kubwa yenye watoto wengi, nyumba nzuri, mwisho wa siku watoto wangu nitawahadithia historia yote ya maisha yangu.
“Kuwa mrembo mweusi wa kwanza katika nchi hii ninawakilisha utamaduni wangu kwa sababu kupitia kwangu mimi natakiwa kuwa mfano bora,” anasema Yityish, ambaye anatarajia kuiwakilisha Israel katika mashindano ya urembo ya dunia (Miss Universe) mwakani.