Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU 

Mashabiki wa soka duniani wanafahamu kwamba kwa sasa Klabu maarufu ya Chelsea ya Uingereza inapita katika wakati mgumu sana. 

Wanakopita Chelsea kwa sasa kunafahamika kwa Kiitaliano kama ‘Vea De ra Rosa’ (yaani njia ya mateso). 

Chelsea, mabingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, haipo tena mikononi mwa bilionea na shabiki maarufu wa soka, Roman Abramovich, raia wa Urusi. 

Miamba hawa wa soka wamo mikononi mwa watu wengine, licha ya kuwa Roman bado ndiye mmiliki wake.

Pamoja na Chelsea kuwapo katika, au kupitia katika nyakati hizi ngumu, lakini mambo mengine yanakwenda vema tu!

Masuala ya posho na mishahara kwa wachezaji, makocha na maofisa wengine wa klabu, inaendelea kutolewa pamoja na Serikali ya Uingereza kumuwekea vikwazo bilionea mmiliki wa klabu hii.

Unadhani ni kwa nini mambo yako hivyo kwa upande wa mmiliki, lakini mambo mengine yanaendelea vema klabuni hapo?

Jibu lake ni rahisi sana tu. Wenzetu wametengeneza mifumo imara inayoziendesha klabu zao bila kutegemea ‘mfuko’ wa mmiliki au mfadhili mmoja pekee.

Sikumbuki mara ya mwisho ni lini Roman alipokwenda Stamford Bridge, uwanja wa nyumbani wa Chelsea, kutazama mechi ya Chelsea katika miaka ya hivi karibuni! Kwa hakika kuna kipindi kirefu tu kimepita.

Pamoja na kutokwenda au kuonekana moja kwa moja akijihusisha na shughuli za Chelsea, mifumo imara aliyoiweka imefanya shughuli za timu kuendelea.

Roman kwa sasa amezuiwa kuingia Uingereza huku mali zake mbalimbali zikifilisiwa au zikiwa katika mpango wa kufilisiwa kutokana na madai ya kuwa karibu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Putin anadaiwa kukiuka hali za binadamu na mikataba ya kimataifa kwa kuingiza majeshi yake nchini Ukraine.

Kabla ya hali ya Chelsea kufikia hivi ilivyo kwa sasa, hatujawahi kuwasikia nyota wa klabu hii wakilalamikia ishu za mishahara yao au marupurupu mengine kadhaa.  

Haijawahi kusikika wala kufikirika kwamba kuna siku itafika kwa Klabu ya Chelsea kushindwa kusafiri kwenda ndani au nje ya nchi. 

Haijawahi kutokea au kufikirika kuwa ipo siku Chelsea watashindwa kusajili wachezaji mahiri na kukiimarisha kikosi chao. 

Chelsea inalipa vema mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wake, inasafiri vema. Kokote timu inakotakiwa kwenda, inakwenda. Inasajili mastaa ghali na kuwalipa mishahara minono.

Yageuze maisha hayo wanayopitia Chelsea kwa sasa na kuyaleta kwa klabu zetu kubwa za Tanzania; Simba na Yanga. Klabu hizi huwa zinatia huruma ukikuta au zikifika katika nyakati za kulazimika kusimama zenyewe kwa miguu yao.

Hawa wafadhili kama akina Mo na GSM wanastahili pongezi na heshima kubwa sana, kwa kuwa hawa wakikaa kando hata kwa siku moja tu, timu zinaingia katika maisha magumu.

Nyota wao wanaondoka kwenda kutafuta sehemu watakayolipwa vema. Timu zinashindwa kusafiri kwa wakati. 

Kulipana mishahara mwisho wa mwezi inakuwa shida. Mwenyekiti anamtafuta katibu, katibu anamtafuta mwenyekiti. 

Tunapopiga kelele timu zetu ziende kwenye usasa ni kutokana na mambo kama haya. Leo GSM na MO wakiondoka Jangwani na Msimbazi ni ‘MISIBA’.

Kuanzia hapo timu zitaanza kurudi katika mfumo wa kutembeza mabakuli. Timu zitarudi katika mfumo wa kusajili wachezaji wa kiwango cha kawaida. 

Sehemu ambayo timu ilikuwa na usafiri wa anga, itarudi kwenye usafiri wa kimbinyiko. Ukubwa wa timu zetu unatokana na siku alivyoamka tajiri, lakini zenyewe ni maskini.