Na Khalif Mwenyeheri

Yanga imeshindwa kupata matokeo mazuri katika mechi zake za hivi karibuni na kuifanya timu hiyo kupunguza nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), hali hiyo inawafanya Yanga kuwa na kazi kubwa ya kufukuzia ubingwa.

Katika msimamo wa ligi, Yanga inaongoza ligi baada ya kujikusanyia alama 55, katika mechi 22, huku Azam ikishika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 48, huku ikicheza michezo 21, hali hiyo inaifanya ligi kuwa ngumu kwani Simba inashika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia alama 36 huku ikiwa na michezo saba mkononi.

Endapo Simba itashinda mechi za viporo, itajikusanyia alama 57, alama mbili zaidi ya mahasimu wao Yanga. Presha ya Ligi Kuu Tanzania Bara imetanda zaidi baada ya Yanga watakapochuana na Simba Jumamosi hii.

Endapo Yanga itapoteza katika mchezo huo dhidi ya Simba, itapoteza matumaini ya kubeba ubingwa katika msimu huu wa 2018/2019, ambapo ligi haina mdhamini.

Azam nayo haipo mbali, kwani inashika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 48, ipo nyuma kwa mchezo mmoja, ikilinganishwa na Yanga.

Yanga ilianza kwa kupoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Stand United katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga waliponyukwa bao 1-0, lililofungwa dakika za majeruhi. Huo ndio ukawa mwanzo wa kuonja shubili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Mechi nyingine zilizofuata Yanga iliambulia sare dhidi ya Coastal Union, mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mechi iliyofuata dhidi ya Singida United, nayo ikaleta suluhu ya 0-0, mechi hiyo ilichezwa katika dimba la Namfua.

Katika mzunguko wa kwanza Yanga ilipambana kufa – kupona licha ya ukata wa fedha unaowakabili, kwani hawakuweza kuruhusu kufungwa katika mechi yoyote zaidi ya kutoka sare dhidi ya timu za Ndada na Simba.

Ligi ya msimu huu imekuwa ngumu ukilinganisha na ligi ya msimu uliopita, kwani mpaka ilivyokuwa hivi sasa Simba ilijihakikishia nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Baadhi ya timu zilizopanda daraja zimeleta ushindani mkubwa kwenye ligi kuu kutokana na kuzisumbua timu kubwa, timu hizo ni kama KMC na Alliance, hivyo zimeleta changamoto kubwa.

KMC imeshinda mechi tano mfululizo, wakati msimu uliopita timu za Mbao na Lipuli ndizo zilizokuwa zinaleta ushindani mkubwa kwa timu kubwa, lakini hivi sasa timu nyingi zinacheza kwa malengo ili kukaa katika nafasi nzuri ya ligi kuu.

Tafsiri ya ligi ya msimu huu inaonyesha kuwa timu nyingi zina nafasi kubwa ya kukaa nafasi za juu katika msimamo wa ligi.

Ugumu mwingine unaojitokeza kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni kutokana na kukosekana kwa uwiano sawa, baadhi ya timu zimecheza mechi nyingi kuliko timu nyingine. Kuna timu zimecheza mechi 25, nyingine 15, nyingine 22, hivyo baadhi ya timu kuwa na viporo vingi.

Hivyo, TFF kupitia Bodi ya Ligi wana jukumu la kuhakikisha timu zote zinalingana, kwa kuwa na idadi sawa ya michezo walizocheza.