Na Tatu Saad,JAMHURIMedia
Uongozi wa Klabu ya Yanga umeweka hadharani mipango na mikakati waliyonayo kuelekea mchezo wao wa raundi ya tano wa kimataifa dhidi ya US Monastir.
Katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa Machi 19, mwaka huu, Yanga watakuwa wenyeji wa US Monastir kutoka Tunisia katika uwanja Wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Makamu Rais wa Mabingwa hao wa ligi ya Tanzania Bara ‘Yanga’ Arafat Haji, amesema wao kama klabu wameshaanza mikakati ya kuichakaza vibaya US Monastiri katika ardhi ya nyumbani ikiwa kama sehemu ya kisasi chao baada ya kufungwa mabao 2-0 nchini Tunisia.
Pia amesema bado hawajafika safari yao na mchezo wao dhidi ya US Monastir ndio tiketi ya robo fainali hivyo wana mikakati mikubwa ya kuhakikisha wanashinda ili kwenda hatua inayofuata.
Arafat amesema huo mchezo sio tu tiketi yao ya kwenda robo fainali,bali wanauchukulia mchezo huo kama fainali, licha ya kuwa na historia ya kushinda mechi mbili mfululizo katika ardhi ya nyumbani moja dhidi Tp Mazembe ya Congo 3-1 na AS Real Bamako ya Mali 2-0.
“Licha ya kushinda michezo miwili mfululizo nyumbani, lakini bado kazi hatujamaliza, tunahitaji kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha tunawafunga US Monastir Uwanja wa Mkapa, kwani huu ndio mchezo wa Fainali kwetu, ili kujihakikishia kucheza Robo Fainali,” amesema Arafat.
Hata hivyo Arafati ameongeza kuwa wao kama viongozi wanaingia msituni kuweka mikakati mizito wakiwa na malengo ya kuchukua alama zote muhimu katika kila mchezo ili kuendelea kuwa sehemu nzuri na kuchukua bonasi za Rais Samia.
“Kama uongozi wenu tunaingia msituni kuanzia sasa nanyi iwe hivyo kuanzia mchezo wa ligi, malengo yetu kutoacha alama yoyote nyumbani, sisi ndio wananchi wenye ubora tutakaoendelea kuwa mfano wa kuchukua bonasi zote za Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Arafat.
Yanga bado inakula kiyoyozi katika nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi D ikiwa na alama saba ikiongozwa na Us Monastir ya nchini Sudan ikijibebea alama 10 kwenye michezo minne iliyocheza.