DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

Vinara wa Ligi Kuu, Yanga, wanaisaka kimyakimya rekodi iliyowekwa na Simba miaka 12 iliyopita ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kufungwa.

Rekodi hiyo ya Simba ipo hatarini kwa sasa wakati ambao Yanga wanaonekana kujipanga vema kuusaka ubingwa walioukosa kwa miaka minne mfululizo.

Yanga wanaongoza ligi wakiwa na pointi 51 baada ya kucheza mechi 19 (kabla ya mchezo dhidi ya Namungo) ikishinda 16 na sare tatu. 

Simba wapo nafasi ya pili na pointi 41, baada ya kucheza mechi 19 wakishinda mechi 12, sare 5 na kufungwa mara mbili.

Pamoja na mafanikio hayo ya Yanga, si Kocha Nasreddine Nabi wala viongozi wa mabingwa hao wa kihistoria wanaozungumzia kuisaka rekodi ya Simba, lakini wanachama na mashabiki wameonyesha wazi kuwa lengo lao ni kuona timu ikitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo wowote.

Wanachama na mashabiki wa Yanga wamekwenda mbali zaidi wakajiwekea lengo la kuchukua mataji yote mawili; Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Mara ya mwisho Yanga kutwaa mataji yote mawili ilikuwa ni msimu wa 2016, kabla ya kupisha utawala wa Simba ambao misimu miwili 2019/20 na 2020/21 ilitwaa mataji yote.

Ndoto ya Yanga kutwaa ubingwa bila kufungwa inabebwa na safu yake ya ulinzi inayoundwa na Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, David Bryson, Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, Paul Godfrey ‘Boxer’ huku viungo wakabaji wakiwa Bangala, Khalid Aucho, Zawadi Mauya na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambayo imekuwa imara zaidi msimu huu ikiwa imeruhusu mabao matano tu hadi sasa.

Michezo ambayo Yanga wameruhusu wavu kuguswa ni sare ya 1-1 dhidi ya Namungo, ikishinda 2-1 dhidi ya Biashara United, wakaichapa Tanzania Prisons 2-1 kabla ya kuichakaza Ruvu Shooting 3-1.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ikiongozwa na kinara wa ufungaji mabao Fiston Mayele mwenye mabao 11, Saido Ntibazonkiza (6) na Feisal Salum ‘Fei Toto’ (4) imekuwa tishio, jambo linalofanya ndoto ya ubingwa Jangwani kuwa nyeupe.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga tayari imefunga mabao 33, ikiwa imezifunga timu zote katika ligi hiyo isipokuwa Simba pekee iliyopata suluhu katika mchezo waliokutana.

Yanga inahitaji kushinda mechi saba kati ya kumi zilizobaki kutangaza ubingwa kwa kufikisha pointi 72 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote. 

Michezo mitano ijayo ya Yanga ni dhidi ya Simba wa Aprili 30, ukifuatiwa na Ruvu Shooting utakaochezwa Mei 4, kabla ya kuwakaribisha vibonde wa ligi, Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa (Mei 21), watakwenda mkoani Mara kuivaa Biashara United (Mei 24), watarudi jijini Dodoma (Juni mosi) kuwakabili Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Simba wanaonekana ndio kikwazo kikubwa kwa Yanga katika kutimiza ndoto yao ya kutwaa ubingwa bila kufungwa msimu huu, jambo linalofanya mchezo baina yao Aprili 30 kuwa wa ushindani zaidi.

Habari njema kwa Yanga kuelekea mchezo huo ni wapinzani wake Simba kuwa na muda mfupi wa kupumzika kabla ya mchezo huo muhimu.

Simba wanakwenda Afrika Kusini katika kuhakikisha wanamaliza kwa kishindo robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, huku siku sita baadaye wakiwa na kibarua cha kuilinda rekodi yao dhidi ya Yanga.

Simba watakuwa na kibarua kizito katika mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates utakaofanyika Jumapili ijayo nchini Afrika Kusini.

Simba wanakwenda katika mchezo wa Aprili 30, wakiwa na mambo mawili; kwanza, kuhakikisha wanashinda ili kuilinda rekodi yao ya msimu 2009/10 walipotwaa ubingwa bila kupoteza mechi yoyote. Pili ni kurudisha matumaini ya kutetea ubingwa msimu huu. 

Msimu wa 2009/10, Simba ikiwa chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri, walitwaa ubingwa bila kufungwa mchezo wowote.

Katika michezo 22 waliyocheza, walipoteza pointi nne pekee, baada ya kutoka sare mbili tu dhidi ya African Lyon na Kagera Sugar; wakishinda mechi 20, na kujikusanyia pointi 62, huku wakifunga mabao 50 na kufungwa mabao 12.

Simba iliyoanza msimu huu kwa kusuasua wanajua wazi kupoteza mchezo dhidi ya Yanga kutawaweka katika nafasi ngumu zaidi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu wakiwa wamebakiza michezo 10, kabla ya kumaliza msimu.

Pia Simba wanaweza kupoteza taji la Kombe la ASFC wakiwa na mchezo kiporo wa robo fainali dhidi ya Pamba FC ya Mwanza na iwapo watashinda, nusu fainali watacheza dhidi ya Yanga.

Ratiba ya mechi za mwisho za Yanga, Simba

YANGA

Aprili 30, 2022: Yanga vs Simba (Benjamin Mkapa)

Mei 4, 2022:      Ruvu Shooting  vs Yanga (Benjamin Mkapa)

ROUND 23, TBA: Yanga vs Prisons (Benjamin Mkapa)

Mei 21, 2022: Yanga vs Mbeya Kwanza (Benjamin Mkapa)

Mei 24, 2022: Biashara United vs Yanga (Karume, Mara)

Juni 1, 2022: Dodoma VS Yanga (Jamhuri, Dodoma)

Juni 8, 2022:  Yanga vs Coastal Union (Benjamin Mkapa)

Juni 11, 2022: Yanga vs Polisi Tanzania (Benjamin Mkapa)

ROUND 29, TBA: Mbeya City vs Yanga (Sokoine, Mbeya)

June 19, 2022: Yanga vs Mtibwa Sugar (Benjamin Mkapa)

SIMBA

Aprili 30, 2022: Yanga vs Simba (Benjamin Mkapa)

Mei 3, 2022:  Namungo vs Simba (Ilulu Stadium, Lindi)

ROUND 22, TBA: Simba vs Ruvu Shooting (Benjamin Mkapa)

ROUND 23, TBA:  Simba vs Kagera Sugar (Benjamin Mkapa)

Mei 22, 2022: Geita Gold vs Simba (Nyankumbu)

Mei 25, 2022: Simba vs KMC (Benjamin Mkapa)

Mei 31, 2022: Azam FC vs Simba (Azam Complex)

Juni 9, 2022: Simba vs Mbeya City (Benjamin Mkapa)

Juni 12, 2022: Simba vs Mtibwa Sugar (Benjamin Mkapa)

ROUND 29, TBA: Tanzania Prisons vs Simba (Mandela Stadium)

Juni 19, 2022: Mbeya Kwanza vs Simba SC (Sokoine Stadium)