Yanga wakiendelea kumsujudia Fei Toto wataingia katika hatari ya kushusha morali ya timu. Siamini kama Fei Toto ndio engine ya Yanga, engine ya Yanga ni Nabi mwenyewe wala sio mchezaji yeyote awaye yote ndio maana kikosi cha Yanga Kila mchezaji anacheza na matokeo yanapatikana.
Hakuna kitu muhimu wanachohitaji Yanga zaidi ya pesa za GSM na akili ya Nabi kwa sasa. Fei Toto anayeondoka kambini Yanga akiwa na mkataba wa miaka miwili mbele ameonekana kuwa bora katika nyakati hizi za Nabi. Nabi ni aina ya kocha anayeinua viwango vya wachezaji na kuhakikisha wanapata nafasi ya kucheza.
Aliposajiliwa Aziz Ki wengi tuliamini Fei Toto atakaa benchi lakini Nabi alitengeneza mazingira ya kuhakikisha Aziz Ki na Fei Toto wanacheza pamoja na alipoulizwa alisema hawezi kumuacha Fei Toto nje kwa maslahi ya nchi na kiwango cha mchezaji husika.
Nabi ana uwezo wa kuwatumia wachezaji alionao na akawa na matokeo mazuri zaidi ya sasa kwa sababu kizunguzungu cha kulazimisha Aziz Ki na Fei Toto wacheze pamoja kitakuwa kimefika mwisho. Mechi yao dhidi ya Azam, Aziz Ki akiwa amejua timu ipo mabegani mwake alifanya makubwa na pengo la Fei Toto halikuonekana.
Ninaamini Fei Toto ni mchezaji mkubwa na bora kwa sasa hapa nchini kwetu lakini alichokifanya hakikuonesha ukubwa tunaodhani anao. Yanga walistahili kuboresha maslahi yake na Fei Toto alistahili kuhitaji zaidi lakini sio kwa mtindo alioutumia ambao umeonesha utoto wa hali ya juu kwake binafsi na menejimenti yake.
Fei Toto ana kiwango kikubwa uwanjani lakini sio kiwango kikubwa zaidi ya ukubwa wa Yanga wala hana ukubwa wa kumzidi Nabi ambaye anaweza kuinua viwango vya wachezaji wengi tu kama alivyofanya kwa Farid Musa, Joyce Lomalisa na sasa anapambana kuinua kiwango cha Tuisila Kisinda.
Yanga wanapaswa kuuheshimu uwezo wa Nabi kuliko mchezaji yeyote, mashabiki wa Yanga wanapaswa kuwaheshimu GSM na wadhamini wengine kuliko kuwalaumu kwa sababu ya mchezaji mmoja ambaye hana adabu na mikataba. Mashabiki wa Yanga wainue mikono waseme daima mbele, nyuma mwiko. Wana Nabi Wana GSM basi yatosha.