Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kama ulifanikiwa kutazama mchezo wa Derby ya Kariakoo kati ya Yanga Princess vs Simba Queens uliochezwa jana katika dimba la KMC Complex Mwenge jijini Dar, basi utakubaliana na mimi kwamba golikipa wa Yanga Princess, Rita Akarekor (23) ndiye aliyechangia kwa asilimia kubwa kuwapa Yanga ushindi mbele ya watani wao baada ya kuwa watumwa kwa misimu kadhaa iliyopita.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya ngao ya jamii kwa wanawake, ambao ulimalizika kwa sare ya mabao (1-1) na kuwalazimu kwenda kwenye mikwaju ya Penati, Rita ambaye ni Raia wa Nigeria, aliokoa mikwaju mitatu ukiwemo ule wa mwisho wa kuamua mchezo.
Bao la kwanza la Yanga lilifungwa dakika ya kwanza ya mchezo na Agness Pallangyo, ambalo lilidumu kwa Dakika 90, ndipo Jentrix Shikangwa alipotibua mipango kwa kusawazisha kwenye dakika tano za nyongeza, ambapo mikwaju ya penati ilikuwa kama ifuatavyo..
YANGA PRINCESS Vs SIMBA QUEENS
Danai Bhobho ✅ – Jentrix Shikangwa ✅
Neema Paul ❌ – Ester Mayala ❌
Uzoamaka ✅ – Precios Christopher ✅
Agness ✅ – Aisha Juma ✅
Wema Richard ❌ – Vivian Corazone ❌
Diana Antwi ✅ – Fatuma Issa ❌
Baada ya kumalizika kwa mchezo mashabiki walimshangilia Rita kwa kumuita jina la Golikipa wa Yanga SC, Djigui Diarra wakimfananisha nae kutokana na ubora aliouonesha.
Rita alitua Yanga Princess akitokea klabu ya Delta Queens inayoshiriki ligi kuu ya Nigeria, ni kipa tegemeo wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Nigeria.
Yanga Princess kwa sasa wanajiandaa na mchezo wa fainali dhidi ya JKT Queens, utakaochezwa Jumamosi Oktoba 05, 2024.