Na Isri Mohamed
Klabu ya soka ya Yanga inatarajia kushuka dimbani kesho Novemba 26, kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika (CAFCL) hatua ya makundi, dhidi ya AL Hilal ya Sudan.
Akizungumza kwenye mkutano wa wanahabari, Kocha wa Yanga, Saed Ramovic amesema licha ya ubora wa wapinzani wao, lakini Yanga ni klabu kubwa na ina uwezo wa kuapata matokeo mazuri.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kwenye ligi ya mabingwa, ni jambo la kheri sana kwangu kushiriki mashindano haya makubwa nikiwa na timu kubwa ya Young Africans SC, Falsafa yangu kubwa ni nidhamu na kujituma Napenda kuona wachezaji wakicheza kama timu, haijalishi unatumia mfumo gani kama wachezaji wako hawana umoja ni ngumu kupata matokeo”
“Young Africans SC ni timu bora sana, lakini tunakwenda kucheza na timu bora pia hivyo tunahitajika tuwe makini sana. Tunapaswa kuwa na utayari kiakili na kisaikolojia kwani tunakwenda kwenye mechi ngumu sana. Hata hivyo ninayo furaha kubwa sana kuiongoza Klabu kubwa kwenye mashindano makubwa”
Nae Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amewataka mashabiki wao kusahau matokeo mabaya waliyoyapata kwenye michezo miwili ya mwisho ya ligi kuu na badala yake kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti wachezaji wao.
“Matokeo ya mechi zilizopita ni mechi za Ligi, sasahivi tunakwenda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, niwaombe mashabiki waondoe hofu na waje kwa wingi uwanjani, Tusahau yaliopita na kesho tuanze safari nyingine”