Rais John Magufuli kuna kitu alikifanya kizuri zaidi Jumapili. Siku ambayo Yanga iliivaa Simba na kuondoka na ushindi wa bao 1-0, katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ile kwenda uwanjani tu, ilikuwa hamasa tosha na kuonyesha kuna ‘derby’ moja kubwa zaidi Afrika kuliko zote kwa sasa. Hata ujio wa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, ulidhihirisha hilo.
Sijui ni ujio wa Dk. Magufuli na Ahmad au la, lakini kwa mara ya kwanza tulishuhudia mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikiamuliwa na waamuzi sita, wakiongezwa waamuzi wasaidizi wawili wanaokaa karibu na kila lango.
Na tukashuhudia mechi ambayo kwa kiasi kikubwa waamuzi hawakutuangusha ukilinganisha na madudu tuliyokuwa tunayashuhudia katika mechi za Ligi Kuu katika siku za hivi karibuni.
Kubwa zaidi, wachezaji wenyewe wakatuonyesha burudani ya kutosha uwanjani. Mchezo ulikuwa ni wa ufundi mkubwa na kudhihirisha kuwa makocha wa timu zote mbili waliifanya kazi yao sawasawa.
Kwa upande mwingine wachezaji nao wakatuonyesha kuwa wamewaelewa walimu wao kwa kuweza kutafsiri vema mafundisho waliyopewa.
Hakukuwa na kuzidiana sana kimchezo ingawa mwisho wa siku Yanga ilionekana imezidi kwa sababu tu ilishinda mechi. Lakini, goli lililofungwa haliwezi kuzua lawama zozote kwa mchezaji yeyote wa Simba. Unachoweza kufanya kama mwanamichezo ni kumsifia mfungaji kwa jinsi alivyoupiga ule mpira kwa kulenga kwa ufundi mkubwa. Golikipa yeyote angeweza kufungwa goli lile la Bernard Morrison kwani mpira ulikwenda kwa kasi sana kiasi kwamba jitihada za ukuta wa Simba na za kipa wake, Aishi Manula, kuuzuia zilishindwa kabisa.
Kwa hakika ujio wa watu hao wawili ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hasa Rais Magufuli, umetukumbusha mambo mengi. Mara ya mwisho Magufuli kufika uwanjani hapo kwenye mechi ya soka ilikuwa ni katika mechi ya Simba ambayo iliishia kupoteza mbele ya Kagera Sugar. Jumapili alirejea tena na Simba ikapoteza mbele ya Yanga. Lakini huo ni mfanano tu, hatuwezi kusema kuwa Rais Magufuli ndiye aliyesababisha Simba wafungwe.
Mashabiki nao wameitendea haki mechi ile kwa kuujaza uwanja kiasi kwamba hata Rais wa CAF aliukubali ‘muziki’ wao.
Ahmad Ahmad
“Sijawahi kuona pambano lenye ushindani na lenye kuleta mashabiki wengi kama hili. Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa na kama CAF tunajifunza kutoka hapa.
“Nimeulizia kuhusu wadhamini na kila kitu juu ya uendeshaji wa ligi hii, kuna mabadiliko yanatakiwa yafanywe, ila hili ndilo soka la Afrika, nimefurahi mno.”
Rais Magufuli
“Huu ndio ustaarabu wa Watanzania na naamini wengi watajifunza kutoka hapa.”
Sven van der Broeck
“Ni mchezo wangu wa pili dhidi ya Yanga, lakini ninapenda kuwapongeza kwa ushindi walioupata na ni moja kati ya timu pinzani ambazo zinakufanya uwe na presha wakati wote.”
Luc Eymael
“Nimekuja Yanga na kukutana na moja kati ya mechi ngumu, sijawahi kuona hili na limenifanya nijue kwa nini nipo hapa. Ila kubwa zaidi soka la Tanzania lifanyiwe mageuzi kidogo tu na litatoka hapa lilipo.
“Hii ndiyo Yanga, na hii ndiyo Tanzania. Nimefurahi kuwepo hapa.”