Hatimaye kindumbwendumbwe cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kinafikia tamati Jumamosi wiki hii, kwa timu zote 14 zinazoshiriki michuano hiyo kuwa dimbani kwenye viwanja tofauti.
Kuhitimishwa kwa ligi hiyo kutakuwa kumekamilisha idadi ya mechi 182 zilizopaswa kuchezwa na timu hizo kwa msimu mzima, na pia kutatoa bingwa mpya wa soka Tanzania Bara baada ya waliokuwa mabingwa watetezi Yanga kulitema taji hilo.
Safari ya timu hiyo ya kuutema ubingwa ilianza rasmi baada ya kupokonywa pointi zake tatu na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF), zile ilizozipata kwa kuifunga Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, mwezi uliopita. Hatua hiyo ya TFF ilitokana na Yanga kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Canavaro’ huku akiwa na kadi nyekundu ya kosa la kupigana uwanjani, hivyo alitakiwa kukosa mechi tatu mfululizo lakini akakosa mbili tu.
Mbali na hizo, timu hiyo pia ilipoteza pointi sita nyingine kwa kufungwa mfululizo mechi mbili ilipocheza na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na baadaye dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Katika kuhitimishwa kwa ligi hiyo Jumamosi wiki hii, mechi zitakazochezwa na viwanja vyake ni kati ya mahasimu wawili – Yanga na Simba (Uwanja wa Taifa Dar es Salaam), JKT Oljoro na Polisi Dodoma (Sheikh Amri Abeid, Arusha) wakati Ruvu Shooting Stars na Villa Squad zitapepetana kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi, Kibaha.
Nyingine ni kati ya Toto African na Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), African Lyon na JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam na Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United itakayopigana vikumbo na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Tayari Moro United na Polisi Dodoma zimeshashuka daraja msimu ujao. Villa Squad na African Lyon nazo zinasubiri ifike Jumamosi ili kujua hasa ipi itang’oka pia. Nafasi za timu hizo zinachukuliwa na Prisons ya Mbeya, Polisi Morogoro na JKT Mgambo ya Tanga. Hizo zimepanda daraja ziliposhika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara – hatua ya tisa bora – iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, na kumalizika wiki moja iliyopita.
Mechi ya kufunga pazia la Ligi Kuu kati ya Simba na Yanga ndiyo inayotazamiwa kuteka hisia za mashabiki wa soka nchini ikilinganishwa na mapambano mengine yote ambayo pia yatachezwa siku hiyo. Yanga itaingia uwanjani ikiwa haina nafasi ya kuwa bingwa wala kushika nafasi ya pili, lakini itakuwa na kazi moja tu ya kutibua mipango ya Simba ya kutaka kunyakua taji hilo msimu huu.
Timu hiyo ambayo sasa inafundishwa na beki wake mahiri wa zamani, Fred Felix ‘Minziro’ Kataraiya ‘Majeshi’, itataka kuikata maini Simba kwa kuifunga idadi yoyote ile ya mabao ili hata ikitwaa ubingwa – kutegemea na matokeo ya jumla ya mechi zote za Azam msimu huu – isherehekee kwa kilio na matanga.
Katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Yanga iliifunga Simba bao 1-0 kwenye uwanja uleule zinapokutana tena Jumamosi, lakini vijana hao ambao ni maarufu kama Wekundu wa Msimbazi, chini ya kocha Milovan Cirkovic, nao hawatakubali kufungwa mara ya pili na mahasimu wao hao msimu huu.
Wakati Yanga ikijivunia mastraika wake wa kigeni, Khamis Kiiza na Kenneth Asamoah, Simba katika upande wake itawategemea zaidi washambuliaji Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango. Hadi sasa, Kiiza ametikisa nyavu mara 11 na kufuatiwa kwa pamoja na Asamoah, Okwi na Mafisango wenye mabao 10 kila mmoja.
Mbali na washambuliaji hao ambao wote ni raia wa kigeni; Kiiza na Okwi wakiwa Waganda huku Asamoah akitokea Ghana na Mafisango nchini Rwanda, Yanga pia ina Davies Mwape na Simba ikiwa na Felix Sunzu wenye mabao sita kila mmoja, wote wakitokea Zambia. Simba itaingia uwanjani ikiwa na pointi 59 na endapo itashinda mechi hiyo itakuwa nazo 62, hivyo itakuwa bingwa wa moja kwa moja maana haziwezi kufikiwa na Azam ambayo ndiyo pekee iliyobaki nayo katika mbio hizo.
Kabla ya mechi ya juzi, Jumapili wakati ilipoumana na Toto African kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, Azam ilikuwa na pointi 53, hivyo kwa kushinda mechi hiyo ya Jumamosi wiki hii dhidi ya Kagera Sugar, timu hiyo inayonolewa na kocha Stewart Hall itakuwa na pointi 59 kama ilizonazo Simba hivi sasa.
Hatua hiyo itafanya ubingwa huo uamuliwe kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa kama ilivyokuwa mwaka jana. Yanga nayo ilinyakua taji hilo katika mechi ya mwisho. Hadi kufikia sasa, Simba imetikisa nyavu za timu pinzani mara 42 huku ikiwa imefungwa mabao 12, lakini kabla ya kucheza na Toto African juzi, Jumapili, Azam ilikuwa imefunga mabao 37 na kufungwa 11.
Katika hali hiyo, kushinda kwake mechi mbili za mwisho kwa kuanza na Toto African na hatimaye dhidi ya Kagera Sugar, Jumamosi wiki hii, kutaifanya Azam nayo ifikishe pointi 59, hivyo endapo Simba itafungwa na Yanga hata bao 1-0 tu itakuwa imeukosa ubingwa huo siku ya mwisho.
Hata hivyo, Azam itatakiwa kufunga mabao yasiyopungua saba au manane katika mechi zake mbili za mwisho, halafu isiruhusu kufungwa zaidi ya bao moja huku ikiomba Simba ifungwe au kutoka sare isiyozidi bao 1-1 katika mechi yake dhidi ya Yanga, Jumamosi.
Ikitokea hivyo, Yanga itakuwa imeikata maini Simba na kuibeba Azam iliyoibamiza vibaya timu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani (zoefu ya ligi za nyumbani) za kuwa klabu bingwa ya kandanda Tanzania Bara msimu huu. Hapana shaka hatua hiyo itakapokelewa kwa nderemo, vifijo na hoihoi nchini kote na mashabiki wa timu hiyo kongwe kuliko zote zinazoshiriki Ligi Kuu.
Lakini kama Simba itaifunga Yanga, ubingwa huo kwake utakuwa na thamani kubwa zaidi na mashabiki wake wanaweza hata kukesha wakishangilia kwa namna zote wanazoweza.
Akizungumza baada ya timu yake kuifunga JKT Oljoro kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kule Geneva ya Afrika, kama jiji hilo lilivyopewa jina hilo na Rais wa Marekani Biol Clinton wakati ule, Jumatano iliyopita kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema: “Tunataka kumaliza msimu kwa kushinda mechi zetu zote. Tulianza na Polisi Dodoma, imekuja JKT Oljoro na sasa inafuatia Simba”. Ni hapo.