Yanga SC leo wanatupa kete yao ya kwanza katika michuano ya Ligi Mabingwa Afrika watakapomenyana na Saint Louis Suns United ya Shelisheli katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajia kuwa mwepesi kwa upande wa Yanga kutokana na timu ya St Louis haina uzoefu wowote katika michezo ya kimataifa hasa hii michezo ya vilabu Bingwa Afrika.
Yanga leo inaanza mchezo wao wa kwanza kuwania kombe hilo la Klabau Bingwa Afrika kwenye raundi ya kwanza ya mtoano ikimkosa mshambualiaji wake hatari, Amissi Tambwe.
Amissi Tambwe, licha ya kupata nafuu ya majeraha yake ya goti, ameondolewa katika kikosi cha timu yake na kutakiwa kufanya mazoezi mepesi ya binafsi.
Tambwe, raia wa Burundi, ameongezewa wiki moja ya kuhakikisha hali yake inaimarika zaidi.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu amesema Tambwe ameongezewa siku hizo baada ya kulalamikia maumivu wakati akifanya mazoezi magumu juzi.
Bavu alisema baada ya kumfanyia vipimo na kuonekana bado hayupo fiti, amemuongezea muda wa kukaa nje ya uwanja na kufanya mazoezi mepesi ya binafsi.
“Tunataka Tambwe akirejea uwanjani awe fiti kwa asilimia kubwa na hiyo ni baada ya hivi karibuni kulalamikia kusikia maumivu wakati anafanya mazoezi na wenzake.
“Ninaamini baada ya wiki moja atarejea uwanjani kwani hivi sasa anapata matibabu huku akiendelea na mazoezi binafsi kwa ajili ya kuwa fiti na kurejea uwanjani haraka,” alisema Bavu.
Wakati huohuo, Bavu alisema beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, ameanza kupata nafuu ya kufanya mazoezi ya ufukweni baada ya kusumbuliwa na maumivu ya misuli.
Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano hiyo, Zimamoto ya Zanzibar ambayo leo inaikaribisha Wolaitta Dicha wa Ethiopia Uwanja wa Amaan, Zanzibar.