Na Robert Mwandumbya
Genilson Santos Santana ‘Jaja’, ambaye kwa sasa ametawala vichwa vya vyombo vya habari, ameifungia Yanga mabao manne katika mechi tano alizocheza. Lakini taarifa nyingine zinasema kwamba katika mazoezi yaliyopigwa Uwanja wa Bandari, Loyola na kule Zanzibar, nyota huyo amefunga mabao zaidi ya 40.
Alisajiliwa Yanga katika dirisha kubwa akitokea timu ya Itabaina ya nchini Brazil. Ni kama alifuatana Coutinho ambaye ni kiungo mshambuliaji. Alipotua Yanga ilikuwa ni gumzo la jiji kwani mashabiki wa Yanga hawakuwapa nafasi ya kupumua wapinzani wao kwa sifa kemkem walizokuwa wakizimwaga kwa mshabuliaji huyo.
Ukigeugeu: Iliwachukua mashabiki wa Yanga muda mfupi kuanza kumbeza mshambuliaji wao huyo kutokana na kile walichokiita “ni mzito.” Mashabiki hawakuwa na subira ya kumpa nafasi ili wajue makali ya mchezaji wao huyo, walianza kumzomea uwanjani huku wakimmwagia sifa Mbrazili mwenzake Coutinho.
Walisikika wakisema kiungo huyo ndiye mahiri kuliko Jaja. Kimsingi mpira uko hivi, kuna kushuka na kupanda kwa kiwango cha mchezaji awapo katika klabu yake husika. Hivyo, inategemea na uwezo wa mchezaji huyo kuweza kukabiliana na hali hiyo ya kushuka kwa kiwango chake kwani ndiyo mapito ya maisha ya uchezaji yalivyo.
Hali kama hii ikitokea, mchezaji aina ya Jaja huhitaji kutuliza akili ili aweze kuitafuta upya fomu yake kama ilivyo kwa kiungo wa Arsenal, Mjerumani Mesut Ozil.
Ukiacha kucheza vema, Jumamosi iliyopita dhidi ya Everton, ukweli ni kwamba Ozil anapitia mapito magumu sana katika maisha yake ya kisoka. Ozil ameshindwa kuonesha makali yake kwani amekuwa katika kiwango kibovu na kushindwa kutoa pasi nzuri za mwisho kama alivyozoeleka kuwa ni ‘mzee wa kutoa pasi za mwisho.
Lakini mashabiki wa Arsenal wanaonekana kuwa watulivu na wavumilivu kwani ni kitu cha kawaida kwa mchezaji kutoka katika fomu.
Kinachoshangaza zaidi kwa Ozil ni kwamba ni miezi miwili tu iliyopita ametokea kutwaa taji la Kombe la Dunia na timu yake ya Ujerumani na medali yake anayo kibindoni. Lakini tangu ametoka katika michuano ya Kombe la Dunia ameshindwa kabisa kuonesha vitu vyake ambavyo mashabiki wamezoea.
Hali kama hiyo naiona kwa Jaja kwa mashabiki wa Yanga kukosa uvumilivu naye kwani awali alionekana hakuwa katika kiwango kizuri kwani alishindwa kufunga mabao, lakini akawabeba kwenye Ngao ya Hisani baada ya kuidungua Azam FC mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0. Bao jingine lilifungwa na Simon Msuva.
Kwa kufunga huko kila shabiki alikuwa akitamka mdomoni Jaja, ambaye Jumamosi iliyopita, amekosa penalti na timu yake kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sukari ya Turiani, Mji Kasoro Bahari. Kinachotakiwa kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa wavumilivu na kuelewa kwamba kuna kipindi mchezaji anapoteza kiwango chake kutokana na mambo mbalimbali ambayo yanatokea nje ya soka.
Baadhi ya mambo hayo ni kushuka kiwango ni kupatwa na msongo wa mawazo kutokana na matatizo ya kifamilia, mahusiano mabaya na kocha au wachezaji wenzake kadhalika mikataba. Kwani hata kocha wao mpya wa hivi sasa Marcio Maximo alikwishawahi kunena kuwa kiwango cha mchezaji hutegemea sana sapoti kutoka kwa mashabiki kiasi cha asilimia 50.
Kinachotakiwa kutoka kwa mchezaji anayesumbuliwa na matatizo ya kushuka kwa kiwango, inatakiwa ajitahidi kupambana na hali kama hiyo ili aweze kuweza kurudisha kiwango. Tumeyaona haya hata kwa wachezaji wengi wanaokipiga Ligi za Ulaya kama Wayne Rooney aliyewahi kushuka kiwango na kutofunga bao lolote kwa kipindi kirefu.
Lakini Kocha wake, Sir Alex Ferguson, enzi hizo aliweza kumuamini na kuendelea kumpanga mpaka alipoweza kurudisha kiwango chake hicho kama zamani na sasa ni tegemeo kubwa kwa timu yake ya Manchester United na ndiyo nahodha wao kwa sasa.