Unatazama taarifa za habari za michezo za Ulaya, unasoma juu ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na matajiri wa Urusi na Uarabuni. Siku moja ya uhai wako inapita ukiwa na afya njema, kesho asubuhi unatazama tena runinga na kukutana na habari ya matajiri kutoka Marekani kuwekeza kwenye klabu za Ulaya na Asia.
Unasoma habari za timu ambazo miongo michache iliyopita zilikuwa na maisha ya kawaida tu yasiyo na mahusiano na mabilioni ya fedha za matajiri.
Nyakati ambazo Pele, Eusebio na Maradona walitamba, hazifanani na hizi za Cristiano Ronaldo, Lionel Messi au Paul Pogba. Lakini kwa hapa Tanzania bado zipo zile fikra zenye kutaka kuzifanya nyakati za kina marehemu Maulid Dilunga zifanane na hizi za kina Simon Msuva.
Wapo ambao aidha ni kwa kutokuwa na ufahamu wa dunia ya sasa au ni kwa sababu ya kutumiwa na watu wachache, wamejikuta wakishindwa kabisa kuondokana na mitazamo ya kizamani. Wapo Yanga, pia wapo Simba. Wapo Stand United, pia wapo Coastal Union. Hawawezi hata kutambua ni kwa namna gani wanavyozidi kuchelewa kwa sababu nyakati zimesonga sana.
Hawawezi wakapoteza hata nusu saa katika kujiuliza ni kwa namna zipi Taifa Stars yenye kutegemea wachezaji wanaokuzwa kwenye mazingira yale yale ya miaka yote, itaweza kweli kupambana na Algeria au Nigeria.
Wanachama takriban 700 wa Simba waliongozwa na hamu ya mabadiliko ndiyo maana walikuwa tayari kuridhia kumwachia Mohamed Dewji asilimia 49 ya umiliki wa timu baada ya kuwa radhi kuwekeza Sh bilioni 20.
Msukumo uliowasukuma wanachama hao ni kule kuchoshwa na mauzauza yanayojirudia kila msimu. Lakini haina maana kwamba ndani ya Simba hakuna watu ambao kama Simba ingekuwa inafanya vizuri uwanjani, basi wangekuwa tayari kulipinga wazo la Mo Dewji.
Wakati yupo Yanga, Yusuf Manji, alikuja na wazo la kutaka kuikodisha klabu hiyo. Upo uwezekano kuwa wazo hilo lilikuwa na upungufu wa namna moja au nyingine. Hakuna kinachopangwa na mwanadamu halafu kikakosa sifa ya kukosolewa au kuongezewa ubora kutokana na maoni ya watu wengi.
Wazo la Yusuf Manji lilizaliwa baada ya uhalisia wa mambo ndani ya Yanga, hasa jinsi ambavyo fedha nyingi inayotumika katika kuendesha timu isivyoweza kurudi, hapo inamaanisha kuna mtu anayepata hasara.
Anayekwenda benki kwenye akaunti yake na kutoa fedha kwa ajili ya wachezaji wa Yanga au wa timu yoyote ile, anakuwa amekubali maisha yake binafsi na mipango yake iweze kuathirika kwa faida ya kile kinachopendwa na wengi.
Mwanachama au shabiki wa Yanga, hata kama kila mechi inapochezwa pale Uwanja wa Taifa anakuwa tayari kuingia uwanjani, atambue kuwa gharama za maisha zinapanda kila kukicha.
Leo hii mchezaji wa kawaida tu ambaye ni mzalendo aliyekuzwa kibahati bahati, anakuwa tayari kutaka dau la Sh milioni 30 ili aweze kusaini fomu za usajili.
Vipi kuhusiana na gharama za kuwaleta David Molinga, Lamine Moro, Tshishimbi na wengineo? Vipi kulipia gharama zote za kuwasajili na mishahara yao? Vipi kuhusu gharama za kupeleka timu kambini? Yanga ni timu yenye hadhi kubwa katika ukanda huu wa Afrika.
Lakini kwa tabia hii ya mtu mmoja kuachiwa mzigo wa kuendesha timu, halafu akitaka kuweka mazingira yenye faida kwake na kwa wanachama wengine anawekewa kauzibe, kwa kweli Yanga itabakia kuwa ni timu kongwe tu. Yanga itakapoyumba kifedha, itakimbiwa na wachezaji ambao msimu uliopita wamefanya kazi ya maana sana.
Yanga hii itarudi kule kule kwenye maisha ya kimaskini, licha ya kuwa na hadhi na kila sababu ya kufanana na timu kubwa za Afrika. Haina maana kusema kwamba wale wanaofadhili watafaidika na Yanga kuliko ambavyo timu itafaidika, wakati hakuna mbadala wa wazo lake.
Wakati hakuna akili mpya zenye kuiona Yanga ikiwa katika anga za ubora mkubwa zaidi, Wana Yanga wanayo kila sababu ya kukumbushwa kwamba kubomoa nyumba hata kama ni ya ghorofa tano, ni kazi rahisi sana kuliko kujenga ya ghorofa moja tu.
Aina yao ya mitazamo iliwachosha wanachama na mashabiki wa Simba kiasi cha kuona ni jambo la busara kwa timu kuingia katika mfumo wa kampuni.
Isije kuwa njaa za mtu mmoja mmoja, mwenye ushawishi miongoni mwa wanachama wakati wanafanya mikutano yao, ndiye chanzo cha timu kukosa mkakati wa kimaendeleo. Naamini kwamba Yanga ya sasa inastahili mjadala mpana sana, lakini wazo linapopingwa, basi yawepo maisha chanya ya uendeshaji wa Klabu ya Yanga.
Isiwe ni kupinga kwa sababu watu wachache wameshazoea neema za kimaisha kwa sababu wapo karibu na Yanga. Tunapoiongelea Yanga tunaongelea taasisi kubwa. Siku zote wanachama wa taasisi huzaliwa, hukua na hufa, huku wakiiacha taasisi ikiendelea kustawi kadiri ya ubunifu na uwezo wa ufanisi wa wenye kuipenda.
Vinginevyo Yanga inaweza kuja kutimiza umri wa miaka 100 huku ikiwa haina mafanikio yoyote kimataifa, na ikijivunia Uwanja wa Kaunda usio na tija kwa sasa na jengo lake, bila ya kuwa na kipya chenye kulingana na umri huo mkubwa.
Mwana Yanga aumizwe na kudumaa kwa timu yake, na asifikiri kuwa kurudi kwenye hali ya kawaida ni jambo lisilowezekana. Ni rahisi sana kurudi katika ile hali ya kuwa wa mchangani kama hakuna mikakati sahihi ya kubakia katika hali ya kuwa wa kimataifa.