Hatua ya uongozi wa Yanga kuingia mkataba na kampuni ya kimataifa ya ujenzi inayojulikana kama Beijing Constructions ya China, imezidi kuwapiku mahasimu wake wakubwa wa soka nchini, Simba, kutokana na kuendelea kuwazidi kete ya mafanikio ndani na nje ya uwanja.
Unyanyasaji wa Yanga kwa Simba, ulianzia kipindi cha usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara, hatua iliyosababisha Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, kushindwa kuongea na waandishi wa habari aliowaita mjini Dodoma na badala yake akaishia kuchuruzikwa machozi.
Rage aliangua kilio hicho baada ya Yanga kuinyang’anya Simba tonge lililokuwa tayari kinywani mwake, kwa kumsainisha ‘kininja’ beki wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbuyu Twite, ambaye awali alimsainisha mkataba mjini Kigali, Rwanda.
Mbuyu alisainishwa na Rage kuja kuchezea Simba akitokea APR ya Rwanda na kumlipa dola 30,000 za Marekani, sawa na Sh milioni 45 za Tanzania, lakini siku chache baadaye akaiacha solemba na kusaini fomu za Yanga kwa kitita cha dola 50,000 za Marekani, sawa na Sh milioni 75 za Tanzania.
Awali, Yanga pia iliifanyia Simba umafia kwa kuinyang’anya beki wake tegemeo wa kati, Kelvin Yondani, ambaye alisaini mkataba na timu hiyo ya Jangwani, Dar es Salaam, huku Wekundu wa Msimbazi (Simba) wakidhani ni utani.
Hayo yote yanakuja huku Simba ikiendelea kuwa bingwa wa kutoa hadithi za alinacha kwa mashabiki na wanachama wake, zinazotolewa na Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), hali inayosababisha baadhi yao wamtuhumu kwamba anatumia uongozi huo wa soka kufanikisha zaidi malengo yake ya kisiasa.
Mbali ya hayo, Mwenyekiti huyo wa Simba pia alitangaza kuwa klabu hiyo ingejenga uwanja wake huko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uwanja huo ulitarajiwa kujengwa na kampuni moja ya Uturuki na ramani yake aliitoa nchi ya Misri, ambako alikwenda kuiongoza Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF), wakati huo ikiiwakilisha Tanzania Bara.
Kushindikana kwa ahadi hizo zote huku Yanga kwa upande wake ikifanikisha kila jambo nje na ndani ya dimba, ndiko kunasababisha wanachama na mashabiki wa Simba kunyanyasika kwa vijembe, kebehi, masimango na kila aina ya kejeli kutoka kwa mahasimu wao hao.
Kasi ya mafanikio ya Yanga imeongezeka tangu kuchaguliwa kwa uongozi mpya chini ya mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji. Ulianza kuiongoza timu hiyo kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati au Kombe la Kagame na kusajili wachezaji.
Baada ya kuinyang’anya kama utani mabeki wawili mahiri uwanjani, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, Yanga iliyoanza kwa kusuasua katika michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, ilisema ingeikamata Simba iliyoanza kwa kishindo kwa kuvuna pointi tatu kila mechi.
Kocha Msaidizi wa klabu hiyo, Fred Felix Minziro Majeshi Kataraiya ndiye alisema timu yake ingeikamata Simba na kuipita, kauli ambayo imeshatimia.
Mbali ya Yanga na Simba, timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ni Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Ruvu Shooting, JKT Mgambo, JKT Oljoro, JKT Ruvu, Polisi Morogoro, Tanzania Prisons, Azam FC, African Lyon na Toto African.
Aidha, kwa upande wake, Yanga imeanza upembuzi wa awali wa ujenzi wa uwanja wake eneo la Kaunda utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 40,000. Uwanja huo utaifanya timu hiyo kuwa ya pili kumiliki dimba lake hapa nchini ikitanguliwa na Azam FC yenye Uwanja wa Chamazi Complex, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya mashabiki waliozungumza na JAMHURI wameonesha kuguswa mno na ujenzi huo na kuwapongeza viongozi wa Yanga kwa kubuni kiuchumi hicho.
Wamesema hata kama Simba ingefanikiwa kujenga uwanja wake huko Bunju bado ungekosa mahudhurio ya kuridhisha kwani ingekuwa vigumu kwa mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Jijini la Dar es Salaam na vitongoji vyake kwenda kuangalia mechi kutokana na umbali uliyopo. Hata hivyo, bado Simba haijapoteza matumaini ya kufanya vizuri kisoka katika siku zijazo.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu ikiwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 24 na Simba inayotetea ubingwa ikiwa na pointi 13.
Timu nyingine na pointi zake zikiwa kwenye mabano ni Mtibwa Sugar na Coastal Union (22 kila moja), Kagera Sugar (21), JKT Mgambo na Ruvu Shooting (17 kila moja), JKT Ruvu (15), Tanzania Prisons na JKT Oljoro (14 kila moja), Toto African (12), African Lyon (9) na Polisi Morogoro (4).