Kila upande wa mabingwa wa kandanda Afrika Mashariki na Kati, Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake makuu katika mitaa ya Jangwani na Twiga jijini, unaelekea kukabiliwa na jinamizi la kisaikolojia.
Wachezaji wa zamani na wapya kila mmoja ameathirika. Benchi la ufundi na uongozi pia vimeathirika. Hilo ndilo jinamizi linaloitafuna klabu hiyo ya soka.
Wachezaji maarufu – Haruna Niyonzima, Athumani Idd Chuji, Oscar Joshua, Nadir Haroub Cannavaro, Khamis Kiiza na wengineo wanapokuwa uwanjani huwa na mchecheto kwamba wasipocheza vizuri watanyang’anywa namba zao na wapya na hivyo “kuozea” benchi.
Wanacheza huku vichwani mwao wakiyafikiria maneno na vitisho walivyopewa na kocha wao, Mbelgiji Tom Saintfiet, kwamba atakuwa anapanga kikosi chake kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji kwa kuzingatia zaidi uwezo wa kila mchezaji na si jina lake nje ya uwanja.
Wanakuwa na mchecheto wa miguu utadhani wameingiwa na ganzi na kushindwa kuamua kwa haraka wafanye nini ili kutopoteza mpira. Wanakosa uamuzi makini wa kupiga chenga, kutoa pasi kwa nani ama wabaki nao.
Kwa mfano, washambuliaji wanashindwa hata kuamua kama wapige mashuti golini kutafuta mabao au watoe pasi, kisha watafute mahali pazuri na kujipanga kwa ajili ya kutafuta nafasi ambayo wakipenyezewa krosi wanafunga kwa uhakika. Mbali ya washambuliaji na mawinga wa pande zote mbili za kushoto na kulia, hali inakuwa ngumu pia kwa walinzi wa pembeni na kati.
Kila mmoja anacheza kwa hofu kwamba iwapo adui atapitia kwake, kisha akaenda kuifungia bao timu yake atakuwa amejitakia benchi mwenyewe. Anahofu kuwa kocha wake, wachezaji wenzake, uongozi na mashabiki wa Yanga hawatamwamini tena.
Ndivyo ilivyo pia kwa viungo, kwamba nao wanacheza kwa namna ileile. Wanakuwa na mchecheto uleule. Wanacheza huku wakiwaza kuwa wasipogawa vizuri mipira “kuwalisha” vyema washambuliaji na kuwaunganisha au kuwasaidia mabeki kikamilifu kulinda goli lao, watakuwa wanajiweka rehani wenyewe.
Licha ya wachezaji hao wa zamani, hata waliosajiliwa msimu huu akina Didier Kavumbagu, Nizar Khalfani, Saidi Bahanuzi, Mbuyu Twite au Simon Msuva, Kelvin Yondani na wengineo wana hali ileile ya mashaka, wasiwasi, mchecheto na kutojiamini.
Wanacheza mpira ili kuonesha kwamba kelele na mbwembwe zote, majigambo na tambo nyingi zilizokuwapo wakati wa kusajiliwa kwao na timu hiyo zinathibitika kwa vitendo kwa kufanya kile walichotarajiwa na si vinginevyo.
Wanacheza soka huku wakisikiliza kelele za mashabiki jukwaani, wanaangalia mwitikio juu yao ili kuona kama wanashangiliwa kwa kukubalika ama wanazomewa. Wanakuwa na ‘viwiliwili’ viwili – kimoja kinakuwa nje ya uwanja na kingine kinachocheza uwanjani.
Wanajua kuwa walisajiliwa kwa fedha nyingi na mishahara wanayolipwa ni minono, wengine ikiwa mikubwa zaidi kuliko wachezaji waliowakuta katika klabu hiyo kwa sababu wanatarajiwa kufanya mambo makubwa.
Wanacheza huku wakijiuliza itakuwaje wakishindwa kuonesha viwango walivyotarajiwa kuonesha. Wanawazia hatima zao endapo watashindwa kuthibitisha uhalali wa “mafungu” yaliyotumika kuwasajili na kuhalalisha ukubwa wa mishahara wanayolipwa.
Hali hiyo inamkabili pia Kocha Saintfiet aliyeingia na tambo za kuibadili Yanga. Aliahidi kuwa angeifanya iwe timu kali uwanjani na yenye umaarufu wa pekee katika Bara la Afrika. Pia kingekuwa kikosi cha ufundi zaidi, bora zaidi na mahiri kwa mabao kuliko alivyokikuta mwezi Juni mwaka huu.
Kocha huyo ambaye hata hivyo alitimuliwa Jangwani wiki iliyopita, alitamba kuwa analijua vizuri soka la Afrika na jinsi lilivyojaa kila aina ya furaha na karaha. Kwamba ana uzoefu nalo wa miaka mingi kutoka mataifa tofauti yakiwamo ya Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Ethiopia alikofundisha hadi timu za taifa.
Anajiuliza kama ahadi zake hizo ikiwamo ya kuifanya Yanga kuwa mashine ya kupachika mabao na kutoka na ushindi zitatimia au zitabaki mdomoni. Hajui itakuwaje akishindwa kuthibitisha hayo aliyoyaahidi mwenyewe, hivyo inawezekana anapanga timu kwa wasiwasi na hofu.
Anatafakari kuhusu hatima yake kama itakuwa ya kujivunia au huenda ikafanana na ya wengi waliotangulia kupewa kazi hiyo Jangwani kabla yake, wakapokelewa kwa nderemo na vifijo lakini hatimaye wakaishia kutimuliwa mithili ya mbwa koko.
Ukimwondoa kocha na wachezaji wake, viongozi nao wanajiuliza maswali mengi, lakini kubwa kuliko yote ni kama usajili waliofanya ukiwamo wa ugomvi nje na ndani ya nchi hii una tija yoyote au walifanya hivyo bila ya utafiti.
Mathalani, kusajiliwa kwa watu kama Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu kulitokana na “ubora” waliouonesha walipokabiliana na Yanga wakati wa michuano ya Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam, lakini hawakuwahi kuwaona wakizichezea timu zao kwenye ligi za ndani huko Rwanda na Burundi.
Kwa mfano, inaelezwa kwamba Kavumbagu alisajiliwa baada ya kuifunga Yanga katika mechi ya kwanza ya timu hiyo ilipochapwa na Atletico de Burundi mabao 2-0 huku yote akifunga yeye. Hapo ndipo alipoonekana ‘mchezaji mkubwa na hatari’ na kuanza kufukuziwa hadi Bujumbura.
Kabla ya kucheza mechi ile ya kwanza ya Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons siku 11 zilizopita, Yanga iliahidi kuzoa pointi zote tatu na kuanzia hapo kushinda mfululizo kwa timu zote inazokwaana nazo, ili kujitengenezea mazingira bora zaidi ya kuja kuwa bingwa.
Tofauti na tambo zake hizo, Yanga ilitoka suluhu na timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu na mara moja kusingizia ubovu wa uwanja huo, lakini ikaahidi kuanza kuonesha soka la kiwango kikubwa.
Iliahidi kufanya hivyo ikianzia mechi ya pili dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Jumatano iliyopita, huku mshambuliaji wake mpya, Saidi Babanuzi akisema angekwenda ‘kufia uwanjani’ ili kuonesha umahiri wake ili kufufua matumaini yake ya kutaka kuwa mfungaji bora wa msimu huu.
Nani hafahamu kilichotokea huko? Huko ilichezea kichapo cha aina yake, ikakosa hata pointi moja kama ilivyobahatisha Mbeya huku mabingwa watetezi wa ligi hiyo ambao pia ni mahasimu wao wakubwa wa soka nchini, Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya jijini, wakizidi kujitanua kileleni kwa kushinda mechi mbili mfululizo.
Nini kinachoihangaisha Yanga kama si kuathirika kisaikolojia kila upande kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wake?