Na Isri Mohamed
Baada ya kumaliza kibarua chao dhidi ya CR Belouizdad kwa kuwapa kichapo cha mabao manne kwa nunge yaliyowafikisha hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika, klabu ya Yanga inatarajia kusafiri leo kuelekea nchini Misri kwa ajili ya kukamilisha ratiba kwa kumalizia mchezo mmoja dhidi ya AL Ahly.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa habari wa Yanga, Ali kamwe, ameelezea maandalizi ya safari yao kwenda mchezo katika mchezo huo utakaochezwa Ijumaa ya Machi 01, 2024.
“Kuna watu wanasema tunakwenda kutembelea Pyramids na kununua kanzu, nafikiri mmeona namna ambavyo tumejiandaa kwenda kwenye mchezo huo, maandalizi haya sio kwa ajili ya kwenda kutalii ni kwa ajili ya kwenda kupambana hata kama tumeshafuzu. Tunataka kuongoza kundi, ili tupate faida ya kuanza mchezo wetu wa robo fainali ugenini, tunataka kucheza na walioshika nafasi ya pili.”
“Timu inatarajia kuondoka saa 11:55 jioni kuelekea Misri, tutaondoka na shirika la ndege la Ethiopia na kufika saa 2:33 usiku, kisha tutaondoka Ethiopia na kuwasili Cairo saa saba usiku kuamkia kesho. Timu itafikia Royal Kempinski Hotel.
“Tutaondoka na msafara wa watu 60, msafara huu umegawanyika makundi matatu, wachezaji 24, benchi la ufundi 13, na Watendaji, maofisa wakuu wa klabu 23” amesema Kamwe
Mpaka sasa kwenye kundi ‘D’ Al Ahly ndiye anayeongoza akiwa na alama tisa, akifuatiwa na Yanga mwenye alama nane, Belouizdad alama 5 na Medeama akishika mkia na alama nne.