Mashabiki wa Yanga wanalia. Wengi wanazungumza mambo mengi hasa katika kile kinachoendelea ndani ya klabu hiyo kwa sasa. Kisa ni sakata la klabu na Kampuni ya GSM ambayo iliamua ‘kujitolea’ kuwasaidia.

Katika kipindi hiki ambacho dunia imejaa hofu ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona (au COVID-19), mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga nao wamo katika hofu juu ya mustakabali wa klabu yao.

Wameacha kuizungumzia corona kwa muda, wanajadili mustakabali wa klabu yao pendwa. Hapa ndipo utakapojua tofauti ya mapenzi na mahaba! Mashabiki wanalia, wengi wamelalamika mno. Wanajua Yanga ilipotoka na ilipo kwa sasa na huku wakiitazama Simba, ndo’ machozi yanawatiririka.

Kisa?

Hilo lilikuja baada ya Kampuni ya GSM kuwasilisha barua ndani ya uongozi wa Yanga, ikieleza dhamira yao ya kusitisha kutoa misaada iliyo nje ya mkataba wao.

Lakini GSM walifanya hivi baada ya baadhi ya viongozi ‘kuropoka’ katika vyombo vya habari wakiituhumu kampuni hiyo kwa kukwepa majukumu yake, huku pia wakidai wachezaji kupunjwa stahiki zao zinazotolewa na wadhamini hao wa jezi.

Uamuzi wa uongozi

Uongozi wa Yanga uliamua kuwasimamisha wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji, Salim Rupia na Frank Kamugisha kuanzia Machi 27, mwaka huu hadi hapo mkutano mkuu utakapofanya uamuzi kwa mujibu wa katiba.

Bosi wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alikiri kufikiwa uamuzi huo baada ya kikao cha siku mbili mfululizo kilichofanyika Dar es Salaam kuanzia Machi 26 hadi Machi 27.

Pia Kamati ya Utendaji ya Yanga ilipokea na kukubali maombi ya wajumbe wengine watatu, Rodgers Gumbo, Shijja Richard na Said Kambi kujiuzulu nafasi zao na kwamba nafasi ya mjumbe wa kuchaguliwa itajazwa mara moja kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya Yanga.

Yanga waipigia magoti GSM

Kutokana na hilo, Yanga imeamua kuipigia magoti Kampuni ya GSM kuhusu mpango wao wa kutaka kujitoa udhamini wa masuala yasiyo ya kimkataba.

Dk. Msolla amekiri barua hiyo imewasilishwa baada ya uamuzi wa pamoja wa kikao cha Kamati ya Utendaji.

Sasa Kamati ya Utendaji Yanga inabaki na wajumbe watano wa kuchaguliwa ambao ni Hamad Islam, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba, Dominick Ikute, Arafat Haji na Saad Khimji pamoja na Dk. Athumani Kihamia pekee wa kuteuliwa chini ya Mwenyekiti Dk. Msolla na Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela.

Wanena

Mmoja wa wajumbe waliojiuzulu, Shijja Richard amesema, ameamua kwa hiari yake kujiuzulu nafasi zote za uongozi katika klabu yake ya Yanga.

“Yanga ni kubwa kuliko mimi na kuliko mtu yeyote. Yamezungumzwa mengi, lakini mimi sitazungumza chochote. Wakati utaongea. Ukweli hata usipousema, huwa una tabia ya kujitokeza wenyewe japo taratibu, lakini huwa unadumu

milele.

“Nimeamua kwa ridhaa yangu mwenyewe kujiuzulu nafasi zangu zote za uongozi ndani ya Yanga. Yanga ni taasisi kubwa kuliko mimi Gumbo, hivyo basi katika kuwajibika kwangu aidha niwe nimefanya au sikufanya kosa, nimeamua kukaa pembeni ya uongozi ili kuiacha Yanga ikiwa salama,” anasema Gumbo.

Kinachowaponza

Yanga kwa sasa inaonekana kama kuna kuzungukana wenyewe kwa wenyewe, kwani kuna baadhi ya watu wanaona kuna wenzao wanafaidika kupitia Kampuni ya GSM na wengine ‘wakilala njaa’.

Hata madai ya baadhi ya wachezaji kudai katika fedha Sh milioni 200 walizoahidiwa na GSM wakiifunga Simba, zimekuwa ndoto kwao na hakuna chochote wanachoona zaidi ya wengi wao kupewa fedha pungufu kuliko kile walichopaswa wapewe.

Wanadai wamejikuta katika wakati mgumu, kwani motisha waliyotakiwa wapewe ‘imekwenda kwa viongozi’ na hapo ndipo baadhi ya viongozi wakaanza kutilia shaka uwepo wa GSM ndani ya klabu hiyo.

Uongozi wajibu mapigo

Katibu Mkuu wa Yanga, David Ruhago, amewaruka wote wanaolisemea suala la mgawo na kusema suala hilo la mgawo wa fedha kwa wachezaji wa Yanga wanapopata ushindi halipo kwenye mkataba, hivyo hawapaswi kulalamika.

Kwenye mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa Machi 8, Uwanja wa Taifa na Yanga kushinda kwa bao 1-0 wadhamini wa Yanga ambao ni GSM waliahidi Sh milioni 200 kwa wachezaji iwapo wangeshinda mchezo huo.

Habari zinaeleza kuwa wachezaji waliopewa mgawo wa fedha ni wale waliokuwa kwenye kikosi kilichocheza uwanjani na baadhi ya wachezaji ambao hawakucheza, jambo lililoibua mpasuko ndani ya timu.

“Kuna haki za wachezaji, hamasa na zawadi, leo nikiamua kutoa zawadi ya chupa moja hakuna mtu atakayelalamikia suala la hamasa nani amepata, ni mgawo lilifanyika na mtoa zawadi alitoa katika kuboresha lakini haimo katika mkataba.

“Hilo linalotembea kwenye mitandao kuhusu nani kapewa nini ni jambo la kawaida katika namna ya kuhamasisha lakini si sehemu ya mkataba kwamba lazima upewe. Ni mambo ya kawaida na yanazungumzika,” alisema Ruhago.

Msolla ashutumiwa

Wanachama wa Yanga hasa wa Tawi la Buguruni wamemshutumu Mwenyekit wao, Dk. Mshindo Msolla wakidai hana ubavu wa kuwakemea viongozi wanaoichafua GSM kutokana na upole wake.

Kwa nyakati tofauti wamemtaka Msolla kuhakikisha anasimama imara, kwani Yanga ni taasisi kubwa na inayopaswa isonge mbele hata kama kwa kuwaacha njiani wengine.

Ushauri

Ni vema Yanga ikajitambua ilipo na kuachana na migogoro inayoanza kujitokeza, kama ni juu ya mkataba wa GSM heri kuondoa shaka na kuuweka wazi ili watu wajue.

Lakini pia kama mtu anajitolea fedha zake nje ya mkataba hauna haki ya kudai, hiyo si lazima na iwapo GSM ilikuwa inafavya hivyo ilikuwa kwa mapenzi yake yenyewe na si kitu cha kulazimishwa, huku wachezaji nao wakipaswa kuelimishwa juu ya mikataba yao inavyosema.

Hii ndiyo Yanga inayowatia hofu mashabiki wake, huku wakiwa pia na hofu ya corona.