DAR ES SALAAM
Na Andrew Peter
Mabingwa mara 28 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, sasa wanahitaji kushinda mechi nne ili kumaliza msimu na rekodi ya kutokufungwa.
Yanga ilitangaza ubingwa wa ligi wiki iliyopita baada ya kuifunga Coastal Union mabao 3-0 na kufikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
Ila Yanga wanapaswa kushinda mechi tatu zilizobaki pamoja na ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Coastal Union ili kuivunja rekodi ya Simba (2009) na Azam (2014) walipotwaa ubingwa wa ligi bila kufungwa.
Hakuna shaka Yanga msimu huu ilijipanga vizuri tangu mwanzo wa msimu na kuweka mikakati imara kuhakikisha wanamaliza utawala wa Simba wa misimu minne ya kunyakua mataji yote ya ndani.
Yanga chini ya Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla na wadhamini GSM, waliamua kuziba masikio kwa mambo ya nje ya uwanja, hasa kelele za mashabiki na kumpa nafasi Kocha raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi na benchi lake kutimiza majukumu yao kwa uhuru.
Nabi amefanya mabadiliko makubwa kwa uchezaji wa Yanga katika msimu huu wakionekana kucheza pasi nyingi na kujiamini huku akitoa nafasi kwa nyota wengi kuonyesha uwezo wao.
Siri kubwa ya mafanikio ya Yanga ni ubora wa safu yake ya ulinzi. Ngome hiyo chini ya uongozi wa kipa kutoka Mali, Djigui Diarra na nahodha Bakari Mwamnyeto, imeruhusu mabao saba tu katika michezo 27, ikifuatiwa na safu ya ulinzi ya Simba iliyoruhusu mabao 12 katika mechi 26 walizocheza.
Uimara wa safu ya ulinzi umeifanya Yanga kuwa na uwezo wa kulinda ushindi wake wa aina yoyote ilipoupata, jambo lililoleta amani hata kwa wanachama na mashabiki waliokuwa wakijitokeza kwa wingi viwanjani kuishuhudia timu yao.
Mbali na safu ya ulinzi, pia kiungo mkongwe, Khalid Aucho (Dokta wa Mpira) na mshambuliaji Fiston Mayele wamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya mabingwa hao wa kihistoria.
Aucho ni injini muhimu katikati akiwa na uwezo wa kuituliza timu na kuchezesha vizuri wenzake. Alipokuwa akikosekana raia huyu wa Uganda, ni wazi ulikuwa unaiona safu ya kiungo ya Yanga inayumba.
Mshambuliaji Mayele ametimiza jukumu lake kwa asilimia 100 akiwa amefunga mabao 16. Hadi sasa ndiye kinara wa ufungaji, mbali ya kufunga pia ametengeneza mabao manne.
Mayele katika mechi tatu zilizosalia atakuwa na kazi moja tu; kuhakikisha anafunga kila mechi ili kunyakua kiatu cha dhahabu anachogombea na mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole, mwenye mabao 15 hadi sasa.
Simba, Azam zaibeba
Waswahili wanasema: “Unamsifu ana mbio… anayemkimbiza ni nani?”
Ndilo swali tunalopaswa kujiuliza kwa sasa. Wakati Yanga wanapata sifa hizo, washindani wao wakubwa katika mbio za ubingwa Simba na Azam walikuwa na hali gani?
Hakuna ubishi kwamba Yanga imenufaika sana na udhaifu wa wapinzani wao msimu huu. Simba waliokuwa mabingwa watetezi tangu mwanzo wa msimu baada ya mdhamini na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini atangaze kujiweka kando, hali ya timu ilipoteza mwelekeo.
Uamuzi wa Mohamed Dewji ‘Mo’ kujiweka kando ilikuwa ni habari njema kwa Yanga, maana ndiye mtu aliyewasumbua kwa miaka minne ya kukaa bila taji, huku timu yake ya Simba ikipoteza dira kidogo kidogo uwanjani na kushuhudia mabingwa wakimaliza msimu mzima bila kukaa kileleni mwa ligi.
Wakati Simba ikipotea hivyo, matajiri wa Chamazi, Azam FC, nao walianza vizuri ligi, lakini majeraha ya nyota wake Mzimbabwe Prince Dude pamoja na uamuzi wa kumtimua kocha ni wazi kulionekana kuiyumbisha timu.
Azam pamoja na kuwa na wachezaji wengi nyota, ni moja ya timu zilizofungwa mabao mengi, 27, hadi sasa, huku ikipoteza mechi tisa za ligi. Pigo kubwa kwao ni kuondolewa katika nusu fainali ya Kombe la ASFC na Coastal Union.
Udhaifu wa Simba na Azam umeisaidia Yanga kukusanya pointi nane kutoka kwao, wakitoka suluhu mara mbili dhidi ya watani wao wa jadi huku wakishinda mara mbili dhidi ya Wanalambalamba.
Nabi ajipanga upya
Rekodi za Yanga katika mashindano ya kimataifa ni wazi ndicho kitu pekee kinachomtesa Kocha wao Nadi, pamoja na mashabiki wa mabingwa hao wapya wakati msimu ukielekea mwishoni.
Tayari mashabiki wa Simba wanawakebehi kwa kusema Yanga itakwenda kutia aibu taifa katika mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Ni wazi Kocha Nabi anapaswa kubadilisha aina ya uchezaji wa timu yake ili kuendana na kasi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, la sivyo aibu ya kuondolewa mapema itawakuta.
Yanga pamoja na kuchukua ubingwa bila kupoteza mchezo, ni timu inayocheza kwa kasi ndogo, hasa inapofanya mashambulizi yake, jambo ambalo litawapa wakati mgumu katika kufanikisha ndoto yao ya kucheza hatua ya makundi kutokana na aina ya ushindani.
Kocha Nabi anasema: “Tutakapokuwa na timu bora ya mashindano ya CAF, moja kwa moja tutakuwa na timu nzuri ya kucheza Ligi Kuu. Ndoto yangu haitofautiani sana na uongozi wa klabu, wote tunataka mafanikio makubwa msimu ujao.”
Hiyo itafikiwa iwapo watafanya usajili kwa kuongeza wachezaji wengi wenye kasi, pia kuitengeneza safu bora ya ushambuliaji itakayoweza kufunga mabao mengi nyumbani na ugenini.
Pia, ili kufanikiwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa ni lazima Yanga wakubali kuiga mazuri ya Simba ya kuhakikisha hawapoteza kizembe kwenye uwanja wa nyumbani, kwani ushindi wa nyumbani umekuwa ni nguzo muhimu ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
0655 413 101