Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, alitoa kauli kali akikemea mtindo wa Tanzania kugeuzwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ katika sekta ya michezo kimataifa.
Kauli hiyo aliitoa akionyesha kuchukizwa na matukio ya kushindwa mfululizo kwa timu za taifa za michezo mbalimbali karibu katika kila mashindano zinayoshiriki, yawe yamefanyika Tanzania, Afrika au nje ya Afrika.
Kwa zaidi ya miaka 30 sasa kauli hiyo ya mzee Mwinyi imeendelea kuwa jinamizi kwa timu za Tanzania, kwani hakuna hatua yoyote ya kujisifia iliyofikiwa na timu zetu, ukiondoa timu ya taifa ya soka ya wanawake ambayo mara kadhaa imekuwa ikijitutumua japo kidogo.
Awamu zote za uongozi zilizopita hazijaonyesha jitihida za kuridhisha katika kulikwamua taifa kutoka katika ‘jinamizi’ lililoachwa na kauli ya mzee Mwinyi, huku juhudi zikitelekezwa ama kwa wanamichezo/wasanii binafsi au kwa vyama vya michezo chini ya BMT bila rasilimali fedha ya kutosha.
Pamoja na kelele za wananchi kuiomba serikali kuingilia kati katika kuboresha michezo, hasa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali vinavyodaiwa kuwapo nchini, ni kama serikali za awamu zilizopita ziliamua kutelekeza sekta hii kana kwamba hazioni umuhimu wake.
Kuna wakati, kwa mshangao wa wengi, serikali ilizuia kama si kuachana na michezo ya shule za msingi na serikali bila kutoa maelekezo stahiki; ingawa kelele nyingi zilipigwa kuikumbusha kuwa vipaji vingi vya wanamichezo wa miaka ya 1970, 1980 na hata 1990 vilitokana na michezo hiyo pamoja na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Lakini hatimaye mwaka huu, mashindano ya shule za msingi na sekondari, yaani Umitashumta na Umiseta, yamerejeshwa yakiwa yamefanyiwa uboreshwaji mkubwa na sasa yanaendelea baada ya kufunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wiki iliyopita.
Zaidi ya watoto 7,000 kutoka mikoa yote ya Tanzania wapo Mtwara kushiriki mashindano hayo ya kwanza ya aina yake katika miaka ya hivi karibuni.
Hii ni hatua kubwa sana kuwahi kupigwa katika sekta ya michezo nchini, na kwa hakika kukusanya watoto 7,000 pamoja, mbali na lengo kuu la kuwashindanisha ili kupata vipaji vya wanamichezo mbalimbali, pia ni kuwajengea moyo wa kizalendo na kukuza udugu miongoni mwao.
Tunaamini kuwa vijana watakaopatikana, au timu za taifa zitakazoundwa kutokana na mashindano haya na mengine yajayo, zitatunzwa na kuendelezwa badala ya kutelekezwa ili baadaye Tanzania iwe na wanamichezo imara, waliopikwa na kuiva tayari kuliwakilisha taifa; tofauti na sasa ambapo wanamichezo wetu wametokana na vipaji na juhudi binafsi zao na wadau wachache.
Wizara tatu zinazohusika katika suala hilo ziweke kanzidata itakayotumika kuwakusanya mara moja watoto hawa kila wanapotakiwa na kuendelezwa badala ya kuagana nao Mtwara na kuwasahau.